Saturday, November 18, 2017

Jinsi Nilivyomgeuza Mwanangu Zezeta Kwa Kuendekeza Ushirikina

Ndoa ni kitu ambacho naamini kila mwanamke anakitamani, kuna umri katika maisha ya mwanamke ukifika akili yake haiwazi kitu kingine zaidi ya kuolewa hasa kama anakuwa amepitia mahusiano mengi ya kutendwa na kuumizwa. Kwangu umri huo ulifika miaka kumi iliyopita, nikiwa na umri wa miaka 32 nilikuwa nimeshaachwa na wanaume watano.
Nikisema kuachwa simaanishi wale wa kuingia katika mahusiano na kuachana bali nazungumzia wale wakuwa kwenye mahusiano siriasi mpaka kufikia hatua ya kutambulishana. Mpaka wakati huo nilikuwa sifahamu tatizo lilikuwa nini kwani kusema kweli Mungu kanijaaalia uzuri na mambo kule kwa sita kwa sita nayajua, hivyo kuachwa na mwanaume kwangu kilikuwa kitu kilichoniumiza sana.

Ndoto za kuolewa zilishapotea, nilishakata tamaa, sikutaka tena mwanaume wakuja kutambulisha nyumbani halafu aniache kwenye mataa na kuingia kwenye aibu nyingine. Nikiwa mfanyakazi wa Benki moja kubwa tu hapa nchini, mwenye mshahara mkubwa nikiwa na nyumba yangu na gari nilikata shauri la kutokuolewa tena na kuamua kutafuta mtoto.
Nilibadili kabisa wazo la kuolewa na kuamua kuanza kutafuta mwanaume wa kuzaa naye tu. Hilo ndiyo lilikuwa lengo langu na ili asinisumbue kwa maana ya kumtaka mtoto nilihitaji mume wa mtu au kijana ambaye hana kazi ambaye hata nikimuambia mimba si yake basi hatahangaika kunifuatilia au nikimuambia tu nina mimba basi atanikana ili kukwepa majukumu.
Nakumbuka ilikuwa ni siku ya jumatano, nikiwa kazini nimechoka, kama afisa mikopo aliingia kijana mmoja wa makamo, akiulizia taratibu za kuchukua mkopo. Kwakumuangalia tu nilimtamani lakini kwa mawazo yangu kuw anina gundu hata sikutaka kuelekeza akili zangu kwake kwani kwa muonekano tu alikuwa ni kijana anayejiweza, nilijua lazima atakuwa naamke au hata kama atakuwa akimiliki binti mbichi kabisa hivyo hata asingevutiwa na mimi.
Alikuja tukaongea nikampa maelekezo yote ya namna ya kuchukua mkopo, sijui nini kilitokea lakini baada ya sisi kama Benki kutembelea biashara yake na nyumba yake aliyokuwa akiiweka rehani mahusiano ya kimepenzi yalinzia hapo. Ndani ya muda mfupi nilijua kijana yule alikuwa akiitwa Joseph au Jose, pamoja na umri wake wa miaka 35 alikuwa bado hajaoa wala hakuwa na mchumba.
Mwanzo nilihisi ana matatizo nikimaanisha labda sio riziki kwani kwa umri ule, uwezo wake wa kifedha na muonekano wake alitakiwa kuwa ameoa, lakini nilikuja kugundua kuwa alikuwa mzima kabisa tena mwenye shughuli hasa, tatizo lake kubwa nikuwa alikuwa bize na kutafuta pesa kiasi cha kusahau kuoa. Tulianza mahusiano harakaharaka na ndani ya miezi mitatu alitaka kuja kujitambulisha kwetu.
******
Kwangu suala la kujitambulisha ilikuwa mtihani mkubwa kwani niliwaza atakuwa sawa na wale wengine watano, hivyo nilimkatalia katalia nikiogopa kumpoteza. Nilijifanya kama nataka tuchunguzane kwanza mpaka aliponiambia, “Doris kwa umri nilionao sidhani kama kuna kipya nitakigundua kwako ambacho kitanifanya nisikuoe, nahitaji familia…” Aliongea kwa kumaanisha kiasi cha mimi kumuamini lakini tatizo bado likawa kwangu, sikumuamini.
