Tuesday, May 1, 2018
NAMNA YA KUONDOA MSONGO WA MAWAZO
Kwa mtazamo wa haraka haraka unaweza kufikiria kuwa hakuna njia ya kukabiliana na msongo wa mawazo kwa sababu hata iweje bili za umeme na maji zitazidi kuja, siku ndiyo ile ile ya saa 24 na kazi za kufanya zinazidi kuwa nyingi na majukumu ya familia yatazidi kuongezeka. Ukweli ni kwamba una uwezo wa kumudu kuukabili msongo wa mawazo kuliko unavyojifikiria. Kuelewa kuwa majukumu haya yote ni ya kwako na kuwa wewe ndiye mtu pekee wa kuyaweka sawa, ndio msingi wa kuanza kukabiliana na msongo wa mawazo. Kukabiliana na msongo wa mawazo kunataka uamuzi wa kuanza kuchukua hatua kimawazo, kihisia na kwa kujiwekea ratiba na hatua nyingine za kukabiliana na matatizo yako.
Kubaini Vyanzo Vya Msongo Wa Mawazo
Hatua ya kwanza kabisa ni kubaini vyanzo vya msongo wa mawazo katika maisha yako. Kazi hii siyo rahisi sana kwa sababu vyanzo hivi huwa sio vya wazi na ni rahisi kudharau mawazo, hisia na tabia ambavyo huwa ndiyo mwanzo wa kukupa msongo wa mawazo. Kwa mfano, unawezajua fika kuwa mara nyingi huwa upo katika wasiwasi mkubwa wa kukamilisha kazi ulizopangiwa katika muda uliopewa, lakini usijue kuwa tabia yako ya kuahirisha kazi ndiyo tatizo na si ukubwa wa kazi unazopewa.
Kubaini ni nini vyanzo vya msongo wa mawazo kwako, chunguza kwa ukaribu sana tabia, mwenendo na visingizio vyako. Kama hutokubali kuwa wewe mwenyewe ni mhusika katika kusababisha na kuvilea vitu vinavyokuletea msongo wa mawazo (Stressors), itakuwa vigumu sana kupamabana na tatizo lako la kuwa na msongo wa mawazo.
Andaa kijitabu kubaini ni nini kinakuletea msongo wa mawazo na vipi huwa unakabiliana na hali hiyo. Kila wakati utakapopatwa na msongo wa mawazo, fuatilia kwa kutumia kijitabu chako. Ukifanya hivyo kila siku, utajifunza ni mambo gani yanakusumbua na yanavyohusiana. Katika kijitabu chako andika yafuatayo:
Ni nini kilisababishia msongo wa mawazo
Nilijisikiaje, kimwili na kihisia
Ulifanya nini kilipotokea
Ni hatua gani ulichukua kurudi kwenye hali yako ya kawaida
Chunguza Namna Unavyokabili Msongo Wa Mawazo
Ni muhimu sana kujua jinsi unavyokabiliana na msongo wa mawazo. Kama uliandika vizuri kijitabu chako, kitakupa picha nzuri ya jinsi unavyokabiliana na msongo wa mawazo. Njia nyingine ni nzuri na nyingine ni mbaya na kwa bahati mbaya watu wengi hukabiliana na tatizo hili kwa kutumia njia ambazo huongeza tatizo na si kulipunguza.
Njia mbaya za kuondoa msongo wa mawazo
Hebu tazama njia ambazo baadhi ya watu hutumia, njia ambazo hupunguza tatizo kwa muda mfupi na kulifanya tatizo kuwa kubwa zaidi baadaye:
Kuvuta sigara
Kunywa pombe sana
Kula sana au kula kidogo
Kukaa kwenye TV au kompyuta, saa nyingi sana
Kujitenga na marafiki, familia na shughuli
Kutumia vidonge
Kulala sana
Kuahirisha mambo
Kujishughulisha saa zote kuepuka matatizo
Kuwatulia wengine msongo wao (kubwatuka, kufoka, kupigana)
Jifunze njia nzuri za kuondoa msongo wa mawazo
Sasa chukua nafasi hii kujifunza baadhi ya njia nzuri ambazo unaweza kuzitumia kukabilina na msongo wa mawazo. Kuna njia nyingine nyingi tu lakini zote zinakudai uanze kufanya mabadiliko kimatendo. Kwa sababu kila mmoja wetu yupo tofauti na atakichukulia tofauti kinapotokea kitu cha kusababisha msongo wa mawazo, hakuna namna moja tunayoweza kusema ufanye linapotokea jambo fulani, hivyo basi itabidi ufanya utafiti na kuona ni njia zipi zinaleta mabadiliko kwako. Zingatia kile unachokimudu na utakochoona kuwa kinachokusaidia.
