Thursday, July 12, 2018

MADHARA YA KUCHAGULIWA MWENZI WA MAISHA KATIKA MAHUSIANO YA NDOA




Mtanzania? Ni imani yangu kuwa uko salama rafiki na unaendelea vizuri katika harakati zako za kila siku kuhakikisha unapata kile unachokitaka kwenye maisha yako. Tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya siku hii ya leo ameweza kutustahilisha tena kuiona siku hii ya leo. Kwa hiyo rafiki, tutumie muda huu wa leo vizuri kwani leo ni siku bora ambayo haitokuja tena kutokea katika maisha yetu hapa duniani.

Mpendwa rafiki, napenda kukualika tena katika makala yetu ya leo tuweze kujifunza kwa pamoja yale ambayo nimeweza kukuandalia siku hii ya leo. Hivyo basi, nakusihi ungana nami mwanzo hadi mwisho wa makala hii ili tuweze kusafiri wote kwa pamoja. Leo tutakwenda kujifunza juu ya madhara ya kuchaguliwa mwenza wa kuishi naye kwenye maisha ya mahusiano. Je ni madhara gani rafiki? Karibu rafiki tuweze kujifunza wote kwa pamoja.

Katika moja ya matatizo yanayowasumbua watu duniani basi moja wapo ni mambo ya mahusiano. Mahusiano haya yanaweza kuwa mahusiano ya uchumba, mahusiano ya ndoa na nk. Sasa katika mahusiano ya ndoa wapo watu wengi sana wanaruka hatua muhimu sana ambazo baadaye zinakuja kuwaumiza vibaya. Hatua hizo muhimu ni urafiki na uchumba kwa hiyo, ikitokea watu wamekutana ndani ya miezi miwili, mmoja na kukimbilia kufunga ndoa ndio hawa wale wanaokuja kujuta kwa nini walifanya maamuzi hayo.

Mpendwa msomaji, malengo mahususi ya somo letu la leo ni madhara ya kuchaguliwa mwenza katika maisha ya mahusiano. Ziko jamii tofauti duniani zenye utaratibu au utamaduni wa kuwachanguliwa watoto wao wenza pale wanapokua wamekaribia ule umri wa kuishi ya maisha ya ndoa kama mke au mume. Wazazi wa jamii za kuwatafutia watoto wao wenza bado wapo mpaka leo katika zama hizi za taarifa na pengine unafahamu watu ambao wanafanya jambo hili kwenye jamii iliyokuzunguka.

Kwa mfano, mtoto tokea akiwa mdogo anawekewa ‘’ oda’’ mapema kuwa wewe utaolewa na mtu fulani au utamuoa mtu bila kujali unataka au la. Kwa hiyo, tabia hii inawanyima watoto wengi kuwa na mtu Yule anayempenda badala yake wanakuwa na watu ambao siyo chaguo lao la kutoka moyoni. Utamaduni huu unakuwa ni kama kumnyima mtu kuishi maisha anayotaka hapa duniani.
Unaporuhusu wazazi wakuchagulie mwenza wa kuishi naye katika maisha ya ndoa kwanza inakuwa ni utumwa wa hali ya juu. Kwanini?

Kwa sababu kuchaguliwa kufanya kitu ambacho hukipendi katika maisha yako ni utumwa. Vivyo hivyo, kuchaguliwa mwenza wa kuishi naye ni utumwa pia. Unapokuwa unachaguliwa mwenza wa kuishi naye unakuwa unavunja hatua muhimu sana katika kuelekea maisha ya ndoa ambayo ni urafiki na uchumba. Kupitia hatua hizi unaweza kumchunguza mwenzako ni mtu wa namna gani, falsafa yake ya maisha ikoje, ni mtu chanya au hasi, ni mtu wa kuigiza maisha au ni mtu halisi anayeishi bila kuigiza maisha na mambo mengine mengi unayotaka kuyajua kutoka kwa mwenzako.

Rafiki, watu wanaoishi na wenza wao kwenye maisha ya ndoa kwa kuchanguliwa na kwenda kuanza kuishi maisha ya urafiki, uchumba na ndoa kwa wakati mmoja huwa wanashinda sana. unakuta mwenzako anaishi falsafa tofauti kabisa na wewe ulivyotarajia. kwa mfano, wewe falsafa yako ni kuishi chini ya kipato chako na unakuta mwenzako anataka kuishi juu ya kipato kwa kufanya mambo ambayo hayana ulazima kwenye maisha. Lakini kama ulikuwa umemgundua mwenzako na kumsoma vizuri katika hatua za uchumba ungeweza kufanya maamuzi mapema kwa kumpima kama mtu huyo anakufaa au la kulingana na vigezo vyako.

Kuchaguliwa mwenza wa kuishi naye katika zama hizi ni aibu kwa kweli kwani ni kuchaguliwa kufanya chochote ambacho hukipendi ni utumwa katika maisha yako. Kumbuka rafiki, hata mzazi akikuchagulia mpenzi ambaye wewe humpendi na ukakubali utakua umejichagulia wewe mwenyewe kuingia shimoni. Kwa hiyo, hata wazazi wakikuchagulia kuishi na mwenza ambaye wanampenda wao ni kama kuchaguliwa maisha ya kuishi hapa duniani. Licha ya kuchaguliwa maisha wewe ndiye utakayeenda kuishi hayo maisha na wala siyo wazazi watakaopata raha au shida, ukiingia shimoni wao hawatakuwepo bali wewe ndio utawajibika.

Hatua ya kuchukua leo; usikubali kuchaguliwa mwenza wa kuishi naye katika maisha yako. Ishi na mtu unayempenda kutoka moyoni, ishi na mtu ambaye mliweza kupitia hatua za urafiki, uchumba ukamjua vizuri tabia zake ni mtu wa namna gani. Fanya kitu ambacho unakipenda ndio furaha ya kweli katika maisha ambapo utapata mafanikio makubwa yenye furaha na ubora wa hali ya juu.

Kwa kuhitimisha, tunaishi karni ya ishirini na moja na hatuko tena katika zama za mawe bali tupo katika zama za taarifa. Kuwa chachu ya mabadiliko kwa kuvunja utumwa huo katika jamii uliyopo siyo unasoma na kupata elimu ya juu bado ukirudi nyumbani wazazi wanakushurutisha kuoa au kuolewa na mtu Fulani bila ya ridhaa yako mwenyewe. Wewe ndio mwenye maamuzi ya maisha yako kwa sababu hakuna mtu mwingine atakaye ishi maisha yako zaidi ya wewe mwenyewe.