Niwiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii ambayo ni namba moja kwa kuandika makala nzuri za kimapenzi. Naamini umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida.
Mpenzi msomaji wangu, wiki hii nitazungumzia suala la kufanya mapenzi ambalo hakika linachukua nafasi kubwa kwenye maisha yetu ya kila siku.
Hakuna anayeweza kusema hili halimhusu, achilia mbali wagonjwa, watoto na wale wasiokuwa na akili timamu. Ukizungumzia ishu ya kufanya mapenzi unagusa eneo nyeti linalowafanya baadhi ya watu wayafurahie maisha na wengine kuyachukia.
Nasema hivyo kwa kuwa, mapenzi ni afya hasa yanapofanywa kwa utaratibu ambao hauwezi kusababisha kero. Lakini pia mapenzi ni starehe kwa wale walioruhusiwa kufanya tendo hilo. Ni tendo takatifu ambalo haliwezi kufanywa kiholela licha ya ukweli kwamba sasa hivi mambo ni vululuvululu.
Vurugu kwenye mapenzi imekuwa kubwa, watu wanalazimisha kufanya tendo hilo hata katika mazingira ambayo si rafiki. Ndiyo maana nikauliza kwamba, hivi kufanya mapenzi ni kwa ajili ya kustareheshana, kupata faida za kiafya au kukomoana?
Nimeuliza swali hilo nikiwa na lengo la kuelezea mazingira yanayowakosesha amani baadhi ya wanandoa ambao wanajikuta wakikosa amani kutokana na wenza wao kujiona wana haki ya kupatilizwa kila wakati wanapojisikia.
Nilizungumza na mmoja wa wasomaji wa safu hii aliyejitambulisha kwa jina la Sada. Huyu dada aliolewa hivi karibuni lakini anasema anafikiria kuikimbia ndoa kwa kero anayoipata kwa mume wake linapokuja suala la tendo la ndoa.
Yaani mumewe huyo amekuwa akipenda sana kufanya mapenzi. Kila wakati anataka atimiziwe kwa maelezo kuwa, ameoa ili apate fursa ya kufurahi.Matokeo yake sasa, mapenzi yanafanywa kama dozi! Asubuhi, mchana na jioni, tena shughuli yenyewe inakuwa si ya kitoto. Dada huyo anaeleza kuwa, badala ya mapenzi kuwa starehe sasa anaona ni kero na wakati mwingine anaona kama anakomolewa.
Sasa najiuliza, haya ni mapenzi ya aina gani? Sawa ni mkeo lakini kwa nini ufanye jambo hilo kuwa la kumkosesha amani mwenza wako? Unataka upewe asubuhi, mchana na usiku, tena usiku ni kukesha eti kwa kuwa umesikia mapenzi ni afya, hivi afya itapatikana kwa hali hiyo?
Nadhani dada huyu anawakilisha wengi huko mtaani. Wapo wanaume ambao wanachukulia mapenzi kama chakula, kwamba eti wasipopata watakufa. Hiyo ni dhana potofu! Mapenzi ni kufurahishana tena yanafanyika pale ambapo kila mmoja anajihisi kuwa na mwenza wake.
Itakuwa si jambo la busara kama mtakuwa mkilazimishana, mkifanya hivyo ni lazima mmoja wenu ataona karaha na hata ile furaha iliyotarajiwa haiwezi kupatikana.Lakini hili la kulazimishana kufanya mapenzi halipo kwa wanaume tu, wapo wanawake ambao nao ni kama vile wana pepo wa ngono.
Kila wakati wanataka! Mume amerudi nyumbani akiwa kachoka kutokana na majukumu ya kila siku lakini mke analazimisha kupewa haki yake.Nihitimishe kwa kusema kwamba, mapenzi si karaha, mapenzi ni furaha hasa yanapofanywa na wawili walio na utayari. Kumlazimisha mwenza wako hata kama hajisikii,unakosea.