Kabla ya kumpeleka nyumbani niliongea kwanza na Mama na baada ya kumueleza wasiwasi wangu niligundua kuwa hata yeye alikuwa nao huo huo hivyo kabla ya yote aliniambia niombe ruhusa kazini ili twende kijijjini kwetu Iringa “Tukamtengeneze Jose kabla ya kumruhusu kuja nyumbani..”. sikubisha wala kufikiria mara mbili, tulirudi Makete ambapo baada ya kukutana na wataalamu walinipa dawa ya kumuwekea Jose kwenye chakula na kweli ilisaidia (nilivyoamini mimi).
Ndani ya miezi mitatu nilifunga ndoa ya kanisani, tena kubwa ya kifahari, baada ya kuhangaika sana kwa muda mrefu, kupitia mateso mengi ya mahusiano hatimaye nilikuwa mke wa mtu. Baada ya mwaka mmoja Mungu alitujalia kupata mtoto wakike na ndoa yetu ikazidi kupata furaha, lakini bado nilikuwa sijiamini hivyo mara kwa mara nilikuwa nikienda kijijini kuchukua dawa kwa ajili ya ‘kumtengeneza’ mume wangu na kuongeza nguvu ya penzi.
Wakati mwanangu akiwa na umri wa miaka minne na mimi nikiwa na ujauzito wa mwanangu wapili miezi ya mwanzo kabisa, kulitokea uizi flani pale ofisini, ingawa mimi sikuhusika lakini ulipita uhamisho wa nguvu ambapo nilipata uhamisho wa kwenda Kigoma, kwangu hiyo ilikuwa ni kama adhabu na nilipomuambia mume wangu hakuwa tayari kulisikia hilo, hata mimi sikutaka kwenda mbali na mume na kwakuwa pesa tulikuwa nayo niliamua kuandika barua ya kuacha kazi ndani ya masaa 24.
Tulikubaliana na mume wangu nijifungue kwanza na kumlea mwenetu kabla ya kutafuta kazi nyingine au kufungua biashara. Katika kipindi hicho ndiyo kila kitu kilibadilika, ile hali ya kukaa nyumbani tu ilinifanya kuwa mpweke sana mpaka kuanza kujihisi kama sipendwi tena. Ingawa mume wangu alijitahidi kwa hali na mali kunionyesha upendo wa hali ya juu lakini nilikuwa niki mmiss sana, nilianza kuwa msumbufu kumpigia simu kila wakati, kutaka kuonge naye na kutaka kujua yuko wapi.
Wakati nikiwa kazini nyakati zote za mchana nilikuwa bize na kama mnavyojua benki tulikuwa tunachelewa sana kutoka hivyo mara nyingi nilifika nyumbani na kumkuta amesharudi au nikifika tu hachelewi. Baada ya kuacha kazi na kuwa Mama wa nyumbani ingawa mida yake ya kurudi ilikuwa ileile lakini kwakuwa mchana kutwa nilikuwa namsubiri niliona kama anachelewa.
Nilianza kuwa na gubu maugomvwi ya hapa na pale na wivu wa kijinga, mume wangu alinielewa kwakuwa alikuwa akijua ni sababu ya mimba na mara kadhaa hata kama alikuwa hajakosea alikuwa akiniomba msamaha. Pamoja nakuwa alikuwa akijitahidi kunionyesha upendo lakini sikuridhika, bado nilihisi kama ananisaliti kila nikimuona na mwanamke tu bila kujiuliza ni nani nilipaniki. Sikuweza kuvumilia niliamua kwenda kijijini kumuongezea dozi ili awahi kurudi nyumbani na kunifikiria mimi tu.
******
Nilifanikiwa kupata dawa ambayo nilipewa kwaajili ya kumuwekea mume wangu kwenye chakula nikiambiwa nihakikishe kuwa ni yeye peke yake anakula hicho chakula. Hilo kwangu halikuwa tatizo, usiku mmoja nilimuandaliwa mume wangu chakula kizuri kisha nikampelekea chumbani kimahaba, mara kadhaa huwa napenda kumfanyia hivyo, kumpikia chakula anachokipenda na sisi kula wawili tu chumbani, hasa nyakati za usiku ambapo wengine wanakuwa wamelala.
Ili nisile naye nilijifanya naingia bafuni kuoga, alitaka kunisubiri lakini nilimuambia sijisikii kula yaani baada tu ya kupika nilianza kujisikia vibaya. “Mwanao sijui anaona wivu hataki nifaidi vitu vizuri…” Nilimtania wakati nikiingia bafuni nikisingizia mimba ndiyo haitaki kula naye. Niliingia bafuni na bila wasiwasi nilianza kuoga, nilitumia muda mrefu bafuni ili amalize kile chakula, lakini kabla ya kumaliza kuoga nilisikia kelele za mume wangu.
