HAKUNA siku ambayo huwa nafurahi ndani ya moyo wangu kama inapofika leo! Unajua kwa nini? Kwa sababu napata nafasi ya kubadilishana mawazo na wewe msomaji wangu wa kona hii! Ni matumaini yangu kama uko poa, karibu kwenye uwanja huu mzuri.
Ipo kasumba inayozidi kushika kasi mitaani, kwamba ukiona mtu anakupenda, lazima umletee maringo au lazima umfanye alihangaikie sana penzi lako. Mara kadhaa sasa nimeshapokea malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali, wengine wapo katika uhusiano rasmi wa ndoa kabisa, wengine wapo kwenye uchumba na wengine wapo kwenye uhusiano wa kawaida.
Malalamiko yao ni kwamba, wenzi wao wanawatesa, wanawanyanyasa, wanawavunja mioyo yao eti kwa sababu tu wamewaonesha kwamba wanawapenda sana na maisha yao hayawezi kuwa na maana wakiwapoteza. Nimeshawahi kusema na naendelea kusema kwamba mapenzi yanatakiwa kuwa ya pande mbili, kwa kizungu wanasema ‘two ways traffic’! yaani usiishie tu kubweteka na kujisifu kwa sababu mwenzi wako anakupenda. Mapenzi ni hiyari, mtu anapokupenda anakuwa ameamua mwenyewe kwa hiyari yake kuwa mateka wa penzi lako.
Maana yangu ni kwamba hakuna mtu anayelazimisha fulani ampende fulani, ni hisia ambazo huja tu zenyewe ndani ya moyo. Kama ilivyo bustani, huwezi kuishia kupanda mbegu tu halafu uache bustani ijitunze yenyewe, ukitegemea kupata mavuno bora.
Hisia za mapenzi ni kama bustani, lazima zimwagiliwe, kupaliliwa na kuwekewa mbolea kila siku iendayo kwa Mungu. Ukishaona mwenzi wako anakupenda, maana yake umepanda mbegu ya upendo ndani ya moyo wake kwa hiyo ni jukumu lako kuhakikisha unaitunza ili ichipue, ikue, ichanue na baadaye kutoa matunda.
Haya yanawezekanaje? Ukishagundua mwenzi wako anakupenda kwa dhati, ni wajibu wako na wewe kumuonesha kwamba unampenda pia, unamjali na kumhakikishia kwamba hajakosea kukupenda! Siyo kwa maneno, bali kwa vitendo. Acha kumfanyia vituko, mpende, mheshimu na muoneshe kwamba unamjali kwa kumfanyia mambo mazuri. Wakati mwingine makosa hayaepukiki lakini lazima yawe ni makosa kweli ya bahati mbaya, siyo eti kwa sababu amekuonesha anakupenda au unajua kwamba anakupenda, basi akikupigia simu hupokei bila sababu yoyote, ukiona ‘missed call’ yake hujibu, meseji ndiyo kabisaa! Wengine wanaishi pamoja lakini hata mazungumzo lazima mwenzake ndiyo amuanze, asipofanya hivyo wataishia kupishana kimyakimya ndani kama maroboti! Mwingine akishajua kwamba anapendwa, basi anaamua kumuumiza makusudi mwenzake, mara leo usikie anatoka na huyu kimapenzi, kesho anatoka na yule, kama ni nyumbani atachelewa kurudi bila sababu, atakuwa mkali bila sababu yoyote, hataki uguse simu yake na vituko vingine kemkemu. Ni makosa makubwa sana kumfanyia mwenzi wako vituko eti kwa sababu tu unajua anakupenda! Itaendelea wiki ijayo.Comment