Saturday, November 11, 2017

HIVI MKE WA SAMPULI HII WA KAZI GANI?

Mpenzi msomaji wangu, wiki hii nimeona nimzungumzie mwanamke ambaye hana sifa za kuendelea kuitwa mke, dawa yake ni kuachwa awe ‘nunga yembe’.

Haridhiki na penzi lako
Wapo wanawake ambao wewe unaweza kujitahidi kumpatia mapenzi kadiri unavyoweza lakini yeye hatosheki. Anakuchukulia wewe ni dhaifu sana na wakati mwingine kuhisi yupo mwingine anayeweza kumpa zaidi ya kile unachompa, huyu ni tatizo.
Ana wivu wa kijinga
Hatukatai, wivu ni muhimu sana kwenye suala la mapenzi lakini kuna ule wivu uliopindukia kiasi cha kuwa kero. Walio kwenye ndoa wananielewa namaanisha nini. 
Kwa kifupi mtu mwenye mapenzi ya dhati na mwenziye lazima awe na wivu lakini ukiwa na ule wa kupindukia ni tatizo linaloweza kuitibua ndoa.
Anaona unamsaliti kila mara
Huku kunatokana na kutokujiamini tu. Ukioa mwanamke ambaye kila wakati unapokuwa mbali naye anahisi unamsaliti, huyo hakuamini na kamwe hamuwezi kudumu. Mara kadhaa mtakuwa mkigombana akihisi una mwingine kumbe hakuna ukweli katika hilo.
Anahisi wewe si mtu sahihi 
Wapo wanawake wanapoingia kwenye ndoa baada ya muda wanahisi wamekosea kuolewa na wanaume husika.
Unakuta mke wa mtu anahisi fulani ambaye zamani alikuwa kwenye uhusiano naye angekuwa sahihi zaidi baada ya kuona upungufu fulani kwa huyo aliyemuoa.
Yuko kimasilahi zaidi
Kuna wanawake ambao ukiwaoa wanakuwa na furaha na wewe ukiwa unazo tu, ukiishiwa wanaanza kununa na kuleta visirani vya hapa na pale. Hawa ni tatizo, mwanamke wa kweli ni yule anayeridhika kuwa na wewe kwenye shida na raha.
uko tayari muachane 
Hivi hujawahi kumsikia mke wa mtu akimwambia mumewe; ‘Kama vipi tuachane, kwanza kwetu sijafukuzwa na nilikuwa nakula, nalala, navaa.” Mwanamke anayeweza kumtamkia mume wake maneno haya, huyo si mke.
Hapendi ndugu zako
Waswahili wanasema ukipenda boga, penda na ua lake. Kama utatokea kuoa mwanamke ambaye anakupenda wewe tu lakini akija ndugu, rafiki au mtu mwingine wa karibu yako anabadilika, huyo ana matatizo kwani atakufanya utengwe na jamii yako.
Mbinafsi
Ogopa sana mwanamke anayependa kutumia kipato chake kufanya mambo binafsi tena kwa siri. Kwa mfano kusaidia kwao, kujenga nyumba kwao, kuanzisha miradi yake bila kukushirikisha.
Anataka awe na sauti
Mwanaume siku zote atabaki kuwa kiongozi wa familia lakini wapo baadhi ya wanawake hawataki kukubaliana katika hilo. Wengi wanalazimisha usawa na wengine wakitaka wao ndiyo wawe na sauti kuliko waume zao.