“Ritha! Ritha! Mwanangu! Mwanangu ….” Ritha ni jina la mwanangu wa kwanza, wakati namtengea mume wangu chakula nilikuwa nimeshampandisha kitandani kulala hivyo niliposikia jina lake linaitwa chumbani bila hata kufikiria kuvaa nguo nilitoka kama nilivyozaliwa. Sahani ya chakula ilikuwa juu ya kitanda, huku mume wangu akijaribu kumtingisha mwanangu aliyekuwa amelegea pale kitandani.
Bila kujijua namimi niliungana nayeye pale kitandani nikipiga kelele za kumlilia mwanangu, alikuwa hanyanyuki na alishaanza kutoa maudenda mdomoni. Mume wangu alimnyanyua na kumpeleka kwenye gari, nilitoka vilevile uchi wa mnyama kutaka kuongozana naye mpaka niliporudishwa na wifi yangu ambaye tulikuwa tukiishi naye, alinivalisha nguo kisha wote tukaingia kwenye gari na kuelekea hospitalini.
Mwanangu alifanyiwa vipimo vyote lakini hakugundulika na kitu chochote, walipima na chakula alichokula kuona kama kilikuwa na sumu lakini wapi, hakuwa na tatizo lolote. Alikaa hospitalini kwa wiki nzima lakini hakupata nafuu, alikuwa haongei tena na kila wakati alikuwa akitoa udenda tu. Mimi nilijua kilichokuwa kimetokea, nilitamani kumuambia mume wangu lakini niliogopa kuachika, nilitamani kumpigia simu mganga lakini hakuwa na simu.
Wakati nikiwa bafuni Ritha aliamka na mume wangu bila kujua akaanza kumlisha chakula ndipo aliposhikwa na hali ile. Ilibidi Mama kuenda kijijini kimya kimya kuongea na mganga kuhusu ile ishu lakini haikusaidia chochote, alipewa dawa ya kumpa ambayo hata baada ya kumpa haikusaidia na iliposhindikana sana mganga alisema tumpeleke mtoto. Sikujua ni kwa namna gani ningeweza kumshawishi mume wangu kumpeleka mtoto kijijini.
Lakini kama walivyosema wahenga utu uzima dawa baada ya kumuambia Mama alienda kuongea na Mume wangu akimuambia kuwa inawezekana yele ni mambo ya kimila hivyo kuruhusu twende kijijini, kwakuwa hakuwa na namna na yeye alishachanganyikiwa tuliondoka kuongozana naye mpaka kijijini mume wangu akiamini kuwa labda mambo ya kimila ya upande wetu ndiyo yalisababisha yote yale.
Tulimpeleka kwa mganga ambaye alihangaika naye kwa wiki mbili nzima bila mafanikio yoyote. Ilishindikana hivyo tukalazimika kurejea Dar mtoto akiwa katika hali ileile. Baada ya hospitalini kushindikana, kwa mganga nako kushindikana, tulihamia kwenye maombi. Ingawa niliogopa kuumbuka lakini nilikuwa tayari kuonekana mchawi ilimradi tu mwanangu apone, tulizunguka makanisa yote na kuita mpaka mashehe kuja kumsomea lakini wapi, hali ya Ritha haikubadilika hata chembe.
******
Maiasha yaliendelea, nilifanikiwa kujifungua mtoto wakiume mzima akiwa na hali nzuri kabisa. Mume wangu aliendelea kunipenda na kuendelea kuhangaika kuhusu Ritha ambaye tulimtafutia mtaalamu wa viungo ili kumfanyia mazoezi, nilijua haitasaidia lakini sikua na namna. Mama yangu hakuridhika hivyo aliendelea kuhangaika akitafuta waganga mbalimbali wa kumponya mjukuu wake lakini nayo pia haikusaidia.
Sikumoja nakumbuka Mama alikuja nyumbani, nilikuwa peke yangu na watoto tu, tukawa tunaongea kuhusu hali ya Ritha na namna ya kumsaidia. Alikuwa amepata mganga mwingine Sumbawanga na tulikuwa tunajadili namna ya kumshawishi mume wnagu kumpeleka huko. Wakati tukiwa tunaongea maneno yetu sebuleni, sikujua kuwa wifi yangu tuliyekuwa tunaishi naye alikuwa ndani, nilijua tayari alishaondoka kwenda chuo kumbe alikuwa hajisikii vizuri na alikuwa amelala ndani.
