Tuesday, May 8, 2018

JINSI YAKUMNASA MPENZI ANAYEKUFICHA TABIA ZAKE MBAYA



Tatizo ambalo limekuwa likiwakuta wapenzi wengi wanaoanzisha uhusiano wa kimapenzi wenye mwelekeo wa maisha ya ndoa ni kuingizwa ‘mkenge’ kwa kufichwa baadhi ya tabia mbaya na wapenzi wao.

Wapenzi wanaoficha tabia wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuteka mapezni ya watu, lakini baadaye wakishafanisha azma yao hujiachia na kuanza kuwatesa wenzao.

“Sikujua kabisa kama ana tabia hizi, ningetambua mapema kama ni mhuni nisingekubali kuoana naye.”

Uchunguzi unaonyesha kuwa wanandoa wengi mpaka sasa wanajuta kufunga ndoa na wapenzi wao na kwamba kama wangetambua tabia za wenza wao mapema wasingekubali kufunga ndoa.

Inawezekana hata wewe unayesoma makala haya unajuta kiasi cha kulalamikia mwenzako alivyobadilika tabia tofauti na mwanzo ulivyoanza kupendana naye. Hebu fuatilia dondoo hizi ili ujue namna ya kumtabua mpenzi anayekufichia makucha, ili usijiingize kwenye uhusiano usiokuwa sahihi.

MPE UHURU WA KUTOSHA

Watu wengi wanapoanzisha uhusiano huwabana sana wapenzi wao kwa kuwapekulia simu, kuwachunga watokapo na waingiapo, jambo ambalo huwafanya wahusika kujilinda sana wakiamini wanafuatiliwa.

Ndugu yangu usimbane mpenzi wako, mwache huru, atembee atakavyo na awasiliane na amtakaye, wewe kaa nyuma yake ukimchunguza bila mwenyewe kujua. “Mke/mume wangu hajali mambo haya” Hujali kumbe unamteka mwisho wa yote utamnasa.

MPE MAJUKUMU

Ukisha mchagua umpendaye, huwezi kutambua uwezo wake mpaka umpe majukumu ya kufanya. Kwa mfano mtume akalipie maji, umeme au mwagize asimamie jambo fulani.

Ukishafanya hivyo kaa kando mwangalie, anavyoiba chenji, anavyopunguza gharama bila kukushirikisha, lakini baadaye muulize, utashangaa alivyotibua mambo akidhani wewe si mtu wa kujali sana, kumbe ulikuwa umemtega na hatimaye umemnasa.

MUWEKE KWENYE WAKATI MGUMU

Njia nyingine ya kumnasa anayekufichia makucha ni kumweka katika wakati mgumu. Wanasema rafiki wa kweli hujulikana kwa dhiki. Tengeneza dhiki kwa makusudi na kuzitekeleza. Akikuambia naomba unitumie vocha mpenzi au ninunulie nguo mwambie sina pesa, halafu uone kama atakuwa na kiwango kile kile cha mapenzi. Wapo wanaume wengine wa pesa na mishahara ya wapenzi wao, ili kuwabaini ni kuwanyima wakati mwingine.

TUMIA WATU

Katika hali ya kawaida, majirani na marafiki wanawatambua zaidi wapenzi wetu kuliko jinsi tunavyowatambua sisi. Inawezekana kabisa mpenzi wako akawa mtakatifu unapokuwepo lakini ukiondoka anajiachia ile mbaya, hivyo ili kujua tabia zake waulize rafiki na jirani zako watakusaidia kumtabua mpenzi wako.

ANGALIA ANAVYOWATENDEA WENGINE

Wapenzi wengi wanapokuwa wamepata wapenzi hutazama wanavyotendewa wao na kudhani inatosha. Mtu muungwana huwatendea wengine mema. “Aa, mama naye kanichosha kila siku anataka pesa.”

Hebu sikia kauli hii, kama mtu analalamika kuchoshwa na mama yake itakuwaje kwako? Amka na kutambua kuwa anakufichia makucha na ipo siku atakubadilikia hata wewe na kukutesa. Amka usikubali kudanganywa na mpenzi mnafiki.