Friday, November 17, 2017

Lipa Kisasi Kwa Kufanikiwa Zaidi Na Kufurahi Zaidi

Nimekuwa nikipata visa vingi vya watu waliopo katika mahusiano kuumizwa na kutendwa vibaya. Kuachana katika mahusiano ni jambo la kawaida tena sana, hiyo haimaanishi mwisho wa dunia au haipaswi kuwa sababu ya watu kugombana au kununiana. Lakini kama mwenza wako mliyekuwa mkipendana sana atakuacha kwa dharau na manyanyaso, atakuacha kwa kukushusha inaumiza zaidi.
Inakuwa vigumu sana kumsamehe mtu aliyekuacha kwa dharau na manyanyaso, mtu mabaye ulitumia muda wako mwingi kumpenda kumbe alikuwa anakupotezea muda makusudi tu, mtu ambaye alikuacha akiamini kua huwezi kuishi bila yeye. Wakati mwingi watu wanaoachwa namna hii hutamani kulipa visasi kwa kuwafanyia mambo mabaya waliowaacha. Kisasi kinaweza kwa kumchukua rafiki yake, kumharibia mali kumharibia kazi, kumharibia sifa au kumkasirikia tu.
Mara zote kulipa kisasi haisaidii kumuumiza mhusika bali unaendelea kuumia wewe kwakuwa huendelei na maisha yako unabaki ukiendelea kumuwaza yeye. Njia pekee ya kulipa kisasi kwa mtu ambaye alidhani kua huwezi kuishi bila yeye ni kuishi bila yeye tena kwa furaha zaidi. Fanya kazi kwa bidii zaidi ili ufanikiwe, kuwa mtu wa furaha kila siku, tabasmau kila wakati, endelea na maisha yako.
Hakuna kisasi kizuri kama mafanikio, hakuna kisasi kizuri kama furaha kwa mtu ambaye alidhani maisha yako yanamtegemea yeye. Muonyeshe kua hata bila yeye maisha yako yanaweza kuendelea tena si kuendelea tu bali kuendelea kwa mafanikio na furaha zaidi. Ondoa chuki katika moyo wako na tengeneza munkari wa kufanyakazi zaidi na zaidi. Maisha yako hayakuanza na yeye usiyaruhusu kuisha na yeye, bado unanafasi nyingi za kua na furaha.