Saturday, November 11, 2017

ETI ‘SIWEZI KUISHI BILA YEYE’, KWANI YEYE NI ‘OKSIJENI’?

Hakuna shaka tulio wengi tupo katika uhusiano wa kimapenzi wa mashaka. Hakuna hata mmoja wetu ambaye anaweza kujiaminisha kwa asilimia mia moja kwamba mpenzi wake aliye naye anampenda kwa dhati kabisa au anazuga. Hii inabaki kuwa siri ya anayependa!
Lakini sasa, kuna kitu nilichogundua miongoni mwetu, kitu ambacho tusipokuwa makini nacho tunaweza kujikuta tunajilazimisha kuishi maisha ya huzuni wakati tunayo haki ya kuishi maisha  yenye furaha. 
Ukweli ni kwamba, kila mtu anao uhuru wa kupenda kwani maisha bila mapenzi lazima yatakuwa na kasoro.
Lakini sasa, uhuru huo usikufanye ukalazimika kumpenda mtu ambaye anaonesha wazi kutokuwa na mapenzi kwako. Waswahili wanasema, mpende akupendaye, asiyekupenda achana naye. Huo ndiyo ukweli wenyewe hasa linapoingia suala la mapenzi.
Hivi utampendaje mtu ambaye hakupendi? Sawa, huwezi kujua kwamba hakupendi kwani huwezi kuufungua moyo wake lakini, kuna dalili za wazi zinazoweza kukudhihirishia kuwa, mtu huyo anakuzingua tu na kutaka kukupotezea muda wako.
Kitu kinachoniuma na ambacho ndicho kimenisukuma kuandika makala haya ni tabia ya baadhi ya watu kung’ang’ania wapenzi ambao wanaonesha kabisa kutowapenda, ukimuuliza kwa nini anamng’ang’ania wakati hapati anachokitaka, anakuambia eti anampenda sana.
Jamani ifike wakati tutambue kuwa, kutokea kumpenda mtu na yeye akakupenda kwa dhati ni bahati sana. Wengi wetu tunatokea kuwapenda watu wasiotupenda, matokeo yake ni kuumizwa kila wakati. Wewe jaribu kuchunguza utabaini walio wengi hawapati mapenzi wanayoyatarajia kutoka kwa wapenzi wao badala yake huishia kilizwa kila mara.
Niseme tu kwamba, kanuni ya mapenzi inasema, nipe nikupe, nipende nikupende, niheshimu nikuheshimu. Kama unabaini dalili za wazi kwamba mpenzi wako hakupendi usijilazimishe kuendelea kumpenda. Ukifanya hivyo utamfanya aendelee kukunyanyasa.
Kipi cha kufanya?
Huenda wewe unayesoma makala haya sasa hivi ukawa unajiamini kwamba mpenzi wako anakupenda, hiyo ni nzuri na ndivyo ambavyo kila mtu anatakiwa kuishi. Tambua ukiwa na imani kwamba mpenzi wako anakupenda itakufanya uishi maisha ya furaha na amani huku na wewe ukijitahidi kuonesha kumpenda kwa dhati, hapo mtaishi.
Lakini kama unaona penzi la mpenzi wako ni la mashaka ni wakati wako wa kuamini kwamba, unaweza kuishi hata yeye asipokuwepo.Kauli ya ‘siwezi kuishi bila yeye’ imepitwa na wanaoishi kwenye dhana hiyo ni malimbukeni. Bila yeye huwezi kuishi kwani yeye amekuwa hewa ya oksijeni?
Hee! Aende zake kama anaona wewe huna hadhi ya kuwa naye lakini akae akijua kwamba, penzi analolipiga teke wapo ambao wanalitafuta na hawalipati. Kwa nini ujizibie bahati yako kwa kumng’ang’ania mtu ambaye moyo wako umemtapika?
Jamani hakuna anayeshikilia pumzi ya mwingine, akikuacha huyo uliye naye maisha yako yatayumba kwa muda tu kisha utampata mwingine na maisha yako yataendelea wala hutakufa kama baadhi wanavyofikiria!
 Kuendelea kumpa nafasi ni kujipa presha na vidonda  vya tumbo bure, magonjwa ambayo ndiyo yanaweza kukutoa duniani na si kwa kumuacha huyo.
Kumbuka, ni wewe na maisha yako! Maamuzi yako ndiyo yatakufanya uishi kwa furaha au amani.
Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.