Saturday, November 18, 2017

MALEZI: KWANINI WATOTO WENGI WANAMATATIZO YA UTULIVU, USIKIVU NA KUSHUKA KWA UWEZO WA KUJIFUNZA?




















Ninaandika makala hii baada ya kukutana na wazazi wengi wakilalamika juu ya watoto wao, wengine wakiwaleta watoto wao ofisini kwangu kwa ajili ya msaada wa kisaikolojia na wengine wakisema wameshauriwa watafute msaada wakisaikolojia na walimu wa watoto hao mashuleni baada ya kuona watoto wao wanaugumu sana kwenye usikivu, utulivu “concentration” na hata kwenye uwezo wa kujifunza “low learning ability”. Utakubaliana na mimi kwamba ukiwasikia walimu wengi leo mashuleni, wengi hulalamika kwamba watoto wa sikuhizi wamekuwa wagumu kuelewa, wagumu kufundishika na wanatabia mbaya. Wazazi nao kwa upande mwingine wamezidi sana kulalamika kwamba malezi ya siku hizi ni tofauti sana na zamani. Imekuwa ngumu kulea mtoto mdogo sikuhizi, na kila mzazi anapata changamoto kubwa sana. Najua wengi tunamaswali, tatizo liko wapi? nini kinasababisha hali hii? Yamkini ulikuwa haujui au haufahamu kwamba chanzo kinaweza kuwa ni wewe mzazi, leo ninakuja na jibu kwako mzazi. Suluhisho liko mkononi mwako, jawabu linaanza na wewe mzazi.
Ni jambo la ukweli kabisa na limehakikiwa kitafiti kwamba leo watoto wanakwenda shule wakiwa wamechoka akilizao, watoto wanasinzia darasani na wengine wanalala kabisa, watoto wanakinai shule badala ya kuhamasika na shule. Wako watoto ambao inamchukua mzazi au mlezi masaa kumshawishi mtoto avae nguo za shule tofauti na awali ambapo mtoto anadamka hata kabla ya muda wa shule anatamani kwenda shule. Watoto hawana hisia na shule, hawana hisia na mambo ya kijamii yanayoendela shuleni “they are emotionally disconnected”. Ni vema kufahamu kwamba ubongo ni kitu kilaini sana kinachoweza kubadilishwa na mazingira, mazingira tuishiyo yanaweza kuufanya ubongo uwe imara au uwe dhaifu sana. Ubongo huu pia unahitaji kufunzwa, na kwa jinsi ubongo unavyofunzwa ndivyo unavyokuwa na kuendesha tabia ya mtu. Watoto wetu kwa kiasi kikubwa wapo vile walivyo na wanafanya yale wanayoyafanya kwa kadiri tulivyotengeneza ubongo wao. Kwa bahati mbaya kwa kiasi kikubwa wazazi wengi tumetengeneza ubongo wa watoto wetu vibaya, na hichi ndicho chanzo cha matatizo yote. Utaniuliza kivipi? Jibu hili hapa!!
1. Matumizi makubwa ya teknolojia
Siku hizi kunakila aina ya mashine au vitu vilivyotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa katika kumfanya mtoto atulie, asisumbue au asilie. Zamani kulikuwa na sehemu za kumweka mtoto mchanga akae pekeyake, sikuhizi sehemu ile imefungwa vikorokoro vingi kumfanya mtoto aweke mawazo yote kwenye hivyo vitu wakati mzazi akiwa anafanya mambo mengine. Watoto wanataka kuwa kwenye simu muda wote wakicheza michezo ya kompyuta “video games”. Teknololojia za michezo ya kompyuta iko katika uwezo wajuu sana katika hali ambayo mtoto huyu mwenye umri mdogo anapofika darasani ambapo mwalimu anatakiwa kumfundisha kwa kuzungumza akiwa mbele ya darasa na akitumia michoro iliyochorwa na mikono kwa ajili ya kiwango cha uelewa cha mtoto huyu, mtoto anapoteza hamasa. Pia maranyingi yale wanayoyaona na kujifunza kwenye michezo ya kompyuta hayahusiani sana na yale wanayojifunza darasani. Michezo hii inawafanya wengi wachoke akili au wachelewe kulala na hivyo kufika darasani wamechoka sana akili na wakiwa wagumu sana kujifunza.

