Thursday, July 19, 2018

CHOMBEZO LA LEO BARUA YA KUSTAAJABISHA


Mpenzi Kiswahili,
H
HABARI, ni matumaini yangu makubwa kuwa u-mzima wa afya tele. Utakapokujua hali  yangu, mimi ni mzima wa siha njema, ila hofu na mashaka ni juu yako wangu wa moyoni.
Mpenzi Kiswahili,
Dhumuni la kuandika waraka huu kwako ni kutaka kukueleza yangu mengi yaliyo moyoni ambayo kwa kweli siwezi kuvumilia kukaa kimya mbele yako na kuwa nimeshindwa kabisa kuishi bila wewe mpenzi wangu. Sihitaji kuyumbisha maneno katika jambo hili ila nataka kukueleza kinagaubaga na utambue wewe pamoja na ahali zako kuwa, tangu nilipoanza kukufuatilia mwaka ule hukuonesha pingamizi kwangu kwa kuwa ulitambua vyema malengo yangu kwako. Hukuonesha majivuno nilipokuambia wewe ni mzuri, hukufanya mapozi nilipokuambia nakupenda, hukuleta maringo nilipokuhitaji nyumbani kwangu, hukuonesha kukerwa kila nilipokuambia tutoke kwa matembezi na zaidi ya yote, ulinionesha mapenzi ya kweli na kunikumbatia kila sehemu tuliyokuwa pamoja.
Mpenzi Kiswahili,
Waneni hunena “Ukipenda Boga, penda na Ua lake”. Ni kweli kabisa mpenzi, ndiyo maana mimi nakupenda wewe Kiswahili, pia nawapenda na nduguzo hasa yule aliye na watoto wawili, naye si mwingine bali ni Fasihi na mwanawe mkubwa Fasihi Simulizi na nduguye Fasihi Andishi. Nampenda pia Isimu na wanawe wote kuanzia Fonolojia, Mofolojia, Sintaksia hadi Semantikia.
Mpenzi Kiswahili,
Mimi nakujua asili yako kwa kuwa umewahi kuniambia ingawaje kuna baadhi ya watu wanadai kuwa, eti wewe umetokana na bibi kizee wa Kiarabu ambaye aliwahi kufika maeneo yetu dahari nyingi jambo ambalo baadhi yao hulishadadia na kutolea mifano mingi hasa kwa kuwa asilimia kubwa ya maungo yako yanaoonekana yametokana na bibi kizee huyo. Pia kuna ambao hudai kuwa eti wewe umetokana na mchanganyiko wa bibi kizee huyo wa kiarabu na mzee mmoja ambaye aliwahi kuishi hapa miaka mingi iliyopita na kuwa baada ya mzee huyo na bibi kizee hicho kukutana, ulizaliwa wewe kutokana na wawili hao kutoelewana katika mazungumzo yao.
Mbali na hao, pia kuna wengine wanaendelea kukufuru kwa kukupa asili isiyostahili, lakini hili halinipi shida kwani wewe umekwisha niambia kila kitu kinachokuhusu na kunisisitiza nisiwe na wasiwasi na uzushi wakuzushiao hao watu wasioijua asili yako.
Kuhusu hilo tu, mimi sina mashaka mpenzi wangu kwani mimi naamini moja kwa moja kuwa wewe ni mzaliwa wa hapa hapa na asili yako ni kule maeneo ya Kameruni kwa mzee Bantu. Ndiyo, ni kweli, kwani unafanana kimaumbile na wale nduguzo wengine waliosambaa karibu eneo zima la kusini mwa Bara Afrika kama vile Baganda, Lingala, Gikuyu na wengineo.
Pia unafanana sana na wapwazo Kimakonde, Kingoni, Kihaya, Kigogo na wengi wanaopatikana katika nyumba hii na hata wale walioolewa na kuoa sehemu mbalimbali barani humu.
Mpenzi Kiswahili,
Pamoja na mapenzi yangu mazito kwako, lakini kuna watu wengi wajinga wasiokupenda, kukujali wala kukuthamini, na hawapendi vile ninavyokupenda. Wanadiriki kunibeza eti kwa sababu nakupenda na kukuahidi kufa nawe na nakusihi kutokuwa na wasiwasi kwani nimegundua furaha niliyonayo inatokana na penzi lako la dhati kwangu. Nakiri pia kuwa, kebehi, kejeli, dharau na matusi nayotukanwa kila siku, havina nafasi kwangu ya kupunguza mapenzi kwako kama ambavyo kelele za mkojo zisivyoweza kubomoa choo.
