Monday, November 20, 2017

Fahamu Katuni Zinavyoweza Kutafuna Ubongo wa Mtoto Wako na Kumpa ‘Kifafa’


Utamaduni wa kuangalia katuni au vikaragosi kama inavyofahamika kwa nchi jirani, ni utamaduni pendwa, maarufu na uliokubalika kwa wazazi wa watoto wengi kama njia ya kuwasaidia kujifunza na kuburudika. Lakini burudani hii ina hatari kubwa pia.
Kwenye familia nyingi hasa za wenye uwezo wa kuanzia kima cha kati na hata wale wa kima cha chini waliofanikiwa kununua runinga, watoto huanza kuangalia katuni tangu wakiwa na umri wa miezi sita. Wanapofikisha umri wa miaka mitatu kitaalam watoto hao hubadilika na kuwa watazamaji watiifu wa katuni.

Katika umri huo wa miaka mitatu na kuendelea, ni wakati ambapo watoto wanakuwa na uwezo mkubwa wa kuelewa mambo wanayoyatazama. Wanatengeneza ufahamu fulani kuhusu dunia kutokana na kile walichokiangalia kwenye katuni au vipindi vingine wanavyopata nafasi ya kuangalia japo kimakosa.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya, katika umri huo, kwenye familia ambazo baba humsikiliza sana mtoto na kutaka afanye kile anachopenda, mtoto hugeuka kuwa na uraibu (addiction) au mfuasi mwaminifu wa katuni. Hivyo, endapo katuni zitakuwa na madhara chanya kwake ikiwa ni pamoja na kujifunza mambo mazuri itamsaidia kwa kiasi chake lakini kama sivyo itamtafuna ubongo na kumsababishia magonjwa, kutokana na madhara ninayoanza kuyataja katika aya inayofuata.
Wataalam wanaeleza kuwa mtoto anayeangalia sana katuni ambazo zinaonesha matukio ya migogoro na mapigano, ana hatari ya kupata matatizo ya kiakili na hisia (mfano kuwa na hasira kupita kiasi), pamoja na ubongo na macho kiasi cha kuongeza hatari zaidi ya matatizo ya kiafya.
Tafiti za taaluma ya saikolojia zimeeleza kuwa katuni za mapigano na migogoro pia zinawafanya watoto kuwa wakorofi na wanaoweza kuchukua hatua kali za vitendo dhidi ya wenzao.
Matatizo mengine pia hushambulia ubongo na macho ya watoto wanaoangalia katuni za aina hiyo. Mwendo kasi wa taswira wanazoangalia kwenye runinga husababisha madhara kwenye macho na ubongo wa mtoto.
Kwa mujibu wa mwandishi na mwanasaikolojia Raymond Villanueva, endapo tabia ya kuangalia katuni za migogoro na mapigano itakithiri, mtoto anaweza kushambuliwa na ugonjwa wa kifafa unaotokana na matatizo yanayogusa utendaji kazi wa ubongo.
Ingawa katuni pia ina faida nyingi hata kwa wazazi ikiwa ni pamoja kuwasaidia kuwafanya watoto wawe na kitu cha kufanya ili wasiwasumbue wanapokuwa bize na majukumu mengine, inawapasa kuchukua tahadhari na kufuatilia kwa makini kitu ambacho watoto hao wanaangalia na muda wanaotumia kuangalia ili kuwanusuru na matatizo haya ya ubongo.