Teknolojia kwa kiasi kikubwa imewatenganisha kihisia watoto na wazazi wao, watoto wakiwa kwenye gari na wazazi, kila mmoja anasimu au mashine ya kuchezea, hakuna anayemwongelesha mwenzake au kuongelea vitu vinavyowahusu wao. Uwepo wa mzazi kihisia kwenye maisha ya mtoto ni kirutubisho cha muhimu sana kwenye makuzi ya ubongo wa mtoto, kwa bahati mbaya sana watoto wetu wananyimwa kirutubisho hiki chamuhimu kwasababu tu ya kitu kiitwacho teknolojia. Hii inaweza kuonekana kama inawagusa watoto wachache wa familia zinazojiweza lakini ukweli nikwamba jamii hii inaongezeka kwa kasi sikuhizi maana kila mzazi anafikiri kumnunulia mwanae michezo hii ndio ukisasa na hapo tatizo linakuwa kubwa zaidi.
2. Watoto kutaka kile wanachokitaka na katika muda ule wanapokitaka
Sikuhizi mtoto anaishi maisha ya kubonyeza anachokitaka na kinatokea saa hiyohiyo, watoto hawaelewi tena kama kuna kitu kinaitwa “kusubiri” au “kungojea”. Watajulia wapi wakati hakuna tena mazingira ya ubongo wao kufundishwa kusubiri au kungojea? Utasikia mtoto anasema nina njaa, saa hiyohiyo mzazi anatafuta chakununua ampe, tena mtoto sio tu kusema ninanjaa, bali nataka chipsi, nataka soda, hawajui tena hata kusema naomba. Mtoto akisema tu nimechoka, mzazi anahangaika kutafuta kitu chakumfanya ajisikie furaha, kwamfano wakiwa kwenye gari, mtoto atapewa simu ili apumzike nayo. Sikuhizi kwenye familia za kati, mzazi akifika nyumbani tu, watoto wanaomba simu ili wacheze michezo ya kompyuta, mtoto akisema nataka simu, ni lazimu apewe afanye anachokifanya. Kwa bahati mbaya tabia hii inawafanya kuwa na furaha kwa wakati mfupi na baadaye kwenye maisha marefu ya mbeleni wanapata shida sana. Kwa kukosa uwezo wa kusubiri watoto wanakosa uwezo wa kuishi au kufanya kazi kwenye mazingira yenye msongo wa mawazo. Haiwezekani kabisa kwenye maisha mtu ashindwe kusubiri. Sio kweli kwamba maishani tunapata kila kitu tunachohitaji katika muda ule tunapokihitaji. Sasa kama mtoto anashindwa kuwa na uwezo wa kusubiri au kuvumilia basi ni dhahiri kwamba atapata shida sana kwenye maisha yake, tatizo ambalo limezaliwa na kukuzwa akiwa mtoto mdogo.
3Watoto ndio wameshika utawala
Watoto wetu wasikuhizi ndio wameshika utawala, watoto ndio wanaosema wanataka nini, wanapenda nini, nini hawataki, wanataka kwenda wapi, wapi hawataki kwenda, wanataka kuwa nanani na nani hawamtaki, wanataka kusoma wapi na wapi hawataki, wanataka kula kipi na kipi hawataki. Kwa bahati mbaya wazazi wanadhani ni sifa kushadadia hali hii, utasikia mzazi anasema “yani wanangu hapendi kabisa uji”, yani mwanangu hampendi kabisa fulani”, “yani mtoto wangu hapendi kabisa kulala mapema”, “yani mwanangu hapendi kabisa kuamka mapema, anapenda kulala hadi muda anaopenda yeye”, “watoto wangu hawapendi wageni”. Hivi wewe ni mzazi au wewe ndio mtoto? Hivi nani anatakiwa kumuongoza mwenzake, mtoto kumwongoza mzazi au mzazi kumwongoza mtoto? Watoto sikuhizi ndiowameshika “remote control” kuwaongoza wazazi wao na wazazi wana “dance” kulingana na watoto wanachokitaka. Leo watoto ndio wanaoamua nini kiliwe nyumbani. Wasichotaka hakitoliwa na wanachotaka ndicho kitaliwa. Wazazi hembu turudi kwenye misingi yetu tuliyoipoteza, tena turudi haraka sana. Kama watoto kila siku watataka kula wanachotaka wao hata kama hakina manufaa kwenye afya zao, iko wapi kazi ya mzazi kuhakikisha afya ya mtoto? Ndio maana vitambi na mashavu yamewazidi watoto sikuhizi, baba anakitambi, mama anakitambi na watoto vile vile. Ndio maana magonjwa yasiyo yakuambukiza “non-communicable diseases” hayaishi kwenye familia zetu. Kama watoto wataamua wenyewe walale sangapi, unategemea wataamka sangapi? na je watakuwa na akili mbichi ya kujifunza kesho yake wakiwa darasani? Watoto leo wanakiu sana ya kuwa watu fulani au kufikia malengo fulani maishani lakini hawajui namna ya kufikia maana mazingira yao hayakuwafunza hayo. Ndiyo maana watoto wengi wanakata tama mapema na kuharibikiwa, hali ambayo inakuja kuwaumiza sana wazazi wao. Wakati huu wazazi hawajui kwamba mbegu hii ya uharibifu waliipanda wao.
