Sunday, October 1, 2017

AINA MBILI ZA KUSHINDWA KUSHIKA MIMBA (INFERTILITY)


KUNA aina mbili za wanawake kushindwa kushika mimba au kwa maneno rahisi, ugumba kitaalamu Infertility, ambao unatambuliwa kitabibu.
Aina moja huitwa kitaalamu Secondary infertility na aina nyingine huitwa primary infertility. 
Ugumba unaotokea baadaye maishani hujulikana kitaalamu kama Secondary infertility. 
Ugumba huu hugundulika pale ambapo wote wawili, mwanamke na mwanaume wameshawahi kupeana mimba mara moja maishani mwao na baada ya hapo hawajafanikiwa kupata au kutungisha mimba tena.
Utafiti umegundua kuwa asilimia kati ya 30 na 40 ya tatizo la ugumba huu huwakumba wanaume ambapo wanawake ni kati ya asilimia 40 na 50.
Asilimia kati ya 10 na 30 zilizobakia ya tatizo hili husababishwa kwa pamoja na matatizo kati ya wanaume na wanawake, japokuwa sababu halisi hazijulikani.

Kwa upande wa wanawake hufikia kilele cha kupata ujauzito (peak fertility) wakiwa kwenye umri wa miaka 20 na 25 ambapo aliye na umri wa kati ya miaka 35 na 40 ana uwezekano wa kupata ujauzito kwa asilimia 10 tu.

Ugumba wa asili (Primary infertility)
Ugumba huu hujulikana pale ambapo mwanaume na mwanamke hawajawahi kutungisha mimba kabisa maishani mwao licha ya kujamiiana kwa muda wa mwaka mmoja tena bila kutumia kinga yoyote ile ya kuzuia kupata mimba.
Jinsi mimba inavyotungwa 
Mimba hutungwa baada ya mwanamke kutoa yai kutoka sehemu maalum ya kutengenezea mayai ya kike iitwayo kitaalamu ovaries, kitendo hiki hujulikana kama ovulation. 
Baada ya hapo yai husafiri hadi kwenye mfuko wa uzazi ujulikanao kama uterus (womb) kupitia kwenye mirija ya uzazi iitwayo kitaalamu fallopian.

Mbegu moja (sperm) ya kiume ni lazima itungishe au iungane (fertilize) na yai au mayai ya kike (ovum au ova) wakati yai likielekea kwenye uterus.Baada ya mbegu ya kiume na yai la kike kuungana, muunganiko uliotengenezwa yaani embryo hushuka mpaka kwenye mfuko wa uzazi na kujiwekeza hapo, hali hiyo huitwa, mimba na hukaa hapo ili kiendelee kuwa kiumbe.

USHAURI
Tatizo la ugumba linaweza likawa ni la mwanaume au mwanamke pekee ingawa wakati mwingine wote wawili wanaweza kuwa na tatizo hili.
Wanawake wanashauriwa kukata shauri la kuzaa wakiwa na umri tulioutaja hapo juu, yaani kati ya miaka 20 na 25 kwani miaka kuanzia 35 kwenda juu uwezekano wa kupata mimba huwa ni mdogo sana (asilimia 10).