Kimsingi kuna njia kuu mbili; kubadili mazingira ya chanzo cha msongo ambapo unaweza kukikwepa au kukibadilisha na pili kubadilisha jinsi hatua unazochukua ambapo unaweza kubalika ili uendane nacho au kukabaliana nacho. Tutazielezea njia hizo za kuukabili msongo wa mawazo hapa chini:
1. Kukwepa Vyanzo Vya Msongo Wa Mawazo:
Si rahisi kukwepa kila chanzo cha msongo wa mawazo na ni vibaya kukwepa chanzo cha msongo wa mawazo ambacho inabidi ukikabili. Ukiwa makini utashangaa kuona uwingi wa vyanzo vya msongo ambavyo unaweza kuvikwepa.
Jifunze kusema hapana: Tambua uwezo wako wa kimwili na kikazi na zingatia kufanya kazi kulingana na uwezo ulio nao. Kuchukua majukumu zaidi ya uwezo ni chanzo cha kujipa msongo wa mawazo.
Wakwepe watu wanaoklsababishia msongo: Kama kuna mtu anakusababishia msongo wa mawazo kila wakati, punguza muda wa kukutana naye au vunja kabisa mahusiano naye.
Dhibiti mazingira mabovu: Kama habari za jioni za kwenye TV zinakukera, zimisha hiyoTV na kama msongamano wa magari kwako ni kero, chukua njia nyingine isiyo na msongamano hata kama ni ndefu zaidi.
Kwepa mada zinazokupa maudhi: Kama mada za dini au siasa hukupa maudhi, acha kushiriki kwenye mada hizo. Kama kila siku unalumbana na watu fulani kuhusu mada fulani, acha kuanzisha mada hizo au tafuta kisingizio cha kuondoka mada hizo zinapoanzishwa.
Chunguza ratiba yako: Itazame kwa kina ratiba yako, majukumu yako na kazi ulizojipangia kwa siku. Kama mambo ni mengi mno, yagawanye kwenye makundi ya yale ambayo ni lazima yafanywe na yale ambayo ni muhimu kufanyika. Yale ambayo si ya lazima sana yaweke chini kabisa kwenye ratiba au yaondoe kabisa.
2. Badili Mazingira ya chanzo:
Kama inashindikana kukwepa chanzo cha msongo wa mawazo, badilisha mazingira yake. Jaribu kufikiria ni nini cha kufanya ili chanzo hicho kisijitokeze tena hapo baadaye, hii inamaanisha kubadili namna yako ya mawasiliano au namna unavyoendesha shughuli zako.
Onyesha hisia zako: Kama kuna kitu au mtu anakukera, mweleze wazi kabisa kwa njia ya kistaarabu. Kama husemi, unajenga chuki na kuiacha hali ikibaki pale pale.
Usilee matatizo: Usilikalie lile linalokukera, liseme wazi na chukua hatua mara moja ya kulizuia. Kama una kazi muhimu ya kufanya na rafiki yako mpenda hadithi anaingia, mwambie wazi kuwa una kazi muhimu na kwamba unampa dakika kadhaa tu za mazungumzo.
Tumia muda wako vizuri: Kushindwa kutumia muda wako vizuri ni chanzo kikubwa cha kupata msongo wa mawazo. Unapokuwa umechelewa kukamilisha jambo lako, utalifanya bila utulivu na utakosa umakini. Lakini ukiwa na mpango mzuri wa muda wako, utafanya kila kitu mbele yako kiufanisi na bila kupatwa na msongo wa mawazo.
3. Badilika Kuendana Na Chanzo:
Kama huwezi kukibadili chanzo cha msongo wa mawazo, wewe badili mtazamo wako kuhusu chanzo hicho:
Kitazame chanzo kwa mazuri yake: Kitazame chanzo cha kero kwako kwa kutazama mazuri ambayo yanaweza kupatikana kutokana na chanzo hicho. Badala ya kulalamika na kukasirika kutokana na foleni ya magari, chukulia kuwa huo ndio muda mwafaka kwako kujipumzika au kusikiliza muziki unaaoupenda ndani ya gari yako.