4. Michezo ya kila wakati 
Wazazi tumetengeneza ulimwengu feki wa furaha kwa watoto wetu, watoto hawafurahii tena kuwa na watu bali kuwa na vitu vilivyowazunguka. Wanafurahia kucheza na vitu zaidi ya kucheza na watu. Utasikia mzazi anasema “yani mwanangu akilia ukimpa simu tu ananyamza kimya” halafu huyu mzazi anafikiri anayosema ni sifa. Maisha yetu wazazi yamekuwa na majukumu mengi katika hali ambayo tunajitahidi kuwapumbaza watoto wetu wadogo na michezo mbalimbali ili iwaduwaze wasahau kwamba wanamuhitaji mama au baba au mlezi mwingine. Unaingia kwenye nyumba ya mtu leo yani sebule haitoshi kwa jinsi kila sehemu kulivyojaa madoli na mamashine yamtoto kuchezea, unawaza anacheza na lipi na lipi analiacha? Sebuleni kumejaa hadi wageni wanakosa pakukanyaga kisa madoli ya mtoto. Nikuulize wewe mzazi, lini utamruhusu mtoto wako akusaidie kuosha vyombo? Lini utamwita nayeye afue hata kama ni nguo yake ya ndani? Lini utamwambia atoe vyombo alivyolia chakula mezani na sio kumtupia dada wakazi aoshe? Leo mtoto anamiaka 10 hajui kuosha kikombe au kufua nguo yake ya ndani. Ndio maana wengine wanapata shida sana kwenye mahusiano wakianza kuingia kwenye mapenzi maana hawajaandaliwa vyakutosha, unakuta kijana wa kiume mzembe kupita kiasi, anataka kuambiwa chakufanya badala ya kujituma, na binti wakike ndio kabisaa, kila kitu dada wakazi, mke anahitaji dada wakazi siku mbili baada ya harusi. Hii hali imeharibikia wapi? Jibu ni utotoni, wakati watoto hawa wakiwa na wazazi wao. Watoto watajitumaje au kujiongeza vipi wafanye kazi au wajibidishe wakati ubongo wao haujafundishwa hivyo? Ubongo wa mtoto unafundishwa kuwajibika na kujiwajibisha kwa kupitia kujifunza kazi sio wakati wote ni michezo tu.
5. Kupungua sana kwa muda wa kuwa pamoja
Muda wa watoto kuwa pamoja na wazazi au watu wengine umepungua kwa kiasi kikubwa. Nimesema hapo awali kwamba muda wa kuwepo pamoja kihisia baina ya wazazi na watoto ni kirutubisho kikubwa sana kwenye maendeleo ya ubongo wa mtoto. Nikasema tena kwamba kwasababu ya ubize wa wazazi, wengi wetu tumewapa watoto michezo na mashine za kuwasahaulisha uhitaji wao kwetu wazazi. Ule muda wa watoto kucheza na wenzao nje ya nyumbani haupo tena, watoto wanacheza ndani, na tena chini ya uangalizi, michezo imehamia kwenye televisheni na kwenye simu. Watoto hawakutani tena na marafiki zao na kucheza michezo ya watoto nje au viwanjani. Michezo na mikutano hii kuwasaidia watoto kuendeleza ujuzi wa kufahamiana kijamii “social skills”. Siku hizi watoto wa ndugu hawatembeleani tena hadi siku za sherehe au misiba, wengine wanasahauliana kabisa. Michezo ya kwenye televisheni na kwenye simu haijatengenezwa kukuza uwezo wa kutengeneza marafiki bali kinyume chake michezo hii yakielekrtoniki inaua kabisa ukaribu wa watoto wetu na watu wanaowazunguka. Tafiti zinasema moja ya tabia za watu waliofanikiwa duniani ni uwezo mkubwa wa kutengeneza na kudumu na marafiki “social skills”. Kitu ambacho kwa maisha wanayoishi watoto wetu watakikosa.
