Sunday, March 25, 2018

Matatizo yako na jinsi ya kujifariji mwenyewe


Katika hali ya kawaida kila mwanadamu anahitaji kufarijiwa juu ya matatizo anayokumbana nayo kwa namna mbalimbali maishani. Mkwamo na vifungo vya hali ngumu ni suala linalohitaji msaada wa faraja kama tiba mbadala.

Hata hivyo uchunguzi unaonyesha kuwa karne tuliyo nayo kwa sasa, hali ya watu kujali na kujitolea kwa ajili ya wengine inaonekana kunyauka siku hadi siku. Mume, mke, ndugu, matajiri na watu wenye uwezo wanaonekana kushindwa kutoa faraja kwenye matatizo ya watu. 

Maisha ya sasa kila mtu anaishi sawa na msemo wa ‘abiria achunge mzigo wake.’ Aidha, kasumba ya kutegemea msaada wa kufarijiwa inatajwa kuwa mzigo unaoelemea wanadamu nyakati hizi hasa pale unapokuwepo ukweli kwamba wafariji hawapo au wamepungua kabisa ulimwenguni.

Jitihada za wanasaikolojia ulimwenguni zimekuwa zikijaribu kutafuta jibu na la tatizo hili la nini kifanyike ili watu waweze kufarijika bila kuwategemea watu wengine? Msingi wa utafiti huo ni kupata suluhisho linalokwenda na wakati kwa watu kuvunjika moyo na kuangamia kwa ukosefu wa watu wa kuwafariji.

Kama wanadamu tunashida zinazotusonga, tumedhurumiwa, tumefiwa na tuliowategemea na kuwapenda, tuliowaamini wametusaliti, tunaumwa magonjwa sugu, ni masikini wa kutupwa, tuna hitaji la faraja, lakini ndugu zetu tunaowategemea wamegeuza na kushupaza shingo, yaani hawataki kutusaidia hata kidogo. Sasa je, tufanye nini? 

Njia pekee inayoweza kutusaidia kukabiliana na maisha magumu ambayo hayana watu wa kutupenda, kutusaidia, kutuhurumia na kutujali, ni sisi wenyewe kuchukua jukumu la kuzifariji nafsi zetu na njia za kufuata ni hizi:

TUSIKOSOE UTU WETU
Tatizo kubwa linalowakabili watu wengi ni kuukosoa utu wao. Ndiyo maana wanakimbilia kuamini kwa wengine kwamba wasipoweza wao ndugu na jamaa zao watawasaidia.

Udhaifu huu wa kujikosoa ndiyo unazaa tunda la kuhitaji faraja kutoka kwa watu. Lakini jambo linalosikitisha zaidi ambalo liliwahi kumchekesha Tara Parker-Papa Mwandishi wa Blogu ya afya aliyochangia kwenye Tovuti ya New York Times ni pale mtu anaposubiri sauti toka kwa mwingine imwambie POLE!.

Ni wazi kwamba hatuwezi kusubiri sauti za pole kwa sababu nasi tunazo, tunachotakiwa kufanya ni kuziambia nafsi zetu. Zaidi ya hilo, kukiwepo na hitaji lolote la pesa au nguvu toka kwa mtu kutuwezesha kufarijika, si faida kwetu kusubiri zije wakati wenye nazo hawataki kutupatia.

Sisi wenyewe kama binadamu tunaweza kusimama peke yetu na kujipenda kwa jinsi tulivyo bila kuainisha na kujali upungufu wo wote tulio nao kwa vile matatizo ya mwanadamu hayajapata kumalizwa na uwezo wa mtu uwe wa kuazima au wa kwake mwenyewe. Lazima tujiwekee mazingira ya kujithamini sisi wenyewe.

Yamkini nitakuwa sawa nikisema, matajiri tunaosubiri watufariji kwa misaada yao nao wana shida zinazowatoa jasho. Hao ndugu, rafiki na jamaa zetu tunaodhani wamekamilika kimaisha wana yao yanayowaondolea faraja. Huo ni ukweli usiopingika.

TUTAMBUE KINACHOFARIJI
Kwa bahati mbaya watu wengi hawatambui kitu kichofariji ndiyo maana wanakimbilia kutegemea msaada. Lakini ukweli ni kwamba mawazo yetu ndiyo faraja pekee ya maisha. 

Tukijikubali, kujipenda na kujiwazia mema hatutafadhaishwa na hali ya wenzetu kutojali shida zetu, badala yake tutafurahia matatizo yetu kwa taraji la yote yanapita. Leo naomba niishie hapa wiki ijayo tutachambua kwa kina tofauti ya maneno BINAFSI na UBINAFSI ambayo ndiyo yanachangia kwa kiasi kikubwa sana watu kutegemea faraja kutoka kwa watu wengine. 

