Tuesday, November 14, 2017

Utagunduaje Kama Mpenzi Wako Katoka Kukusaliti ? Soma Hapa

Miongoni mwa mambo yanayowafanya wapenzi wakose amani ni suala la usaliti. Katika makala zangu nyingi ambazo nimekuwa nikiandika kupitia ukurasa huu, kila nilipogusia ishu ya usaliti nilipokea simu na sms nyingi.

Wengi wamekuwa wakilalamikia jinsi wanavyoumia pale wanaposalitiwa au hata kuhisi kwamba kuna mtu mwingine wanashea penzi. Kiukweli hakuna kitu kibaya kama mtu unayempenda kujua ana mtu mwingine, inauma sana!

Inauma kwa sababu ishu ya uhusiano inaleta suala la uchoyo f’lani hivi kwamba ukiwa na mtu wako iwe ni yeye na wewe, asitokee wa kukumegea wala hata kunyemelea, mtu anayetaka amege penzi lako lazima utamgeuza adui.

Lakini licha ya hali hiyo, bado kila kukicha wapenzi wamekuwa wakisalitiana, kwa siri na hata kwa wazi. Kwa nini? Kwa sababu uaminifu umepungua kwa kiwango kikubwa sana. Swali ni je, mtu anawezaje kumzuia mpenzi wake asichepuke? Jibu ni kwamba ni ngumu sana.

Mtu mwenye nia ya kukusaliti, asiyetosheka na penzi unalompa, mwenye tamaa za kijinga akiamua kukuzunguka anaweza kufanya hivyo na wala usigundue. Ndiyo maana leo hii wapo wengi sana ambao wanasalitiwa lakini bado wamejenga imani kubwa kuwa wapenzi wao wametulia.

Na kwa taarifa yako sasa, bora usalitiwe ukiwa hujui kuliko kila mpenzi wako anapotoka unajua kabisa huko anakoenda si salama. Utaumia sana na kila wakati utakuwa huna amani ukijua kuwa hauko peke yako.

Swali lingine ni je, kama mpenzi wako ametoka kukusaliti, kuna namna yoyote ya kuweza kumgundua? Kwamba kama mumeo au mkeo karudi na huko alikotoka alikuwa na kamchepuko, unaweza kutambua?

Kimsingi katika hili kuna ugumu kidogo. Hata uwe makini vipi, kubaini kwamba ametoka kukusaliti inaweza kukuwia vigumu kutokana na kwamba, wasaliti wenyewe wako makini sana.

Ni tofauti na enzi zile ambazo mwanaume anaweza kwenda kuchepuka, asioge kisha akarudi nyumbani akiwa na lipsitick shavuni, love bites shingoni au ananukia ‘pafyumu’ ambayo hakutoka nayo nyumbani. Siku hizi watu wameerevuka, ataenda kwenye mambo yake na akirudi kama siyo yeye vile.

Ndiyo maana wataalam wa masuala ya mapenzi wanaeleza kuwa, usijihangaishe kumchunguzachunguza mwenza wako eti ili kutaka kujua kama alikotoka ni salama.
Wapo ambao mumewe akirudi nyumbani cha kwanza atachukua simu yake na kuanza kusoma meseji. Hivi unadhani ni mwanaume gani ambaye atarudi nyumbani akiwa na sms za mchepuko?

Wakati wewe unaichukua, mwenzako ameshafuta kila kitu hadi namba alizopiga na kupokea. Sasa ukijifanya unakimbilia simu ili kumtafuta mwizi, utakuwa unapoteza muda wako bure.


Kipi cha kufanya?

Hakuna mbinu za wazi za kubaini kama mwenza wako ametoka kukusaliti, sanasana unaweza kutumia akili zako. Kama siku kajisahau karudi na ‘love bites’, hapo ndipo unaweza kujua.



Au amerudi akiwa amechoka kuliko siku zote na ukimuangalia anakwepesha macho, yaani anakuwa hajiamini, jua umeibiwa.


Hapo kidogo unaweza kumtilia shaka, lakini pia anaweza kukuambia amechoka kutokana na kazi za kutwa nzima. Ndiyo maana kunakuwa na ugumu wa kugundua.


Na kwa taarifa yako sasa, hata kama atarudi na ‘love bite’ shingoni, unaweza kushangaa anakataa kabisa kwamba ametoka kufanya mambo yake, atakuwa tayari hata kuapia. Sasa mkifikia hatua hiyo utakuwa na kipi cha kushika?


Ndiyo maana tunasema, uhakika wa asilimia zote kwamba mwenza wako anakusaliti ni mpaka utakapomfuma laivu, lakini hizi dalilidalili wakati mwingine zinatupotosha.


Cha msingi hapa ni kuepuka kuishi huku ukimfikiria vibaya mweza wako. Hii kumchunguza kila wakati, kumnusa kila akirudi nyumbani, kumkagua mwili na kukimbilia simu yake akirudi nyumbani ni kujipa presha bure. Kama anakusaliti, ipo siku Mungu atakuangazia utagundua.


Lakini sasa, tukeshe tukiomba sana ili hata kama wale ambao tumetokea kuwapenda wanatusaliti, tusijue! Hivi unajisikiaje kujua kwamba mtu ambaye unampenda sana anakusaliti?


Je, ukigundua utakuwa na ujasiri wa kuchukua uamuzi wa kumuacha? Hakika ni ngumu sana kwani kumuacha mtu ambaye moyo wako umemzimikia si kazi rahisi. Ndiyo maana leo hii unaona mtu anamfumania kabisa mkewe au mumewe lakini anapiga moyo konde, anamsamehe na kuyaacha maisha yaendelee.


Hii yote ni kwa sababu, endapo kila utakapobaini kuwa unasalitiwa unaacha, basi utaacha wengi na kamwe hutapata mtu wa kutulia naye. Nasema hivyo kwa sababu hakuna utakayempata ambaye ametulia kwa asilimia zote, na kama yupo basi ni mmoja kati ya watu kumi.


Labda kwa kumalizia niseme tu kwamba kwenye mapenzi kuna sarakasi nyingi. Kusalitiwa kumekuwa kukishamiri kila kukicha kiasi kwamba huwezi kusimama leo na kujiaminisha kwamba uliyenaye hakusaliti.


Kikubwa ni wewe kujenga imani naye, kutopenda kumfuatilia sana huku kila kukicha mkikumbushana juu ya umuhimu wa kutulizana.


Madhara ya kuchepuka ni mengi kiasi kwamba ukigundua kuwa mwenza wako hatosheki na penzi lako, ana tamaa za kijinga, haoni hatari kukutengeneza ‘mtungo’, bora umuache ili asije akakuingiza kwenye matatizo makubwa