Kama nilivyokwisha sema awali kwamba ubongo ni mshipa unaoweza kupokea kitu au kuruhusu kitu kilichoingia kuondolewa. Unaweza kuufundisha kitu na kile kitu kisipoendelezwa basi kuondoka au hufa taratibu. Kama unataka mwanao afahamu kujituma basi mpe majukumu kwanza, unataka afahamu kuendesha baiskeli basi mpe baiskeli ajifunze. Kama unataka awe na uwezo wakusubiri basi mfundishe uvumilivu, unatamani awena tabia nzuri anapokuwa na watu basi mfundishe tabia za kijamii, nini anapaswa kuzingatia anapokuwa mbele ya watu, la sivyo kila siku mtoto anakuwa mzuri mkiwa nyumbani lakini mkitoka tu kidogo, anaharibu. Watoto wengi tunaona wanafungiwa kwenye magari au anarudishwa nyumbani kwasababu tu hawezi kukaa hata kidogo na watoto wengine. Fundisha ubongo wake kuwa bora angali mtoto ili awe vile unavyotamani awe.
Unaweza kabisa kusababisha utofauti kwa mtoto wako kwa kuufundisha ubongo wake kijamii, kihisia na hata kielimu. Haya hapa mambo muhimu ya kuzingatia
1. Punguza teknolojia kwenye maisha ya mtoto wako, kumbuka sijasema acha
kabisa. Punguza na badala yake ingia kwenye maisha yamtoto wako, zungumza naye, cheka naye, unganisheni hisia zenu. Muulize nini kinaendelea kwenye maisha yake ya nyumbani na shuleni, fahamu nani ni rafiki yake na nani ni adui yake. Fahamu nini anapenda na nini hapendi na kwanini? Chezeni pamoja, na kuwa na wakati pamoja nae au nao nje ya nyumbani.
2. Mfundishe/wafundishe kusubiri
Epukana na tabia ya kuwapa kila wanachohitaji kwa wakati uleule wanapohitaji kitu. Waruhusu kujifunza kusubiri. Kumwambia mtoto wako au watoto wako kwamba hawatopata wanachohitaji sasa hivi sio dhambi hata kama wanakiona kitu hicho wanachokihitaji. Kuvumilia na kuwa na subira ni kitu chamuhimu sana mtoto kuwanacho angali mdogo. Anataka kitu mwambie subiri kidogo. Nitakupa lakini sio sasa.Ninunulie kitufulani, mwabie sio wakati huu, haina haja ya kumdanganya kuwa sina hela, afahamu tu kwamba hela ipo ila sio kwa kitu hicho kwa sasa. Epukana kabisa na matumizi ya teknolojia mnapokuwa kwenye gari au mnapokuwa pekeyenu, eti kwasababu tu wamesema wanataka kuchezea hicho walichokitaka. La hasha.
3. Usihofie kuweka mipaka kwenye maisha ya watoto wako
Watoto wetu wanahitaji mipaka ili kukua katika mazingira ya afya njema ya mwili na akili. Watoto wasio na mipaka maishani sio watoto wazuri kabisa. Weka ratiba ya kula, kuwe na muda maalumu wa kulala na kuamka, baadaye watakuwa vijana, waanze kujua kuna muda maalumu wakurudi nyumbani, sio ukienda kucheza unakaa huko hadi muda unapoamua wewe. Watoto wafahamu kuna muda wa kuangalia televisheni na sio muda wote. Watoto wafahamu ninini wazazi wanapenda na ninini hawapendi. Fikiria na fanya kile ambacho ni chema kwa ajili ya leo na kesho yao sio tu kufanya kile kinachowafanya wafurahie. Kuna kufurahia leo na kusononeka kesho. Mzazi bora atataka furaha yao ya leo na hata kesho pia, hata kama maranyingine leo itaonekana kama sio furaha nzuri.