Dalili za ujauzito
- Kukosa hedhi
- Kichefuchefu
- Kujisikia mchovu
- Kukojoa mara kwa mara
- Matiti huwa laini na kuongezeka ukubwa
- Kuongezeka uzito
Ujauzito unapofikia miezi 4½, mama anaweza kusikia mtoto akijigeuza na mfanyakazi wa afya anaweza kusikiliza mapigo yake ya moyo kwa kutumia kifaa kiitwacho fetoskopu ambacho huwekwa juu ya tumbo la mama yake.
Mtoto atazaliwa lini?
Ujauzito huchukua takriban miezi 9 (miandamo ya miezi 10 au wiki 40). Kupata picha halisi lini mtoto atapozaliwa:Kwa mfano, chukulia kwamba hedhi ya mwisho ya mwanamke ilianza Februari 30.
Februari 10 + miezi 9 = Novemba 10 Novemba 10 + siku 7 = Novemba 17 Tarehe ya mtoto kuzaliwa inatarajiwa kuwa Novemba 17.
Jinsi ya kuendelea kuwa na afya bora wakati wa ujauzito.
Mama na mtoto wake wanaweza kuendelea kuwa na afya bora kwa:- Kupata chakula cha kutosha chenye virutubishi.
- Kupumuzika sana kila siku.
- Kuepuka kemikali, pombe, moshi, na sehemu kubwa ya madawa.
- Kupata huduma kutoka kwa mkunga au mfanyakazi wa afya mwingine ambaye anaweza kutibu, au kusaidia kupata matibabu kwa ajili ya tatizo lolote la kiafya ambalo linaweza kujitokeza.
- Upendo na huruma.
Kula chakula cha kutosha chenye virutubishi
Mchanganyiko wa chakula chenye virutubishi kitamfanya mwanamke awe na nguvu na afya; aweze kupata nguvu za kujifungua na kumhudumia mtoto. Kama mwanamke mjamzito hali chakula cha kutosha, inawezekana anawachia chakula wana familia wengine, au mama mkwe kwa nia njema katika uelewa wake amemwambia asile baadhi ya vyakula au asiongezeke uzito ili aweze kujifungua kwa urahisi. Kumbuka mwanamke analazimika kula chakula cha kumtosha yeye na mwanae. Hivyo anahitaji kula chakula zaidi kuliko watu wazima wengine na siyo kidogo kuliko wao.Wanawake wajawazito, kama watu wengine, wanahitaji mchanganyiko wa protini, mbogamboga,matunda, na wanga. Pia wanapaswa kula mara nyingi zaidi, wakipata vyakula vidogo vidogo kati ya milo ya kawaida siku nzima.
Zuia upungufu wa chembe nyekundu za damu (anemia)
Anemia (upungufu wa chembe nyekundu kwenye damu) hutokea sana wakati wa ujauzito. Husababisha kujisikia mchovu kila mara. Anemia ni hatari zaidi hasa kwa akinamama wajawazito kwa sababu damu hupotea wakati wa kujifungua. Hii inaweza kuzidisha upungufu huo na kusababisha mama kupoteza maisha. Zuia anemia kwa kula vyakula vyenye protini na wingi wa madini chuma, na pia kutumia dawa ya kuongeza madini chuma mwilini.Asidi ya foliki
Ukosefu wa asidi ya foliki (au vitamini ya foleti) kunaweza kusababisha hitilafu katika umbaaji wa mtoto na hata ulemavu. Chagua dawa za kuongeza madini chuma mwilini ambazo zinajumuisha asidi ya foliki, au dawa za kuongeza foliki mwilini.Vitamini A
Mbogamboga za kijani na matunda ya rangi ya chungwa huwa na vitamini A, kirutubishi ambacho kinahitajika kwa ajili ya afya ya macho. Mwanamke mjamzito anahitaji mbogamboga za kijani na matunda ya rangi ya chungwa zaidi kwa sababu vitamini A anayokula hutumika kwanza kukidhi mahitaji ya mtoto. Ukosefu wa vitamini A unaweza kusababisha kutoona usiku au upofu kwa ujumla.Epuka Matumizi ya Bidhaa Hatari
Moshi na sigara
Sigara na tumbaku huathiri mapafu ya mama na vinaweza kusabisha saratani na hata kifo. Moshi unaweza kusababisha mtoto kuzaliwa kabla ya muda wake au akiwa na uzito mdogo sana, au akiwa amekwisha kufa. Akina mama na watoto wao wanaweza hata kudhurika kutokana na watu wanovuta sigara karibu nao. Ikumbushe familia na wengine kuepuka kuvuta sigara katika chumba kimoja au kweye gari wanapokuwa na mama mjamzito au watoto.Pombe na madawa ya kulevya.
