Mara nyingi wapendanao huwa na njia mbali mbali wanazozijua wao katika kukorofishana au kusuluhishana pale walipo korofishana. Labda njia au staili hizi wameamua na kudhamiria kuzitumia au yamkini zimejijia tu na kujikuta wanazitumia. Jinsi unavyotofautiana, au kugombana wewe na mpenzi wako yamkini ni tofauti na vile rafiki yako afanyavyo na mpenzi wake. Aina hizi hamjifunzi shuleni, hamfundishwi na wazazi wala maeneo ya ibada. Ni wewe kuzitilia mkazo na kuzielewa sasa.
Ingawa aina hizi za migongano zinatofautiana baina ya watu na watu na hazifanani, watafiti wa sayansi ya jamii wamejaribu kuziweka katika makundi matano yafuatayo:
1. Washindani (Competitors)
Watu wa aina hii mnapotofautiana kidogo hupayuka kwa sauti kama vile mko katika vita, wengine hulia kwa sauti. Kiu na lengo lao ni kushinda vita hiyo na kukunyamazisha wewe uliyetofautiana nao. Wao hujijali zaidi wenyewe na sio kumjali hata kidogo yule wa upande mwingine. Matakwa yao daima ndiyo yakuwekwa mbele na siyo ya mtu mwingine yeyote.
2. Waepukaji (Avoiders)
Mara nyingi mkitofautiana na watu wa jinsi hii na mkataka kukuzungumzia kile kitu kilichokuwa kwazo utasikia wakisema “sitaki tuliongelee hilo jambo” au “Usinikumbushe hayo”, au “ hayo yameshapita yanini tuyakumbushie tena”. Watu hawa huweza kuzuia vile wavipendavyo au kuvitamani na pia hawahusiki sana na matamanio ya wapenzi wao. Mfano; kama yeye hapendi maua au mitoko, hajali hata kama wewe unapenda maua au mitoko. Wakati ugomvi au kutofautiana kunapo zidi basi kusitisha kuzungumza na kuamua kukaa kimya kwa lolote lile hali ambayo huleta ugumu kwa mpenzi mwingine kwa kutojua nini mwenzake ana maanisha au anahitaji. Watu wa jinsi hii kuzira ndio wataalam. Magomvi ya staili hii hudhuru sana ukaribu (intimacy) baina ya wapendanao na ni hatari sana kwa sababu ni rahisi kuua au kuvunja ndoa, au mahusiano.
3. Walazimisha muafaka (Compromisers)
Hawa ni wale wanaolazimisha muafaka kwa kuweka mazingira yao binafsi. Hawa mara nyingi mnapotofautiana na mnataka kumaliza tofauti zenu waweza kusikia wakisema “mimi ntafanya hivi kama na wewe utafanya vile”, “Usipofanya hivi na mimi sifanyi vile” Wapendanao wa jinsi hii hujijali zaidi wao binafsi kuliko wanavyo wajali wenzao. Wale wanaouwezea mgongano wa staili hii huweza kupunguza kwa kiasi kikubwa tofauti zao lakini kwa kushusha kiwango cha mahitaji yao ili kila upande uweze kutosheka kidogo kidogo.
Mfano nimewahi kupata kesi ya wanandoa waliotofautiana sana juu ya suala la kumhudumia mtoto baada ya kurudi kazini, wote wamechoka na baba alikuwa analala sana usiku pasipo msaada wowote. Wakalazimika kukubaliana kwamba mara wakirudi, baba atashuhughulikia kila kitu kinachomhusu mtoto hadi muda wa kulala, na usiku wote, baba hatabugudhiwa, maana ni zamu ya mama, hapa vita ikapoa, na kwa aina hii ya suluhisho nikagundua kuwa watu hawa ni compromizers.
4. Washiriki (Collaborators)
Watu wa jinsi hii hutumia ile filosofia kwamba “kama huwezi kupigana nao basi jiunge nao” (if you can’t beat them join them). Hawa wanafanya tofauti na waepukaji (avoiders) Hawa hukimbilia makubaliano yenye kutafuta suluhisho, na mara nyingi katika kutafuta kutosheleza mahitaji ya pande zote mbili. Mara kwa mara hujiona na kujihisi wanaoweza nahii hujionyesha katika jinsi wanavyojali maslahi yao na ya wenzao. Malengo ya watu wa kundi hili sio ushindi katika tofauti zenu bali kuhakikisha kila mmoja anaridhika.
5. Wasaka amani (Accommodators)
Hawa ni wale watafutao amani kwa gharama yoyote, na hili ndilo lengo lao. Wanavutiwa sana na kuhakikisha amani inarudi, na katika kufanya hilo huweza kusamehe mahitaji yao, kuwaridhisha wanaowapenda.
Hawa ndio wale unaowasikia wakisema “kama hili gari ndilo linaleta tabu basi wewe lichukue tu ili mradi tuishi vema”. Staili hii ni kinyume na ile ya washindani (competitors). Watu wa kundi hili huingia katika migongano na wapenzi wao lakini mwisho wake kujitoa, hughairi ili tu kuitafuta amani. Huwa tayari kuyazika matakwa yao kwasababu tu ya furaha ya mwingine.
Ukiukuta ugomvi wa washindani utaishia:-
- Toka kwangu, acha kila kitu hapa, na kununulia, nakulisha, nakuvisha, nimekutoa mbali sana, kwanza jiangalie ulivyo sikuhizi, hukua hivyo wewe, nimekupendezesha sana tu.
- Nachukua kila kilicho changu hapa, mambo mengine utajua wewe mwenyewe.
- Tugawane sawa kwa sawa, kwanza wote tumetafuta hapa.
- Tutajua haki iko wapi hapa, na lazima mwenye haki ajulikane.
- Wako tayari kukata nusu picha mlizopiga pamoja ili tu mgawanyike, nakila mmoja aondoke na kipande chake.
Ukikuta ugomvi wa wasaka amani au accommodators
- We chukua kila unachokitaka tu mi niko sawa na hilo.
- We fanya kile unachokiona ni sawa mimi haitonisumbua sana.
- Wala usipate shida kutoka, mimi nitakupisha hapa.
Kila mmoja wetu anastahili yake aliyoizoea, ingawa maranyingine hubadilika kutoka moja kwenda nyingine. Tafiti zinaonyesha kuwa muunganiko wa makundi yaliyotajwa hapo juu (Collaborators, Compromisers, naAccommodators) huzaa mahusiano mazuri ambayo huweza kudumu kwa muda mrefu.
Ni dalili ya kuwa mtu mzima pale mnapotofautiana katika mambo ya msingi na sio kukwaruzana na kupigana kutwa kucha kwa vijimambo visivyo na tija. Kama kuna kitu cha muhimu na unachokiamini kimepingwa basi kipiganie na uachane na vijimambo vidogo vidogo. Wakati wote kumbuka kuwa hekima hupunguza wingi wa hasira. Najua kuwa wote tuna nishati nyingi tu miilini mwetu, tuzitumie nishati hizi katika yale yatakayokuza na kuujenga ukaribu wetu na siyo yale yatakayo ubomoa.