Friday, October 20, 2017

Dondoo 14 za Uvaaji ili Utoke Bomba Zaidi na kukuza Utanashati na kuonyesha Uzuri Wako.

Fasheni ni mada kuu inayosumbua kichwa wanaume wengi kwa kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, wengi wamegundua kuwa katika muonekano mzuri na kutoka bomba kimavaza sio tena sekta ambayo wanawake pekee ndo wanaotakiwa kuitilia mkazo, uhalisia wa fasheni unaongeza thamani ya muonekano wa mtu katika kila nyanja ya maisha ya siku hizi iwe kikazi, kijamii, kibiashara hata kibinafsi.

Japo kuna watu bado watataka kuleta ubishi, kiukweli na kiuhalisia wa maisha haya yalioingiliwa utandawazi na tekinolojia, mwanaume aliyevaa kinadhifu zaidi na kwa muonekano wa kitanashati na kupendeza siku zote lazima atatupiwa jicho la pili, japo tabia nazo ni muhimu ila hakuna atakayesema "Mmhn.. Cheki jamaa alivyo na vichekesho."

Kwa dunia ya sasa, ni vizuri kuendana na fasheni na kuwa na staili ya uvaaji ambayo itakupa utu na heshima, Kiumeni.com tumekuandalia ndoondoo 14 za fasheni zitakazo kuweka nadhifu, kuonyesha utanashati wako na kuukuza uzuri wako uliojificha mara dufu zaidi.

1. Nguo inayoendana na mwili wako ndio ufalme. Kitu ambacho unaweza kufanya mabadiliko kwenye nguo zako ni kuzipunguza kuendana na mwili wako, usiipenguze ikakubana sana au ikapwaya sana. Nguo ili ikutoe kiutanashati lazima iendane kwa jinsi mwiliwako ulivyo, ikukae kama vile umezaliwa nayo.

2. Ukivaa nguo vaa katika uhali wa kawaida. Hakuna kitu kinachopoteza utanashati wako hata kama nguo iwe nzuri kama kuvaa nguo bila mpangilio, ukivaa nguo usivalie vito vingi, kuweka pete nyingi na mikufu mingi shingoni utaonekana limbukeni, usivae kama msanii kama vile unaenda kufanya shoo, kama ukitaka kuonekana umependeza vaa nguo katika uhali wa kawaida, kama ni vito usizidishe zaidi ya vitatu hapo nimejumlisha cheni, mikufu na pete.

Unaweza kuongeza muonekano kwa kuvaa saa nzuri kuonyesha unajali wakati.

3. Kuwa mwangalifu na nguo unayoivaa juu ya nguo zingine. Sweta zingine huwa ni kubwa mno au zinakuwa zimekubana kupitiliza, ili utoke bomba mwili wako juu na chini unapaswa uendane, kama umevaa bwaga juu (nguo kubwa), basi na chini vile vile nguo unayotakiwa uvae inatakiwa iendane na ya juu.

4. Usiende kununua nguo peke yako. Mara nyingi ni ngumu kumwamini muuza nguo sababu yeye yupo pale ili auze nguo, sidhani kama anaweza kukupa ushauri uache kununua nguo yeye mzigo umgomee kuuzika, ukiwa na jamaa au rafiki wakati wa kununua ngua atakupa ushauri mzuri ni kipi ununue na kipi uache ili kupata nguo zinazokupa mvuto zaidi.

5. Usichukulie pupa vitu vidodo vidogo. Angalia shati lilivyokukaa, kama umevaa skafu angalia inavyoendana na nguo. Kama ni tai angalia jinsi ulivyoifunga, unaweza kuwa unatembea kumbe mifuko imetokelezea nje, na kama hujui kufunga tai ni vizuri ukamtafuta mtu mwenye utaalamu huo akufungie na kukufundisha pia.

