Saturday, November 11, 2017
ULIMUACHA, AMEBADILIKA NINI UNAMFUATA!
Karibu kwenye Jumatatu nyingine mpenzi msomaji wa XXLove. Leo nitazungumza na wale wenye tabia ya kuacha wapenzi wao na baadaye kugundua walikosea na kuamua kuwarudia kwa nguvu na vitisho vingi.
Ninaowazungumzia hapa ni wale wapenzi wenye tabia ya kuacha kwa kujifanya wao ni zaidi lakini mwisho wa siku wanagundua kuwa kumbe wao ndiyo hawawezi kabisa kuishi bila wapenzi waliowaacha.
Kumekuwa na kasumba kwa baadhi ya wapenzi kuwaacha wapenzi wao kwa sababu mbalimbali. Tena sababu nyingine zikiwa ni za kipuuzi na huwaacha kwa mbwembwe na kashfa za kila aina ilimradi tu kumfanya anayeachwa ajione si kitu, si lolote kwa mpenzi wake huyo.
Baada ya kila mtu kushika hamsini zake ndipo aliyeacha anagundua kuwa kumbe hana ubavu wa kuishi bila yule aliyemuacha kwa mbwembe nyingi. Kinachofuatia hapo ni yule aliyeacha kuamua kumrudia mpenzi wake kwa nguvu na vitisho vya kila aina bila kujali kama ana mpenzi mwingine au la!
Unapoamua kumuacha mpenzi wako, lazima ujue kuna mambo yafuatayo; yawezekana mpenzi wako uliyemuacha akaendelea kuishi mwenyewe bila mpenzi hadi atakapoikubali hali halisi na kupata mpenzi mwingine au kitendo cha wewe kumuacha na yeye kutafuta mpenzi mpya kwa maana ya kupunguza machungu ‘stress.’ Hakuna kitu kibaya kama kumsababishia mwenzi wako stress katika maisha tuliyonayo kwa sasa.
Baada ya kujitathmini na kugundua aliyemuacha ndiye mpenzi sahihi na anayestahili katika maisha yake, ndiye mke bora au mume bora mwenye kujenga familia bora, wengi hutamani kurudi lakini wakati mwingine anakuwa amekwishachelewa kwani tayari nafasi anakuwa ameshapewa mwingine.
Aliyeacha hushindwa kuukubali ukweli kuwa yeye ndiye tatizo na chanzo cha yote, anachofanya sasa ni kulazimisha mpenzi wake warudiane na inapoonekana ana msimamo, basi aliyeacha huchukua hatua ya kutoa vitisho ikiwemo kusambaza baadhi ya picha zao ambazo walipiga au ulipigwa ukiwa faragha au hata picha za pozi tatanishi.
Usikurupuke tu kujifanya unaweza kumuacha uliyenaye na kumpata mpenzi bora kwa haraka, uwe unafikiri kabla ya kutenda. Jaribu kujiuliza ulimtosa kwa nini? Na sasa amebadilika nini unamfuata!
Kama ulimtosa au kumkataa kwa kujua ataadhirika mjini, imekuaje leo unamlazimisha mrudiane kwa nguvu na vitisho? Au kwa sababu uliyemtegemea hakufai?
Ungana nami wiki ijayo kwa mada nyingine murua.