Mama mjamzito anapokunywa pombe, pombe hiyo huenda kwa mwanae na inaweza kusababisha hitilafu za kudumu kwenye ubongo wa mtoto na mwili wake. Kadri anavyozidi kunywa pombe nyingi ndivyo madhara kwa mtoto yanavyongezeka. Vivyo hivyo, madawa ya kulevya yakiwemo kokeni, bangi, unga na madawa mengine ni hatari kwa akinamama wajawazito na watoto wao.Madawa ya kawaida
Dawa nyingi anapozitumia mwanamke mjamzito pia humfikia mtoto wake. Kwa sababu watoto tumboni wanakuwa wadogo sana na wakiendelea kuumbika, dawa ambazo ni salama kwa mtu mzima zinaweza kusababisha hitilafu wakati wa kujifungua na hata madhara kwa mtoto. Hivyo akina mama wajawazito wanapaswa kuepuka kutumia dawa holela. Kupumzika na vinywaji laini — siyo dawa — ndiyo tiba bora zaidi kwa matatizo madogo madogo kama vile maumivu ya kichwa, maumivu ya tumbo, na mafua.
Isipokuwa tu kama una uhakika yanahitajika, ni bora zaidi kuepuka madawa wakati wa ujauzito.
- malaria.
- VVU na UKIMWI.
- maambukizi ya njia ya mkojo.
- maambukizi kupitia ngono kama vile klamidia, kisonono, na kaswende.
Dawa za asili na mimea/mitidawa zinaweza kusababisha madhara zaidi kuliko kutoa tiba. Kitabu kiitwacho Dawa, vipimo na matibabu (kinaandaliwa) kimependekeza njia za kuzingatia unapotaka kufanya maamuzi juu ya matumizi ya dawa za asili.
Epuka kukutana na wagonjwa
Ugonjwa wa Rubella ambao ni aina ya surua kawaida siyo hatari sana. Lakini unapompata mwanamke mjamzito unaweza kusababisha hitilafu katika viungo na hata ulemavu kwa mtoto akiwa tumboni. Katika kumlinda mtoto, mwanamke mjamzito anapaswa kuepuka watu wenye upele, hasa watoto, ambao mara nyingi hupatwa maambukizi hayo. Hata watoto wengine wa mama mjamzito ambao wanaumwa wanapaswa kuhudumiwa na wanafamilia wengine au marafiki. Kampeni ya chanjo kwa jamii nzima ndiyo kinga bora zaidi kwa wanawake wote.
Huduma ya mkunga au mfanyakazi mwingine wa afya
Mkunga mzoefu au mfanyakazi wa afya mwingine anaweza kumshauri mwanamke mjamzito jinsi ya kuishi na afya nzuri na salama, kutibu magonjwa yote ya kawaida na kupunguza kero, na kutambua lini mwanamke mjamzito anapohitaji kutafuta msaada kwenye hospitali au kituo cha afya. Wanawake wote wanapaswa kuhudumiwa na mfanyakazi wa afya mwenye huruma na ueledi wakati wa ujauzito, pale wanapojifungua na katika wiki zinazofuata.Chanjo
Mwanamke mjamzito anapaswa kuchanjwa dhidi ya pepopunda (tetanasi) mapema iwezekanavyo katika ujauzito. Anatakiwa kupewa chanjo nyingine wiki 4 baadaye iwapo atakuwa hajapata chanjo zote. Hii husaidia kuwalinda wote wawili-mama na mtoto wake.Vipimo vya Maabara
Vipimo rahisi vinaweza kugundua baadhi ya magonjwa mengi ambayo ni hatari kwa wanawake na watoto wachanga. Vipimo hivi huwatahadharisha mama na mfanyakazi wa afya kuanza matibabu mara moja, hatua ambayo inaweza kuzuia matatizo makubwa wakati na baada ya kujifungua. Ni busara kufanya vipimo dhidi ya:- anemia (kwa kutumia kipimo maalum cha himoglobini).
- kaswende.
- malaria (kwa kutumia vipimo ambavyo hutoa majibu haraka kwa maeneo ambapo malaria ni ugonjwa wa kawaida).
Kuna aina mpya ya vipimo vya VVU ambavyo havihitaji maabara na hufanyika kwa urahisi kwa kutumia kifaa kidogo kupangusha ndani ya mdomo au ukeni, au kuchukua tone la damu kutoka kwenye tundu dogo kwenye kidole. Ulizia kwenye kituo cha afya kilichoko karibu iwapo vipimo hivi hutolewa na serikali, au kama kuna shirika lolote ambalo linatoa huduma hiyo.