Tuesday, May 8, 2018

SOMA UKWELI KUHUSU SIDIRIA KWA WANAWAKE

Kwa miaka mingi wanawake wamefunzwa kuvaa sidiria ili waweze kunyanyua maziwa yao au kuyaweka katika umbile la kupendeza.
Hata hivyo, sidiria imetajwa kuwa chanzo cha maradhi ya mgongo, misuli ya kifua, maradhi ya moyo na kusababisha kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa fangasi chini ya matiti, inapovaliwa kwa muda mrefu.

Utafiti mpya uliofanywa na wataalamu wa afya kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Besancon, Ufaransa umebaini kuwa sidiria haimsaidii mwanamke zaidi ya kumsababishia maradhi kadhaa.

Profesa Jean-Denis Rouillon ambaye ametumia miaka 15 kufanya utafiti kwa wanawake 330 alibaini kuwa sidiria zina madhara kadhaa kwa wanawake akipingana na dhana iliyojengeka kuwa sidiria ni miongoni mwa mavazi muhimu kwa kundi hilo.
Profesa Rouillon hajawakataza wanawake kuvaa sidiria bali anasisitiza kutovaa kwa muda mrefu (mfano kulala nazo) na kutovaa mapema hata kama hunyonyeshi.

Sidiria haimpi manufaa yoyote mwanamke” anasisitiza Profesa Rouillon, ambaye katika utafiti wake alibaini kuwa wanawake ambao hawavai sidiria tangu usichana, wana maziwa imara yaliyozungukwa na misuli kakamavu kuliko wanaopendelea kuvaa nguo hiyo ya ndani.
Anasema kwa kiasi kikubwa binti anayeanza kuota maziwa anapovaa sidiria husababisha maziwa kuanguka mapema kuliko binti ambaye hatavaa sidiria.

Profesa huyo ambaye alianza kufanya utafiti tangu mwaka 1997 anasema alitumia rula na vifaa vingine kufanya utafiti huo na aligundua kuwa kuna tofauti ya milimita saba za urefu na msimamo wa maziwa kwa wasiovaa sidiria.

Sidiria imekuwa kama tegemeo pale tu mwanamke anapoanza kuota maziwa, ina maana kwamba misuli inayobeba maziwa haitumiki na badala yake sidiria inachukua wajibu huo na hivyo misuli hiyo husinyaa kwa kukosa kazi” anasema

Anasema si kweli kuwa mwanamke asiyevaa sidiria maziwa yake huanguka bali huwa na ngozi nzuri zaidi katika viungo hivyo, huwa huru na matiti huwa katika umbile zuri zaidi.

Katika ushauri wake wa majumuisho ya utafiti huo Profesa huyo alisema: “Ni dhana potofu kudhani kuwa sidiria ni msaada kwa wanawake, ninachowashauri wanawake ni kutotegemea zaidi sidiria.”

Utafiti mwingine kama huu ulifanyika Aprili 2012, nchini Uingereza na Dk Nicholas Ericson ambaye alibaini kuwa wanawake wanaovaa saizi kubwa ya sidiria wapo hatarini kupata saratani ya maziwa.

Gazeti la ‘Bussiness Week’ la nchini Marekani liliwahi kuandika ripoti kuwa viwanda vinavyotengeneza sidiria nchini humo vinapata mapato ya zaidi ya dola bilioni 11 (sawa na trilioni 17 na bilioni 600 Tsh)

Hata hivyo tafiti nyingine ziliwahi kufanyika na kugundua kuwa wanawake wasiovaa sidiria wakati wa mazoezi wamo hatarini kuharibu matiti yao.
Cletus Kiwale, Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake anasema hajawahi kusikia iwapo sidiria ina madhara kwa mwanamke.
Sidhani, labda sidiria inayobana sana, hata hivyo suala hilo linahitaji uchunguzi wa kina” anasema Dk Kiwale.

Naye Dk Sebalda Leshabari, Mwalimu wa Ukunga katika Chuo Kikuu cha Muhimbili anasema hakuna ukweli kuwa sidiria inasababisha madhara ila tu kwa wale watakaozivaa muda mrefu.
Mtu anapovaa kwa muda mrefu lazima atapata fangasi kwa sababu ya jasho, lakini pia, hatakuwa huru anatakiwa auache mwili upate hewa” anasema

Anasema kwa wanawake wanaonyonyesha hawana budi kuvaa sidiria ili watengeneze maumbile yao ambayo wakati huo matiti yao huwa makubwa.
Mwanamke anayenyonyesha anatakiwa avae sidiria ili azuie maziwa yasimwagike na pia ukubwa wa maziwa wakati huo humfanya asiwe huru” anasema

Dk Robert Mansel, daktari wa upasuaji katika chuo kikuu cha wales, anasema wanawake wengi wenye maumivu ya mgongo, hasa wale wanaokaribia kufunga hedhi, hupata maumivu hayo wanapovaa sidiria.
Anasema wanawake waliovaa sidiria kwa miaka mingi, wanapoacha kuvaa hupata unafuu na wepesi katika miili yao.

Profesa Mansel anasema wanawake wengi wanaopata maumivu ya mgongo na maziwa husababishwa na uvaaji wa sidiria.
Hakuna utafiti uliowahi kufanyika na kubaini iwapo sidiria ina manufaa yeyote kiafya kwa mwanamke, lakini imekwishabainika kuwa zinaleta maumivu” anasema Dk Mansel

Dk Mansel anasema utafiti zaidi ufanyike ili kupata ukweli zaidi kuhusu madhara ya sidiria kwa wanawake.
Anitha Senkoro, mkazi wa Kigogo Dar es Salaam anasema wanawake wengi wanavaa sidiria ili kuyaweka maziwa katika umbile zuri.
Baadhi maziwa yao hayajalala (kulegea) lakini wanavaa sidiria kwa fasheni tu na mkumbo” anasema.

Angelina Mitande,(75) Mkunga mstaafu aliyefanya kazi katika Hospitali ya Muhimbili miaka ya 70, anasema zamani wanawake walivaa sidiria baada ya kujifungua ili kuhifadhi maziwa yasivuje lakini si kwa fasheni.

Unavaa sidiria ukiwa unatoka kwenda katika sherehe tu. Hatukuvaa kila wakati kama mnavyofanya siku hizi. Hata watoto wetu tuliwakataza kuva sidiria mapema” anasema

Angelina anasema kuvaa sidiria muda mrefu kunasababisha maradhi ya ngozi hasa mwanamke asipozingatia usafi.
Naishooki Kosey, Mmasai, mkazi wa Morogoro, anasema watu wa kabila hilo katu hawavai sidiria lakini maziwa yao ni madogo na mazuri.

Hata tukinyonyesha hatuvai sidiria, si jadi yetu hata kidogo. Wala mavazi yetu hayatufanyi kukosa uhuru tusipovaa sidiria” anasema Naishooki.
Anasema binti akifundishwa kuvaa sidiria mapema, atajikuta anakuwa mtumwa wa vazi hilo hata asipovaa hawezi kutoka.

Wakati mwingine maziwa yake yana umbile zuri tu, lakini anafuata mkumbo na kuona ni nguo ya lazima kuvaa” anasema