Saturday, February 17, 2018

VIDONGE VYA UZAZI HAVILETI SARATANI - MTAALAM

 
MTAALAMU wa masuala ya uzazi wa mpango, wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Calista Simbakalia, amesema vidonge vya uzazi wa mpango havileti saratani ya uzazi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Simbakalia alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa mada katika semina ya kutambulisha uzinduzi wa mpango mkakati wa uzazi wa mpango utakaofanyika Machi 30, chini ya wizara hiyo kitengo cha Uzazi wa Mpango na Mtoto.
Alisema si kweli kuwa vidonge vya uzazi wa mpango husababisha ugonjwa wa saratani ya uzazi bali vidonge hivyo hutumika pia kwa matibabu ya ugonjwa huo.
“Kumekuwa na kundi kubwa la watu ambao wamekuwa wakiamini matumizi ya dawa hizo huleta saratani ya uzazi wakati ukweli ni kwamba zimekuwa zikisaidia kutibu ugonjwa huo.”
Simbakalia alisema kuwa mwanamke asiyetumia njia za uzazi wa mpango hubeba mimba kila wakati jambo linalomfanya muda mwingi autumie katika kulea watoto badala ya kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Alibainisha kuwa ubebaji mimba wa mara kwa mara humfanya mwanamke kuwa tegemezi sambamba na kuifanya familia husika kutopiga hatua za maendeleo.
“Mama atakapotumia uzazi wa mpango unamsaidia kutopata mimba ambayo hakuipanga; hivyo atatumia muda wake mwingi kufanya shughuli za kumuongezea kipato,” alisema.
Naye mratibu wa taifa wa shughuli za uzazi wa mpango nchini, Maurice Hiza, alisema uzazi wa mpango unasaidia kupunguza vifo kwa kina mama wajawazito sambamba na kuboresha afya ya mama na mtoto wake.
Alibainisha kuwa uzazi wa mpango pia huisaidia serikali kuboresha huduma za jamii kama elimu, miundombinu, huduma za afya ambazo zimekuwa zikilegalega kutokana na uwiano mdogo kati ya idadi ya watu na uwezo wa serikali.
Alisema wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamepanga kuwaelimisha wanaume ambao inadaiwa ndiyo kikwazo kikubwa cha kuwakubalia wake zao au wao wenyewe kutumia njia zinazotakiwa za uzazi wa mpango.
Aliongeza kuwa iwapo elimu ya uzazi wa mpango itayafikia makundi ya vijana wanaochipukia na wanaume wakaelewa dira ya taifa ya mpango mkakati wa kupunguza vifo vya kina mama hadi kufikia mwaka 2010 -2015 itafanikiwa kirahisi.
You might also like: