Thursday, October 4, 2018

Je unataka kuwa huru na kupata mafanikio makubwa maishani mwako?



Je umejikuta una wasiwasi wa mambo mengi pasipo kuwa na sababu yoyote ya maana ya kuwa hivyo? Wasiwasi ni ukosefu wa imani kuwa mambo yatakuwa vizuri. 


Usijutie sana kuhusu maisha yako na amini kuwa maisha ni mkusanyiko wa mitihani mbalimbali pamoja na faraja. Kwakuwa katika maisha yetu ya kila siku huwa tunawaza na kuwazua mambo mengi  leo nimeona niandike mambo ya kuacha kuwa na wasiwasi nayo au kuyafikiria sana ili uwe huru na maisha yako.

Usijisikie vibaya unaposhindwa kufanya vizuri.
Unaweza kuwa umefanya vibaya sana katika kazi au mitihani uwapo shuleni, usife moyo na kukata tamaa. Ni kawaida mtu kushindwa kufanya vizuri, kila mtu ana udhaifu wake mahali fulani hivyo ukijipanga upya na kuongeza bidii katika kujifunza wapi umekosea na wapi unahitaji kutilia mkazo zaidi hapo baadaye utaweza kuwa hodari na mahiri kwa kile ulichokifanyia kazi. Chukulia mapungufu yako kama ni mwalimu wa kukuonyesha makosa na udhaifu ulionao ili ujirekebishe na kuwa mtu bora.

Usiogope kushindwa .
Kila mtu ana njia yake kimaisha, hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi utashindwa ikiwa unajua kitu unachofanya sio kibaya au hakitadhuru maisha yako. Kuna mambo ya kuogopa lakini sio yote, wewe ndiye mwenye maamuzi ya nini ufanye na nini usifanye. Jaribu na ushindwe, thubutu kutenda na ushindwe lakini usife moyo na kuogopa kujaribu.

Usijutie sana kukosa fursa ya kupata kitu ulichotegemea kupata.
Inatokea hukubahatika kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wako kuwa unaweza kufanya kitu fulani au kuonekana unastahili. Penye watu wengi wenye nia moja kila mtu anategemea kushinda kama wewe.

Isikupite hii: Watu wenye sifa hii, ndiyo wanaofanikiwa.

Usifikirie maisha yako ya baadaye kuwa mabaya.
Hakuna sababu ya kuwa na mawazo hasi kwani maisha ni safari ndefu na hubadilika kila siku kwa kadri utakavyojitahidi kupambana na maisha yako. Ikiwa una matumaini kuwa mambo yatakwenda vizuri na kujitahidi kutafuta maisha yaliyo bora kwako ni wazi kuwa utashinda. Katika maisha hakuna hali ya kudumu hivyo mambo hubadilika. Muhimu ni kujituma kwa bidii bila kuchoka au kukata tamaa.

Usiwaze sana kwa nini watu hutenda mabaya.
Duniani kuna watu wa kila aina, kwa maana ya kila mtu ana tabia au hulka yake. Kuna watu wabaya na wazuri. Kwa kulijua hilo tegemea kukutana na watu tofauti  katika maisha yako. Amini kuwa kuna watu wengi wazuri lakini sio wote, hivyo uasi au ubaya wa mtu usikufanye uhuzunike au kubadilisha mtazamo wa maisha yako kwa sababu unastahili kuishi kwa amani, upendo na furaha.

Usitamani  na wala usijilinganishe na watu wengine.
Kutamani ni chachu ya maendeleo lakini tamaa inapozidi hukufanya ukose msimamo wa namna maisha yako unavyotaka yawe. Kama mwenzako ana mafanikio makubwa na umevutiwa na maendeleo yake ni vyema ukajifunza kutoka kwake. Hatuwezi wote kuwa na mafanikio makubwa kama matajiri wa dunia lakini tunaweza kuwa na mafanikio makubwa yaliyo bora kimaisha kulingana na matakwa yetu. 


Ni vyema ukawa na ufafanuzi wako wa nini maana ya mafanikio kwako iwe ni kuwa na pesa nyingi au mali tele, maendeleo binafsi ya kujiimarisha kitabia, kimahusiano n.k. Una uwezo wa kufanikiwa chochote kile unachotaka lakini itategemeana na jinsi utakavyojipanga na kujibidiisha katika utafutaji.

kuwa na imani.
Kuna hali ambayo ni ya kawaida kuwa na mashaka na mtu juu ya utendaji wake wa kazi au namna alivyo. Hofu yako inapozidi ni vigumu kuridhika na kazi au jambo lolote atakalofanya mtu mwingine. Kama una mashaka na mtu ni bora ukamweleza jinsi unavyotaka mambo yawe au mtafute mtu mwingine unayefikiri anaweza kufanya utakavyo. 


Hakuna mtu awezaye kufanya mambo yote mwenyewe, kugawana majukumu na kushirikiana kwa pamoja ndio mafanikio ya kuwa na mahusiano bora na utendaji mzuri wa kazi.

Isikupite hii: Aina 5 ya watu ambao hawafanikiwi katika maisha.


Usifikirie watu wengine watakuonaje iwapo utaamua kubadilika.
Wewe ndiye mmiliki wa maisha yako, rubani wa maisha yako na una kila sababu ya kufanya maamuzi unayoona yanafaa kuhusu maisha yako. Huwezi kuwa mtu bora pasipo kubadilika, huwezi kufanya mambo yenye manufaa kwako ikiwa huna maamuzi na maisha yako.   Unapodiriki kubadilika, mwenye nafasi kubwa ya kuamua nini ufanye ni wewe. 


Watu wengine wanaweza kukushauri , kukusihi na kukueleza watakayo lakini mwenye maamuzi ya mwisho ni wewe. Usiogope kufanya maamuzi yako binafsi ikiwa unajiona upo sahihi kwa kile unachoamini ni sawa. Kumbuka wasiwasi haubadilishi chochote, ni bora uamue kuchukua hatua au uwe mtulivu.