Wednesday, November 22, 2017
Sababu 3 muhimu, Kwanini hupaswi kufanya ngono siku ya Valentine
Siku hii imekuwa ikichukuliwa na idadi kubwa ya watu kama siku maalum ya watu kuwa na wapenzi wao karibu iwe ni wana ndoa, wachumba au hata watu wanaoanza kuwa na uhusiano wa mapeni au wenye uhusiano wa mapenzi usio na tafsiri ya moja kwa moja… wamejikuta tu ni wapenzi na hawana dira maalum.
Naamini kama kuna utafiti wa takwimu utaweza kufanyika leo, itagundulika kuwa leo ndio siku ambayo idadi kubwa zaidi ya watu watakuwa wameshiriki tendo la ndoa.
Wengi kati ya hao huhakikisha siku ya leo haipiti bila kufanya mapenzi. Kwa sababu wanaamini ni siku teule, ya pekee na bora zaidi ya kutoliacha tunda liende bila kuligusa! Fikra hizi ni potofu. Hii sio siku nzuri zaidi ya kufanya mapenzi, uzinzi au uasherati na ni siku hatari zaidi!
Sitaki kuzungumzia usaliti, ugomvi na kuvunjika kwa mapenzi baada ya siku hii.. nitakupitisha kwenye sababu maalum ambazo zitakufanya uone namna ambavyo hii sio siku bora zaidi ya kufanya mapenzi.
Lakini kabla sijaanza kukueleza, ningependa ufahamu kuwa hata neno Valentine lenyewe halina maana ya mapenzi, limetokana na neno ‘Valens’ ambayo maana yake ni ustahili/thamani, nguvu au Mamlaka.
Nitakujuza maana ya sikukuu ya Valentine na chimbuko lake mwishoni.
Hizi ni sababu tatu za kwanini sio siku nzuri ya kufanya mapenzi:
1. Ni siku Hatari Zaidi
Hii ni siku hatari zaidi ya kufanya mapenzi. Hatari hii huanzia kwa wanandoa ambao wamekuwa wakitumia ratiba nzuri ya kupanga uzazi ambayo huenda ikavurugwa na ratiba ya Valentine. Na kwasababu wanakuwa hawajazoea kutumia kinga, ni siku ambayo wana uwezekano mkubwa wa kushiriki ili kujiunga na kundi la wanaosherehekea siku hii na badala yake wakajikuta wanapeana mimba zilizo nje ya mpango.
Hatari nyingine kwa wapenzi inatokana na namna ambavyo wengi huisherehekea kwa kutumia vilevi mbalimbali wakiwa na wapenzi wao. Hivyo, hujikuta wakiishia katika kufanya ngono ambazo kwa asilimia kubwa zinakuwa sio ngono salama.
Kadhalika, hii ni siku ambayo wapenzi wengi hujikuta wakibakana. Mmoja kati ya wapenzi hao anaweza akawa hayuko kabisa katika ‘mood’ za kushiriki tendo. Lakini kwa kuwa mmoja wao yeye anataka kujiunga na kundi la wanaosherehekea, hujikuta akilazimisha hadi apate tunda kujisikia anasherehekea.
2. Mapenzi sio Mkumbo
Utakubaliana na mimi kuwa watu wengi wameamua kuifuatisha siku hii na kuinganisha na masuala ya ngono kwa kufuata mkumbo tu. Wengi watafanya ngono ili wajiunga na kundi la watu wengine ambao wanaamini leo ni siku yao.
Unapaswa kufahamu kuwa kufanya ngono kwa kufuata mkumbo ni ‘ushamba’ na kujipotosha. Hata kama sio sikukuu ya chochote duniani.
Ili penzi lako lidumu, unapaswa kuwa wa pekee na uache kukimbia mbio za ‘manyumbu’. Samahani kama nimekukwaza kwa lugha hiyo, lakini nilitaka kukwambia kuwa unapaswa kukimbia ‘mbio zako mwenyewe’ (Run your own race). Ufanye uhusiano wako kuwa wa pekee, na upekee huo uonekane kwa mwenzi wako. Usimuoneshe ukurupukaji, mapenzi ni maridhiano na utaratibu. Usifanye kitu kwa sababu fulani kafanya au wengi wanafanya.
3. Valentine’s Day sio sherehe ya Ngono
Ni kosa kubwa, na kama wewe ni mtu unayeamini katika dini yoyote inayomuamini Mungu, nakushauri kabisa ufahamu kuwa ni dhambi kubwa sana kuihusisha sikukuu ya Valentine na ‘ngono’. Sipaswi kukuhukumu kwani mimi sio mkamilifu ila naamini ntapata baraka kukuonya usitumbukie huko.
Ngono au mapenzi ya kuitafuta ngono sio mpango wala nia ya siku hii. Bali ni mpango wa shetani kuitumia sherehe hii kuvua wafuasi wengi zaidi kupitia ngono, uzinzi na uasherati. Hakika leo atavuna wengi zaidi ya siku zote.
Usiwe sehemu ya wanaosherehekea ngono. Ni vyema ukawapinga kwa kutofanya ngono hata kama una uhalali. Weka mgomo kupinga na kutoingia kwenye rekodi hii chafu.
Ngoja nikupe kwa ufupi chimbuko na nia njema ya siku kuu ya ‘Valentine’s Day’;
Hii ni siku Takatifu. Inakumbukwa kusherehekea matendo mema aliyoyafanya Mtakatifu Valentine wa Rome, mtumishi wa Mungu alifungwa jela kwa kosa la kukiuka amri ya watawala na kufungisha ndoa kwa siri wanajeshi na kuhubiri injili. Wakati huo, wanajeshi walikuwa hawaruhusiwi kufunga ndoa ili washiriki vyema kwenye shughuli za ulinzi wa Taifa lao ikiwa ni pamoja kujikita katika vita bila kuwaza familia.
Kwa kuwa Mtakatifu Valentine aliiona ndoa kama Sakramenti muhimu ya dini ya Kikristo, aliamua kuwafungisha ndoa kwa siri. Hata hivyo, alikamatwa na kufungwa jela akisubiri hukumu ya kifo.
Wakati Valentine alipokuwa gerezani, aliweza kumponya mtoto wa kike wa askari Magereza aliyefahamika kwa jina la Asterius. Alimpenda sana kwa mapenzi ya ‘Agape’ na sio ‘Romance Love’.
Kabla ya kuuawa, alimuandikia mtoto huyo barua ambayo mwishoni alimaliza kwa kusema ‘Your Valentine’ (Valentine Wako).
Dini za Magharibi ziliichukua siku hiyo na kufanya kuwa siku ya ‘Wapendanao’ kwa mapenzi ya Agape, yaani mapenzi ya baba na mama, marafiki na hata wanandoa.
Kwa bahati mbaya, siku hii imeguzwa kichwa chini miguu juu na kizazi hiki kipya ambacho naamini hiki kizazi chetu huenda sio kile ambacho Yesu alikiita ‘Kizazi cha Nyoka’. Hivi sasa Valentine ni siku ya mapenzi ya Romance.
Kwa usahihi, itakuwa baraka endapo utaitumia siku hii kupiga hatua katika uhusiano wako, mvishe mwenzio pete ya uchumba sio kwa kufuata mkumbo bali kwa kumaanisha ili uwe na kumbukumbu sahihi. Mnunulie mama/baba yake mpendwa au mtu umpendaye yeyote zawadi na kadhalika.
Shtuka, achana na hisia za ngono kwenye sherehe Takatifu,