Tuesday, November 21, 2017

Nimembebea Mimba Mpenzi Wangu Amegoma Kunioa Kamchukua Rafiki Yangu

Mimi ni binti wa miaka 22, sifanyi kazi yoyote na nipo tu nyumbani. Tatizo langu ni huyu mpenzi wangu, tumekuwa naye kwenye uhusiano kwa miaka miwili na na mpenda sana ingawa mwenzangu kabadilika yaani hata sijui nianzie wapi, kila nikiwaza nachanganyikiwa kabisa.
Yeye ni mtu mzima kidogo kuliko mimi ana miaka 30, anafanya kazi na ana kipato kizuri tu. Mwanzoni alikuwa akinipenda na kunihudumia kwa kila kitu, kwakuwa alikua tayari ameshajitambulisha kwa wazazi wangu basi tulikuwa huru sana na mara nyingi nilikuwa nikienda kulala kwake na kusema kweli tulikuwa tukiishi kama mke na mume.

Lakini mwaka jana alibadilika sana, akawa hanijali tena kama awali na nikawa nikienda kwake anakasirika sana au anatafuta sababu za kuniambia niondoke kwakuwa ana mambo mengi au wageni ambao hataki nionane nao. Basi niliamua kuvumilia lakini nikichunguza sababu za yeye kubadilika, huwezi amini niligundua anatembe na rafiki yangu mkubwa ambaye tulikuwa kama mapacha tukielezeana kila kitu.
Nililia nusu kuchanganyikiwa, nilipomuuliza alikiri na kunijibu maneno ya kashfa. Lakini kwakuwa nilimpenda nilimsamehe ingawa hata hakuomba msamaha. Ili kulilinda penzi letu niliamua kumtegeshea mimba kwani nilijua anahitaji sana mtoto mara nyingi huongea hivyo na kweli alipojua kuwa mimi ni mjamzito alibadilika na kurudia kwangu, alikuja kwetu kutoa mahari na mimi nikahamia kwake moja kwa moja wakati tukijipanga kufunga ndoa.

Samahani kwa maelezo mengi lakini sijui namna ya kufupisha. Baada ya kuendelea kuishi kwake hakuendelea na maandalizi ya harusi wala nini aliishia kutoa tu mahari na kukaa kimya, nikimuuliza anasema ngoja kwanza afanye maandalizi ya mtoto kwakuwa mtoto anahitaji gharama kubwa na harusi nayo inahitaji gharama kubwa, nikishajifungua ndipo tutafunga ndoa. Nilimuelewa kwakuwa alionekana siriasi na alishaniahidi kuwa kaachana na yule rafiki yangu.

Lakini kumbe nilikuwa najidanganya, wiki iliyopita nilifumania meseji anachat na rafiki yangu, kumbe yule rafiki yangu baada ya kuona kuwa mimi ni mjamzito nayeye bila aibu alibeba mimba, mimi nina mimba ya miezi mitano yeye ana mimba ya miezi miwili. Nililia sana nusu kuchanganyikiwa, sikutaka kumuambia lakini kwa hali niliyokuwa nayo alijua kuwa nimejua na hapo ndipo ugomvi ulipoanzia.
Hatukuwa tukizungumzia tena kuhusu mimba ya rafiki yangu bali kuhusu mimi kuchungulia simu yake. Alikasirika sana na kuanza kunipiga, alitoa vitu vyangu nnje na kunifukuza akisema hawezi kuishi na mwanamke kama mimi ambaye siheshimu vitu vyake. Kama utani nilifukuzwa na kuamua kurudi nyumbani na ndani ya siku mbili tu yule rafiki yangu alihamia kwake na walianza kutangaza kuwa wanaoana.
Nimeumia sana yaani sijui hata chakufanya, nyumbani kwetu hali duni naishi na Mama na wadogo zangu ambao wote hawana kazi ya kufanya. Sijui nini kilinikuta nilijikuta nawaza kuitoa hii mimba mbayo sasa ina zaidi ya miezi mitano kuelekea sita. Watu wananiambia nitakufa lakini sina namna sina hata pesa, mwanaume simu hapokei na nikienda kwake namkuta yule rafiki yangu ambaye hunitukana na kuniambia kiko wapi nilikuwa naringa yeye amemuwekwa ndani na simtoi.
Naona kama yule mwanaume si akili yake kalishwa dawa kwani mimi ni mzuri zaidi na alikuwa akinipenda mimi, naomba ushauri wako kwani nikisoma post zako unaonekana kama mtu muelewa unayeweza kunisaidia. Nataka nitoe miamba klakini sijui kama itatoka Mama anataka kunipeleka kwa mganga wa kienyeji ili yule mwanaume arudi kwangu, sijui nifanye nini. Nisaidie nipe uelekeo sijui hata pakwenda, sina kazi sina chochote.

JIBU LA MAHUSIANO LIVE;

Kwanza pole sana na yaliyokukuta natamani kutiririka sana hapa lakini kutokana na hali yako na ulipofikia sitaki kufanya hivyo. Nikuambie tu hali uliyonayo inawakumba wasichana wengi, ambao hudhani kwa kubeba mimba au kumzalia mwanaume ndiyo kuweza kumshika, ndiyo tiketi ya kuelekea kwenye ndoa. Ukweli nikuwa mwanamme anayekupenda hahitaji mimba ili kukuoa au kuwa na wewe.
Najua kwa hali uliyonayo unapitia machungu mengi lakini huu si muda wa wewe kupaniki. Kwanza nianze na suala la kutoa mimba, hakuna dhambi mbaya kama hiyo, ingawa wasichana wengi huona kitu rahisi lakini usijaribu, tena kwako hali ni mbaya zaidi kwani mimba ni kubwa, miezi mitano hiyo mtoto ashakuwa mkubwa unaweza kutoa mimba na wewe ukafa.
Nimesisimkwa kuona unaweza kufanya kitu kama hicho, hata kukiwaza tu, naomba pepo hilo baya likutoke. Kila mtoto huja na baraka zake na wala usiwaze kuhusu namna ya kumlea. Miezi mitano ni mimba kubwa sana nikama unaua mtoto mkubwa, nakushauri usifanye

Kuna mamilioni ya watu wanahitaji watoto huna haja ya kuingia kwenye dhambi hiyo. Kuhusu kwenda kwa mganga achana na mawazo hayo, huyo mwanaume hajalogwa wala nini? Hakupendi na acha kujishusha kiasi hicho. Umrembo sana nina hakika utajifungua salama mtoto mzuri acha kujidhalilisha kwa mwanaume ambaye hakujali.

Hata ukimloga mara mia mbili hawezi kuwa wako kama hakupendi hakupendi tu atakuja kwako kwa muda atakuzalisha tena na kukuacha. Shukuru Mungu kakuonyesha sura yake mapema kabla ya kuingia kwenye ndoa. Kuwa single mother ni kitu cha kawaida kabisa, huna haja ya kuumiza kichwa. Pole sana yameshatokea, jua tu mwanaume hashikwi kwa mimba, kama kakupenda kakupenda tu hatajali kama una mimba au hata unauwezo wa kuzaa atakuoa tu na kuwa na wewe.

Kwa bahati mbaya sana mabinti wengi huingia katika mtego huu wa kulazimisha mimba ili kupata tiketi ya kuolewa. Nikweli anaweza kukuoa lakini asiwe Mume wako, Mume ni zaidi ya kukubaliana kanisani na msikitini kuwa mnaoana. Anaweza kukuoa ukawa umeingia kwenye ndoa ya mateso na halitakuwa kosa lake kwani moyo wake haukuwa kwako tangu awali.