Thursday, September 27, 2018

KIUNGULIA CHA UJAUZITO NA NAMNA YA KUKIEPUKA

Kiungulia cha ujauzito au HeartBurn kwa kimombo ni miongoni mwa matatizo yanayowapata wanawake wengi wanapobeba mimba. Kiungulia ni hali inayopelekea mtu ajihisi kuungua au kuwaka moto sehemu ya katikati mwa kifua. Tatizo hilo huwapata wajawazito mara nyingi katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito, lakini pia wapo wakina mama wajawazito wanaopatwa na kiungulia miezi ya mwanzoni ya mimba. Ili kuelewa namna ya kuzuia kiungulia kisitokee ni bora kwanza tufahamu kiungulia kinasababishwa na nini wakati wa mimba. Kiungulia hutokea wakati kiwambo au valvu kilichopo kati ya tumbo na umio (esophagus) kinapolegea na kushinda kuzuia asidi ya tumbo isipenye na kurejea katika umio. Mimba huongeza kiungulia kwa sababu homoni ya progesterone hulegeza kiwambo hicho. Hivyo asidi inayozalishwa tumboni hasa baada ya kula hurejea katika umio na kuleta kiungulia. Kiungulia hutokea katika miezi mitatu ya mwisho ya mimba kutokana na fuko la uzazi kuwa kubwa na kubana utumbo mdogo na tumbo. Mbano huo wa tumbo hupelekea vilivyoko tumboni kusukumbwa upande wa umio au esophagus. 
Kwa kawaida kutokula vyakula vyenye kusababisha asidi na gesi tumboni, hupunguza kiungulia. Vyakula hivyo ni kama vinywaji vyenye gesi ya carboni, vyakula vyenye kiasi kikubwa cha asidi kama vile jamii ya maharagwe kama maharagwe, kunde, mbaazi n.k, nyanya, vyakula vyenye viungo, matunda kama machungwa na juisi ya machungwa, chocolates, vyakula vyenye mafuta mengi, grape fruit na hata kitunguu swaumu. Lakini pia inategemea mtu na mtu inabidi ujichunguze na kuona ni vyakula gani ukila unapata kiungulia na gesi. 
Zifuatazo ni njia za kujiepusha na kiungulia:

1. Kutumia baadhi ya dawa salama zinazozuia kiungulia na gesi wakati wa ujauzito. Kwa nchi zetu za Afrika Mashariki sote tunaifahamu dawa iitwayo Magnesium ambayo husaidia kuondoa tatizo hilo. Kama upo nchi nyinginezo pia natumaiani unaweza kupata dawa hiyo kwa msaada wa daktari wako. (Muhimu ni kupata ushauri wa daktari utumie dawa gani ya kuondoa heartburn au kiungulia ambayo ni salama wakati wa ujauzito).
2. Hakikisha unakula kiasi kidogo cha chakula na usile ukashiba sana. Kwa kuwa mama mjamzito huwa anasikia njaa mara kwa mara na anahitajia kula vyema ili aujenge vizuri mwili wake na watoto, basi ni bora chakula chake ukigawe katika sehemu kadhaa ndogo, na ale mara kadhaa, badala ya kula sana wakati mmoja. Suala hilo litafanya tumbo lake lisijae na kusaidia kuzuia asidi isipande juu ya tumbo na kusababisha kiungulia na gesi.
3. Jitahidi usinywe maji mengi sana baada ya chakula au wakati wa kula, kwani husaidia kuzalisha asidi tumboni kwa haraka na kuleta kiungulia.
4. Unaweza kula ubani au chewing gum baada ya kula, kwani ubani kutengeneza mate na mate hupunguza asidi.
5. Jitahidi usilale tu mara baada ya kula, subiri kama nusu saa hivi ipite ndio ulale. Unapolala usilaze kichwa moja kwa moja bila mto, bali tumia mito kuegemeza kichwa ili kuzuia asidi isirejee juu ya tumbo na kusababisha kiungulia.
Unapohisi kiungulia kunywa glasi ya maziwa au kula mtindi.
Na kama hali hiyo haijatoweka kunywa maji ya moto glasi moja yaliyowekwa kijiko kimoja cha asali.