Kuwa na mtazamo wa jumla: Litazame jambo linalokukera kisha jiulize kama ni jambo litakalokusumbua kwa muda gani, mwezi mmoja, mwaka na jee mwisho wa siku ni madhara gani yatakayotokea. Kama ni suala la mpito tu, elekeza nguvu zako kwenye mambo mengine.
Rekebisha viwango vyako: Moja ya sababu ya kujipa msongo wa mawazo ni kutaka kila kitu kiende sawa kwa kiwango cha hali ya juu. Usijiweke kwenye mtego wa kushindwa kwa kujiwekea viwango vya juu kiufanisi. Jiwekee viwango vinavyowezekana kwako na kwa wenzako na jifunze kukubali matokeo ambayo hayakufika kiwango lakini siyo mabaya.
Yakumbuke mazuri yako: Msongo wa mawazo ukikunyemelea, chukua muda kidogo kushukuru kwa yale yaliyo mazuri katika maisha yako, ikiwa ni pamoja na vipawa nyako vizuri na vyenye nguvu. Hili litakusaidia kukupa mtazamo tofauti wa mambo yaliyo mbele yako.
4. Kubaliana Na Yale Ambayo Huwezi Kuyakabili:
Vyanzo vingine vya msongo wa mawazo huwezi kuvibadili wala kuvizuia. Huwezi kukizuia kifo cha mtu wa karibu yako, wala ugonjwa mkubwa, au mporomoko wa uchumi wa nchi. Hapa inafaa kukubaliana na hali ingawa ni vigumu, lakini ni bora kuchukua msimamo huo kuliko kugombana na kitu usichoweza kukibadili.
Usijaribu kudhibiti kisichowezekana: Vitu vingi sana katika maisha yetu vipo nje ya uwezo wetu – hasa tabia za watu wengine. Kuliko kung’anga’nia na kugombana nao wabadili tabia, fikiria zaidi namna unavyoweza kuepukana na matatizo yao.
Tazama upande wa pili: Unapokumbana na vikwazo vikubwa, chukulia kuwa ni nafasi ya kujifunza na kukomaa. Kama ni maamuzi yako mwenyewe ndiyo yaliyokusababishia matatizo, chukua nafasi hiyo kutafakari na kujifunza kwa maamuzi yako ya baadaye.
Jifunze kusamehe: Lazima ukubali kuwa tunaishi katika ulimwengu wenye mapungufu mengi na kwamba binadamu kufanya makosa ni kawaida. Usiwe na hasira na chuki, jifunze kusamehe na kuendelea na mambo mengine.
5. Pumzisha Na Burudisha Mwili Wako
Mwili wako utapata uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na msongo wa mawazo endapo utaulea kwa kupata muda wa kuupumzisha na kuuburudisha. Katika kuulea mwili wako unaweza kufanya yafuatayo:
Fanya matembezi
Pumzika kwenye bustani au sehemu zenye mazingira ya asili
Mkaribishe rafiki nyumbani
Pata kikombe cha chai au kahawa
Jishughulishe kwenye bustani
Soma kitabu kizuri
Sikiliza muziki
Angalia vichekesho
Cheza na mnyama uliyemfuga
Kuulea mwili ni jambo la lazima na si jambo la kujifurahisha tu. Katika kuyafanya hayo, jipangie kabisa ratiba yako na usimruhusu mtu au vitu vingine kuvuruga ratiba yako, huu ni muda wako wa kuurudishia nguvu mwili wako. Jichanganye na marafiki wenye mawazo mazuri, hao watakusaidia kuondokana na madhara yanayotokana na kuwa na msongo wa mawazo. Jaribu kuwa ni mtu wa kufurahisha na kufurahia mambo kwani kicheko ni dawa ya kuondoa msongo wa mawazo kwa njia nyingi.
6. Mazoezi Na Chakula Kizuri
Unaweza kuongeza uwezo wako wa kukabiliana na msongo wa mawazo kwa kujenga afya ya mwili wako.
Fanya mazoezi
Kula chakula kizuri
Punguza matumizi ya kahawa na sukari
Acha sigara, pombe na madawa
Pata usingizi wa kutosha