Mpenzi Kiswahili,
Naomba pindi upatapo waraka huu, utambue kuwa naweza kuwa na pesa nyingi, vitu vingi vya thamani, nyumba nyingi za fahari na marafiki wengi, lakini nakiri vitu hivi havifui dafu mbele ya penzi lako la kweli na nimeamua kukuandikia waraka huu kwa nguvu zangu zote na utambue kuwa nafanya hivi si kwa shinikizo toka kwa mtu yeyote ila ibaki siri ya mapenzi yetu wawili-mimi na wewe.
Hapo awali niliamini kwamba unapokuwa na mpenzi, basi wewe ndiyo huwa bora zaidi kuliko mpenzi wako, lakini sivyo ila nilikuwa najidanganya. Sasa nimegundua kuwa wewe mpenzi Kiswahili ni bora kwangu na utaendelea kuwa hivyo daima. Sifikirii kukuacha ingawa nakiri kuwa kuna wehu wamewahi kunishauri hivyo.
Mpenzi Kiswahili,
Daima wewe ni thabiti, imara, mwenye msimamo na unayeheshimu maamuzi yako, unampenda anayekupenda, unamthamini anayekuthamini na kumjali anayekujali. Nakumbuka ulivyokuwa na sura nzuri na umbo la kuvutia kipindi kile tunasoma shule ya msingi, ambapo wengi tulianza harakati za kukumiliki. Kwa kweli ulikuwa ni mzuri sana. Nakumbuka wakati huo nilianza kukufuatilia taratibu, lakini hukuonesha ushirikiano. Hata hivyo sikukata tamaa na tulipomaliza shule ya msingi, tulibahatika kwenda pamoja shule ya Sekondari. Ni wakati huu ambapo sikuelewa kama ulikuwa unanipima imani ama la! Kwani tulipoingia tu mwaka wa tatu, ulinifuata na kuniambia umenikubalia ombi langu la siku nyingi tangu tunasoma shule ya msingi. Nilifurahi sana, tena sana!!!
Mpenzi Kiswahili,
Nakumbuka pia ahadi zako ulizowahi kunipa kuwa, endapo nitakupenda, kukulinda, kukuthamini na kukujali, basi utanifanyia mambo mazuri, nami nilikuahidi kufanya kila ulilonitaka kufanya kuhakikisha tu unakuwa na furaha wakati wote.
Tuliendelea na penzi la dhati hadi pale tulipomaliza kidato cha nne na kujiunga kidato cha tano na sita, lakini tulipotezana baada ya kuhitimu kidato cha sita. Kwa kweli nilipata taabu sana kuishi bila wewe kwani nilikuzowea, nilikutafuta sana na naamini hata wewe uliumia sana kunikosa katika kipindi hicho na ulikuwa unanitafuta.
Mpenzi Kiswahili,
Nashukuru kwamba baada ya kupotezana kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita, niliona tangazo sehemu fulani hivi kuwa upo Chuo Kikuu cha Dodoma na ulikuwa unanitafuta. Jambo zuri ni kuwa uliweka mawasiliano yako ili nikupate kwa urahisi. Mara tu tulipokutana tena kwa mara nyingine, mpenzi ulinikumbatia kwa furaha huku ukibubujikwa machozi ambayo sikujua kama machozi hayo yalikuwa ya furaha ama huzuni hadi pale ulipofungua kinywa chako na kuniambia kuwa mara tu tulipopotezana, ulikutana na watu ambao hawakuwa na mapenzi ya kweli na kuwa walikunyanyasa, walikutesa na hawakukuthamini wala kukujali.
Lakini pamoja na yote hayo, jambo la kustaajabisha na kushangaza ni kwamba, pamoja na kuteswa na kunyanyaswa sana, bado umeendelea kuwa yule yule Kiswahili mwenye sura nzuri yenye kung’ara na umbo la kuvutia na kuwa mvuto huo unaongezeka kila leo na umenawiri mara dufu. Sikuamini uliponiambia hivyo, lakini sasa nimeamini kuwa wewe ni mpenzi mwema usiyestahili aina yoyote ya mateso, manyanyaso wala bughudha yoyote.
Nakupenda sana Kiswahili wangu, ahadi yangu ya kukulinda, kukuthamini na kukujali ingali bado iko pale pale, tafadhali naomba unipende na utimize ahadi zako kwangu.
Mwisho kabisa, mpenzi Kiswahili naomba utambue kuwa mimi ni yule yule, sibabaishwi na wageni ambao kuna baadhi ya rafiki zangu wamezuzuka nao eti kwa sababu hao wageni ni weupe sijui! Wekundu sijui! Mara ooh, wanasafiri kwa Eropleni nawe waenda kwa miguu, tena peku. Mimi siwajali nakupenda wewe tu, Kiswahili wangu.