Matatizo yako na jinsi ya kujifariji mwenyewe-2

Zaidi ya saa 126 tangu niandike makala haya kwa mara ya kwanza wiki iliyopita, nimejiridhisha kuwa imekuwa ni vigumu kwa watu wengi kutofautisha UBINAFSI na BINAFSI.

Kutokujua tofauti kubwa iliyopo kati ya maneno hayo, kunaweza kuwa msingi wa matatizo ya kimaisha kwa mwanadamu na ukosefu wa faraja.

Kama lilivyo jina la kolamu yangu JITAMBUE, watu wengi hawajitambui na kujithamini, ndiyo maana wanadhani wamezaliwa ili wateseke hapa duniani.
Ni ukweli usiopingika, kila mmoja wetu angejua kusimama vema kwenye mhimili wa maisha yake tungepunguza kwa kiasi kikubwa mifadhaiko ya mioyo yetu na msongo wa mawazo usiokuwa na sababu.

Ifahamike kwamba mwanadamu wa kwanza aliumbwa BINAFSI (Mwanzo 2:7, “....mtu akawa nafsi hai”). Tafsiri ya neno hili inayopatikana kwenye kamusi ya kiswahili sanifu ya TUKI Toleo la Pili; “kwa nafsi yangu, kwa ajili yangu mwenyewe tu.” Mwisho wa nukuu.

Po pote pale duniani, mwanadamu binafsi ndiye mwenye kuishi kwa furaha, ndiye mwenye mafanikio, anayeweza kujifariji mwenyewe kwa umasikini wake, hali yake duni, ugonjwa wake sugu, taabu na shida zake, kwa sababu yeye ni mwenyewe tu.

Katika hali ya kawaida, nyuma ya binafsi kuna ubinafsi ambao unaelezwa kwenye kamusi kuwa ni “hali ya ya mtu kujifikiria na kujipenda yeye mwenyewe.” Mwisho wa nukuu ambayo kwa mtazamo inaelea hewani na kuwafanya wengi wadhani kuwa maana ya maneno haya ni moja.

Ingawa si mhubiri, nikiri kuwa ni mchunguzaji wa maandiko matakatifu ambayo yananirudisha kwenye kitabu cha Mwanzo 3:4-5, ambapo nabaini mwanzo wa ubinafsi ulivyoanza kwa mwanadamu wa kwanza.

Nukuu ya maandiko hayo inasomeka hivi: “Nyoka akamwambia mwanamke, hakika hamta kufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba, siku mtakapokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu kwa kujuwa mema na mabaya.”

Hapa wanadamu hawa wa kwanza wanatamani kuishi kwa ubinafsi, wanataka kufanana na Mungu wao. 

Ubinafsi halisi ninaouzungumzia ndiyo huu, ambao unamfanya mwanamke ambaye hajazaa atamani kuzaa kama fulani, amiliki gari, awe na maisha ya juu, mawazo ambayo humsogeza kwenye hali ya kujidharau na hatimaye kufadhaika.

Hii ndiyo sumu ya ubinafsi ambayo inaua, inadhoofisha na kuondoa hali ya uthubutu wa kukabiliana na matatizo yetu kama wanadamu na kutufanya tulilie kusaidiwa na kufarijiwa na wenzetu.

Msomaji wangu, kuanzia leo fahamu kwamba ukifadhaishwa na cho chote ujue unaumizwa na ubinafsi wako unaokusukuma kutaka uwezo na mali za mtu mwingine uwe nazo wewe. 

Amini usiamini, mtu mwenye mawazo ya ubinafsi ikitokea eneo lote analoishi watu wote wakawa wagonjwa kama yeye, hawajaolewa, hawana kazi, masikini utashangaa kuona mwanadamu huyo anaishi kwa furaha, si kwa sababu ya mafanikio yake bali amekosa aliyemzidi wa kujifananisha naye.

Najua maisha binafsi ni magumu, lakini yanamafanikio makubwa sana. Kwani maisha kwa ujumla yana changamoto nyingi sana. Mimi nimejifunza kwa vitendo na kuamini yanafuraha na matumaini makubwa.
Geuza mtazamo wa matatizo yako na kujitambua, hakika kwa kufanya hivyo utaona utofauti wa kimaisha. Onyo, usiache kuyashughulikia kwa mtazamo chanya.

Hata hivyo, Mungu akinisaidia wakati mwingine nitazungumzia faida za ubinafsi kwenye safari ya mafanikio ya kimaisha, ingawa sitaeleza tamaa ya kutaka vya wengine viwe vyako, ila nitafafanua umuhimu wa kutaka kufanana na mtu fulani mwenye maendeleo zaidi yako.