Nilistuka baada ya kusikia mtu analia huko chumbani baada ya kusikia tuliyokuwa tukizungumza kwnai tuliongea yote. Nilikimbia kuangalia lakini aliwahi kufunga mlango na kila nilipogonga hakufungua, nilimsikia akionge ana simu akisema “Kaka njoo nyumbani…kuna matatizo yametokea…” Kweli hata nusu saa haikuisha mume wangu aliingia, hapo ndipo wifi alipotoka chumbani na kumwaga mchele wote.
Kilikuwa ni kilio kitupu, nilipiga magoti kuomba msamaha lakini Jose hata hakunisikiliza, kila alipomuangalia mwenetu alikuwa akitokwa machozi kama mtoto mdogo. “Ulikosa nini? Ulikosa nini…mpaka kufanya yote haya…? Aliniuliza Jose huku bado akiendelea kububujikwa na machozi, sikuwa na jibu zaidi ya kuendelea kulia kwani kusema kweli sikukosa chochote kwake.
Kutokujiamini na wivu wa kijinga ndiyo kulisababisha yote hayo. Hakutaka hata kuniangalia, aliingia ndani na bila kuchukua chochote alimchukua Ritha na kuondoka naye yeye na mdogo wake. Sikujua wameenda wapi mpaka wiki moja baadaye aliporudi na wazee na kufanya kikao, waliitwa viongozi wa dini ili kusuluhisha lakini alisema yeye hayuko tayari tena kuendelea kuishi na mimi.
Alimchukua Ritha na kuondoka naye, wakati huo Ben mtoto wangu mdogo wa mwisho alikuwa bado mdogo hivyo alimuacha lakini alipotimiza mwaka mmoja alikuja kumchukua. Nilitamani kupigania ili angalau nipate haki ya kuwalea wanangu lakini nilikosa nguvu, kwa niliyokuwa nimefanya sijui ningeanzia wapi, pia Jose alinitisha.
Aliniambia “Nakuachia kila kitu ila siku nikisikia hata unawakaribia wanangu nakuchinja, sikuui nakuchinja wewe na Mama yako…kaa mbali na familia yangu…!” Aliniambia hivyo wakati akimchukua Ben. Ingawa niliachiwa kila kitu kwa maana ya nyumba na gari lakini maisha yangu sasa hayana uelekeo,, bado nazidi kumuomba Mungu anisamehe na kumponya mwanangu.
Ingawa sasa hivi Jose amelegeza msimamo na anaruhusu niwaone watoto lakini bado hajanisamehe. Pamoja na kumpeleka kwenye maombi karibu kila siku lakini bado Ritha yuko kwenye hali ileile hajapata nafuu na amekuwa mlemavu wa kudumu. Kwangu mapenzi siyatamani tena, kazi sina tena, nilifungua kabishara lakini hata hakachanganyii kwani kila jirani ananiona mchawi, hakuna anayetaka kununua kwangu.
Nimeamua kupangisha nyumba na kuhamia mtaa mwinngine, nilitamani kuhama kabisa Dar na kuanza maisha sehemu nyingine lakini itanifanya kuwa mbali na wanangu kwani sasa angalau naruhusiwa kuwaona. Maisha yangu nikama yamesimama, sijui nini chakufanya, sina hisia za mwanaume, kila mtu amenitenga hata ndugu zangu wa damu nao hunisalimia kwa mashaka, yaani ni ile salamu tu basi hakuna hata anayetaka kuwa karibu na mimi.
****MWISHO*****
Mapenzi ya dawa kweli yapo lakini mwisho wake si mzuri, anaweza kukupenda na kukupa kila kitu lakini siku dawa ikiisha au ukapata mwenye ujuzi zaidi basi ndiyo mwisho wako. Kutumia waganga ni kutokujiamini tu, wapo watu wanaopendwa kwa dhati, wenye wapenzi wakujitoa lakini kwakuwa walianza kwa kutumia waganga bado hawaamini kuwa wanapendwa na kudhani nguvu ya dawa ndiyo iliyowavuta wapenzi wao.
Ubaya wakutumia dawa nikuwa hata upendwe vipi, hata akuonyeshe mapenzi kiasi gani bado utaendelea kujiona kama takataka, mtu asiyependwa hivyo kujikuta unaabudu waganga. Kama Mungu amekupa mpenzi bila kutumia dawa nikwanini uhangaike na dawa kumuweka kwako. Kwanini uwe mtumwa wa waganga wa kienyeji. Haijalishi una umri gani wewe jua kuwa Mungu ana mtu wako kakuandalia, huna haja ya kumshirikisha shetani.