6. Wekeza kwenye viatu vizuri. Kwa wanawake kitu cha kuanza wakimuona mwanaume humchunguza na kumwangalia juu hadi chini, akifika chini huangalia viatu vyako ambavyo vitampa taswira zaidi juu ya ulivyo na msimamo wako kimaisha, vikiwa visafi, vyenye mng'ao na kukaa vizuri nadhani hata wewe unaweza tabua ni fikra gani zitakuwa zinatembea kichwani mwake, wanaume wengi huwa hawavitii mkazo viatu, anaweza kuosha kila kitu ila viatu akaacha, onyesha wewe ni mwanaume mtanashati na mwenye radha flani kwa kuwa na viatu nadhifu zaidi.

7. Usivae matangazo au nembo kubwa kwenye nguo. Unapokuwa unavaa nguo yenye nembo kubwa au tangazo unakuwa kama ubao wa matangazo ya kulipia, unashusha uthamani wako na muonekano wako kwa ujumla, tsheti za makampuni haziwezi kukamilisha unadhifu wako, vaa tisheti yanye v kwenye shingo na piga jinzi yako kwa muonekano mulua zaidi.

8. Usinunue nguo kisa umeiona imevaliwa na msanii au mtu flani. Angalia usiwe unanunua nguo kwa sababu ndo mtoko mpya uliouona, angalia mavazi na staili unayoipenda. Watu wengi hununua nguo kwa sababu ni mtoko mpya na kujikuta na nguo nyingi ambazo hawazivai, tafuta nguo nzuri ambazo hazitoki kwenye wakati na ambazo unazipenda na kuendana na wewe na pia zenye kukuongezea mvuto zaidi.

9. Usinunue nguo kwa sababu ya jina. Kabla hujaamua kununua kitu jiulize unanunua kwa sababu umekipenda na umeipenda staili ya nguo ilivyokaa au unanunua kwa sababu imetengenezwa na mtu flani?, jiulize tena iwapo kweli ungekinunua iwapo kusingekuwa na hiyo nembo ya mtengeneza nguo unayempenda.

10. Angalia na tilia mkazo na kuitengeneza taswira yako. Wekeza muda na hela kwenye taswira yako, angalia ni staili gani ya nguo inayoendana nawe, nguo gani inakutoa vipi na fasheni unaielewaje.

11. Muulize rafiki yako anauonaje muonekano wako. Ni vizuri kujua ili kuelewa ni aina gani ya sataili inakukaa vizuri mwilini kwa kuwauliza wale wa karibu yako walio wawazi kwako, kama nguo haijaendana kwa kiaina flani na wewe ni vizuri kuelewa na kujua ili ujue ufanye mabadiliko gani.

12. Ujali muonekano wako wa mwili na uso. Paka mafuta yanayoendana na wewe, yanayoendana na ngozi yako ili iwe angavu na nyororo, jaribu kuwa unanyoa mara kwa mara, tinda nywele na ziweke vizuri ndevu zako kwa muonekano unaovutia zaidi, na ni vizuri ukawa na kinyozi wako atakayeweza kukufahamu kichwa chako kilivyokaa na ni staili gani ya nywele akikunyoa unapendeza kiutanashati zaidi.

13. Fanya majaribio kwa staili. Ukifanya majaribio utaelewa nguo gani inaendana na wewe, staili gani ya nguo inayokufaa zaidi na kipi ufanye kuongeza muonekano wako kwa utanashati zaidi.

14. Vaa mavazi kwa mpangilio wa rangi. Sio rangi zote zinaendana, hata rangi yako ya ngozi inaumuhimu pia kwenye mpangilio wa rangi za nguo unazozivaa ili upendeze na kuonekana mounekano wako wa thamani zaidi, jaribu rangi mbali mbali ili kujua na kuzoea ni rangi gani ya nguo inaendana na ipi, na pia kujua ni rangi gani ambazo hazipaswi kuvaliwa pamoja. Mpangilio wa rangi ndo huleta pendezo la nguo, viatu na mkanda kwa muonekano ulio bomba zaidi.