Sunday, November 12, 2017

TATIZO LA KUTOKWA NA MAJIMAJI SEHEMU ZA SIRI

Majimaji haya yanaweza kuwa mepesi au mazito, pia yanaweza kuwa ni usaha kutegemea na chanzo cha tatizo.
Mwanaume mwenye tatizo hili, majimaji yanaweza kutoka yenyewe na kujikuta amechafua nguo za ndani au asubuhi anapoamka anajikuta amechafuka.
Wakati mwingine unapojisaidia haja kubwa majimaji haya hutoka kama manii yakiwa yanateleza toka katika njia ya mkojo.
Kwa upande wa mwanamke, kutokwa na majimaji haya inategemea ni wakati gani, aidha wakati wa ujauzito au wakati ambao siyo wa ujauzito.
Hali hii ikitokea wakati wa ujauzito siyo dalili nzuri, wakati mwingine huhatarisha hali ya ujauzito. Katika kipindi ambacho siyo cha ujauzito, tatizo hili linapotokea huwa na vyanzo vingi.
Jinsi tatizo linavyotokea
Mwanaume mwenye tatizo hili, kama anatokwa na usaha, utakuwa na historia ya kufanya ngono zembe siku za nyuma na siyo muda mrefu sana. Endapo utakuwa na majimaji mepesi itategemea kama yanawasha au la, kama hayawashi basi aidha utakuwa una tabia ya kujichua au ulishawahi kuumia njia ya mkojo.
Majimaji yanapotoka na kuhisi muwasho katika njia ya mkojo, inaashiria maambukizi sehemu hiyo yanayoweza kusababishwa na Fangasi, Klamidia na Trikomonia.
Hali hii pia inaweza kuwatokea hata wanawake ambao wanaweza kupata matatizo ukeni na katika njia ya mkojo kama inavyojielezea hapo juu.
Mwanamke kutokwa na uchafu mzito ukeni inategemea na chanzo, aidha inaweza kusababishwa na mabadiliko ya mwili au maambukizi. Hali hii inategemea na uchafu au majimaji hayo yapo katika hali gani.
Mwanamke mjamzito na asiye mjamzito endapo atatokwa na uchafu mzito ukeni ambao hauna harufu wala muwasho, hilo siyo tatizo na maambukizi, ni mabadiliko tu ya mwili. Kwa mwanamke ambaye siyo mjamzito, hali hii inaashiria kutopevusha mayai na hawezi kupata ujauzito.
Uchafu wenye rangi aidha njano, rangi ya udongo au damu, au unatoa harufu, basi ni tatizo linalohitaji uchunguzi wa kina.
Dalili za tatizo
Kama nilivyoelezea jinsi tatizo linavyotokea, hali ya kutokwa na uchafu au majimaji ukeni huambatana aidha na muwasho, harufu au la.
Kama hakuna harufu au muwasho hali inapotokea kwa mwanamke tatizo linaweza kuwa katika mfumo wa homoni na hali inapotokea ikaambatana na muwasho harufu tatizo ni maambukizi.
Maambukizi yanaweza kuwa Kisonono au Gono, Kaswende, Klamidia, Trikomonia na Fangasi.
Matatizo haya yanaweza kuambatana na  maumivu katika njia ya mkojo, chini ya tumbo na kiuno kwa wanaume na hata kuathiri uwezo wa kufanya tendo la ndoa.
Kwa wanawake tatizo linaweza kuambatana na maumivu katika njia ya mkojo, maumivu ukeni, maumivu wakati wa tendo la ndoa, maumivu chini ya tumbo na maumivu ya kiuno.
Mwanamke pia hupoteza hamu ya tendo la ndoa, mzunguko wa hedhi huvurugika, kutopata ujauzito na kupoteza hamu ya tendo la ndoa. Matatizo haya humfanya mgonjwa apoteze hamu ya kula na mwili kuwa mchovu na kukosa raha.
Uchunguzi
Hufanyika katika kliniki za magonjwa ya kinamama. Muone daktari bingwa wa kinamama kwa uchunguzi wa kina.
Vipimo vipo vya aina nyingi kama vya damu, kupima shingo na mdomo wa kizazi, kupima uchafu utokao ukeni, kipimo cha Ultrasound na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa.