Friday, July 13, 2018
Dalili kumi na tatu za mwanamke mjamzito
MWANAMKE anapopata ujauzito kwa kawaida huwa anaanza kuona dalili ambazo si za kawaida. Na ni wakati huo ambao ni muafaka kwake kuanza kuuchunguza mwili wake.
“Homoni zinazosambaa mwilini mara tu unapopata ujauzito husababisha mabadiliko kadhaa katika mwili wake ambayo yanaweza kugundulika kabla hata ya uchunguzi halisi wa kujua kama mjauzito au la,” anasema Melissa Goist, Profesa na Mtalaama wa Masuala ya Uzazi wa Chuo Kikuu cha Ohio, Marekani.
Maumivu kwenye matiti
Hii ni dalili ya kawaida ya ujauzito ambapo nguvu za homoni mwilini huongezeka wakati yai linavyopata “rutuba”, jambo ambalo huongeza wingi wa damu na kuyafanya matiti ya mwanamke kuvimba na kuwa makubwa isivyo kawaida.
Maumivu mwilini
Utaanza kusikia maumivu kama vile unataka kuingia katika siku zako. Kwa kawaida hali hii hutokea wakati yai likiwa linasafiri kwenda katika chumba cha mimba. Hivyo, hali hiyo husababisha sehemu hiyo itanuke taratibu na kusababisha maumivu hayo.
Kutokwa damu bila kutegemea
"Wanawake wengi hufikiria kutokwa na damu kidogo ni dalili ya kuwa katika siku zao. Lakini, katika hali halisi, kutokwa damu kusikotegemewa, huwakumba asilimia 25 ya wanawake wakati wa kurutubika kwa yai,” anasema Goist. Ambaye anaendelea kusema kwamba iwapo utaona hedhi yako inakuwa fupi au inafanyika katika hali ambayo si ya kawaida, unashauriwa kwenda kufanya kipimo cha ujauzito..
Kuchoka
Unapojisikia kuchoka na kukosa raha, au kutaka hata kulala wakati ukiwa kazini, lazima ufahamu kwamba mwili wako unajirekebisha kuingia katika kipindi kipya cha mabadiliko.
“Tambua kwamba katika kipindi cha mwanzo cha ujauzito ni muda ambao mtoto tumboni huanza kutumia sehemu ya nguvu zako na hivyo kukuletea uchovu na usingizi” anasema Goist.
Chuchu kuwa nyeusi
Chuchu huanza kubadilika rangi yake kutokana na chembechembe za uhai (seli) kuanza kufanya kazi kwa nguvu zaidi. Hata hivyo, Goist anasema: “Wanawake wenye ngozi nyeusi hawawezi kuiona dalili hii mapema hadi muda wa kama wiki kumi zipite.”
Kichefuchefu
Hali hii huwapata asilimia 85 ya wanawake wanapopatwa na ujauzito, ambapo nyakati za asubuhi ndipo hasa hujionyesha.
Mwili kuvimba
Kuna wakati kupungua kwa nguvu za uyeyushaji chakula kunaweza kukusababishia kuona tumbo limevimba na nguo zikawa zinakubana kutokana na chakula kujaa katika utumbo. Lakini hali hiyo ikiendelea na ukaona siku zako haziji, basi ni vyema ukatambua kwamba tayari una ujauzito na kinachokupasa ni kwenda kuhakikisha.
Kwenda haja ndogo mara kwa mara
Kwenda haja ndogo kila mara ni dalili kwamba kibofu chako kimeanza kufanya kazi ya ziada, ambapo huwa kinafanya kazi ya kuondoa maji kwa uthabiti zaidi wakati wa ujauzito. Hali hii pia hujitokeza mwishoni mwa ujauzito, ambapo kibofu kitakapokuwa kinarudia hali yake ya kawaida baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu.
Tamaa ya vitu mbalimbali
Kutokana na mwili kuwa na “mzigo” wa ujauzito na hivyo kuchoka, hali hiyo humfanya mwanamke kutamani vitu mbalimbali ili kukidhi mabadiliko yaliyojitokeza katika mwili wake. Hii ni pamoja na kutaka vyakula fulani au kufanya mambo ambayo hapo nyuma alikuwa hayapendi.
Kuumwa kichwa
Kuongezeka kwa damu kunaweza kusababisha kichwa kuuma japokuwa si sana, hususani katika wiki za mwanzo za ujauzito. Hata hivyo, hali hii hukoma mwili unapojirekebisha na mzunguko wa homoni unaotokana na ujauzito.
Kufunga choo
Homoni ambazo husababisha mwili kuvimba pia husababisha kufunga choo kutokana na mfumo wa kuyeyusha chakula kutofanya kazi vyema. Hata hivyo hali hii inaweza kujitokeza zaidi wakati ujauzito unapoendelea kukua.
Kuwa na hasira
"Kutokana na kuongezeka kwa homoni za utendaji kazi mwilini, hali hiyo itakusababishia uchovu, na kukufanya kuwa na hasira,” anasema Goist
Kuongezeka kwa joto mwilini
Kipimo cha joto la mdomo ni muhimu katika kutambua hali ya ujauzito. Kwa kawaida joto huongezeka kwa nyuzi moja au zaidi wakati yai likiwa linatunga mimba. Hali hiyo ikiendelea kwa zaidi ya wiki mbili, itakuwa inaonyesha dhahiri kwamba kuna “mtoto anakuja”.