Saturday, November 18, 2017

Ondoka Katika Mahusiano Ambayo Hayana Uelekeo

“Miaka kumi iliyopita nilikuwa katika kipindi ambacho wasichana wengi wapo kwa sasa…” Anaongea Dada Anna. Nilikuwa katika mahusiano ambayo hayakuwa na uelekeo, niliumia sana mpaka pale nilipogundua kuwa sikupaswa kuishi kwaajili ya mtu. Kama ipo ipo tu, niliamua kufanya maisha yangu mwenyewe kujiimarisha mimi kwanza kama mwanamke ndipo niwaze wengine.
Nilikuwa na mwanaume ambaye baada ya mahusiano ya miaka mitatu, wote tukiwa tunafanya kazi alikuwa bado hajamaliza ujana na alitaka tuendelee kutoka kila mwisho wa wiki kunywa na kufurahi na rafiki zake, nilikuwa na mwanaume ambaye ukimuuliza mipango yake ya maisha ya baadaye anakuambia “Mbona unaharakisha mambo…” akidhani labda namuulizia unanioa lini?

Nilikuwa na mwanaume ambaye ukimuambia kiwanja kinauzwa sehemu flani anakuambia sina pesa lakini mwisho wawiki anakuambia twende Zanzibar tukapumzike. Ingawa najua kwa baadhi ya mabinti wengi anaweza kuwa mwanaume wa ndoto zao, lakini mimi wakati huo sikuwa binti tena, miaka 27 tayari nilishakuwa mwanamke na nilipaswa kuwaza kuhusu maisha ya mbeleni kuliko burudani.
Niliamua kuachana naye kwakuwa nilikuwa sioni uelekeo, tayari alishaanza kunipoteza, ingawa sikubadilisha mawazo kwa maana bado niliendelea kubaki na malengo yangu ya kimaisha, lakini mambo yake yalinirudisha nyuma. Nilijikuta naingia katika matumizi ya kipuuzi kwajaili ya kulinda penzi, mpo club kaishiwa kama mwanamke inabidi nitoe hela yangu kuokoa jahazi. Baada ya kuona napotea basi niliamua kujitoa na kuanza maisha yangu bila yeye.
Leo hii nina kampuni yangu, ndoa yangu na familia niliyokuwa nikiitamani, sikusubiri mwanaume kutimiza ndoto zangu nilianza kuziendelea ndoto zangu mimi mwenyewe. Hata wewe unaweza kama utatambua thamani yako, kama utafahamu kuwa hakuna mwanaume yeyote ambaye anaweza kukuinua kama wewe mwenyewe hutaaamua kuinuka.
Kama huoni dalili za mtu uliyenaye kubadilika, kukua, kuwa mtu mzima ni vyema ukajitoa na kufanya mambo yako ya kiutu uzima. Mtu sahihi atakuja na atakupa furaha ya kweli. Acha kujilazimishia kuwa labda unapenda sana, kama umefika wakati unaona kabisa mtu uliyenaye sio kwamba tu hataki kubadilika lakini pia anakubadilisha taratibu na unaelekea kuwa kama yeye, basi ni wakati sahihi wa kuachana naye....