Monday, December 4, 2017

Kuna Madhara Mke Kuwa Muongeaji Sana Kwa Mume, Jifunze!


UMESHAWAHI kukutana na mwanamke anaongea sana? Yaani yeye ni bandika bandua. Likiisha hili anaingiza hili, anajua kila kitu. Ana ujasili wa kuzungumza kwelikweli hata kama waliomzunguka wote ni wanaume. Akianza kuongea jambo lake hakubali kushindwa. Anataka aongee, asikilizwe na ikiwezekana waliomzunguka wote wawe upande wake. Haoni aibu. Hajishtukii hata pale wanaume wanapokuwa kimya kumsikiliza yeye.
Mpira anaujua yeye. Siasa za Bongo, nje ya Bongo zote anazifahamu. Ukirudi kwenye ubuyu wa mjini ndiyo kabisa, anawajua Shilawadu kuliko hata ndugu wa ukoo wake. Mshipa wa aibu unakuwa kama umekatika hivi. Yeye ni kupiga soga, soga na yeye.
UKING’ANGANIZI
Sifa nyingine ya mwanamke muongeaji sana ni king’ang’anizi kweli. Akikusudia jambo lake, hataki lishindikane. Atang’ang’ania hadi kieleweke. Mwanamke wa aina hiyo ni hatari sana kwenye uhusiano. Asili yao ya kuongea sana, hujikuta wamepitiliza. Huharibu mambo kwa kuzungumza hata ambayo hayastahili kuzungumzwa katika muktadha husika.
Mathalan, anaweza kumsifia mwanaume fulani kupita kiasi na kusahau yeye ana wajibu wa kumpa sifa zile mpenzi wake. Tena anampa bila kupayuka. Anamsifia katika uwanja wao wa kujidai. Anamsifia katika eneo ambalo lina utulivu wa kutosha na si mbele ya kadamnasi.
Tabia ya kuongea sana wakati mwingine huzaa umbeya. Unapoishiwa pointi za maana, kinachofuata ni majungu. Utaanza kusema fulani kafanya hivi, mara fulani kafanya vile ilimradi tu uonekane unaongea.
TATIZO ZAIDI
Mwanamke anapokuwa mzungumzaji sana, haishii kwa wenzake au mitaani bali huwa anahamishia uzungumzaji huo hata kwa mwenzi wake, matokeo yake anasababisha madhara.
HUWAPA AIBU WENZI WAO
Wanawake wa aina hii mara nyingi huwapa aibu wapenzi wao. Mwanamke unatambulishwa kwa rafiki wa mpenzi wako, unakiteka kikao wewe unakuwa ndiyo mzungumzaji mkuu. Unamnyima mpenzi wako, haumpi kabisa upenyo rafiki uliyetambulishwa. Asilimia tisini ya mazungumzo yote unaongea wewe, wakati mwingine hugeuka aibu kwa yule aliyekutambulisha.
NI CHACHU YA UGOMVI
Kiasili, wanaume hawapendi kuongea sana. Wanapenda kuzungumza kidogo, vitendo zaidi. Ndiyo maana mwanamke anapokuwa muongeaji sana, ana asilimia nyingi zaidi ya kutofautiana na mwanaume wake.
HAIBA NJEMA YA KIKE
Hata kama unajua jambo fulani, mwanamke unapomuelekeza mwanaume wako, hupaswi kuwa mzungumzaji sana. Unaongea maneno mawili, matatu na wewe unampa nafasi mwenzi wako aongee. Mwanamke usipayuke. Ongea kwa lugha ya staha. Yenye madaha, laini. Sauti kavu yenye ubabe ya nini kwa mwanaume wako?
KUONGEA SANA KUNAZAA UBISHI
Mwanamke ukiwa muongeaji sana, mara nyingi kunakuwa na kamchanganyiko ka ubishi ndani yake. Ubishi huwa nalo ni tatizo lingine kwa wanaume. Wanaume wengi huwa hawapendi kubishana. Wanapenda kuzungumza kidogo, waeleweke.
Hawapendi mashindano. Mwanamke anayeongea sana, mara nyingi haishiagi kwa wenzake. Tabia hiyo anaihamishia kwa mumewe. Anapoidai haki yake, inapotokea wametofautiana basi anajua kweli kujitetea.
HAIBA YA KIKE NI KUJISHUSHA
Mwanamke unapaswa kuwa na aibu kidogo unapoongea na mwanaume. Siyo unakuwa macho makavu wakati unayeongea naye ni mwanaume. Kuna kale ‘kahaya’ f’lani hivi ka kike unakotakiwa kuwa nako. Ndiyo raha yenyewe ya kike kwa wanaume. Watakupenda kweli kuliko mwanamke unakuwa mkavu, huoni haya, huna aibu hata tone, nani atakupenda?
Jishushe pale inapobidi. Hautagharamia hata shilingi moja ukijishusha kwa mumeo. Hakuna atakayekushangaa akisikia unajishusha kwa mumeo. Hauwezi kuonekana mjinga eti kwa sababu tu umejishusha kwa mumeo. Sana sana itakuongezea thamani kwake, wanaume wengi wanapenda kuheshimiwa, ukijishusha ataona unamheshimu, atakupenda kwelikweli.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!