Mimi ni binti wa miaka 27 sijaolewa na nafanya kazi. Nilikuwa na mpenzi wangu ambaye tulikaa muda mrefu kwenye mahusiano tangu tukiwa chuoni na baada ya kumaliza chuo wote tulipata kazi Kusema kweli tulikua tunapendana sana kiasi kwamba kila kitu tulikuwa tukifanya pamoja.
Ingawa hatukuwa tukiishi pamoja kwakuwa tulikuwa mikoa tofauti kutokana na ajira lakini mambo yetu tulianza kufanya pamoja na tulijiwekea malengo mengi. Sasa mwenzangu kuna kiwanja alikinunua Dar anakoishi, mimi naishi Morogoro na wakati tukijipanga kufunga ndoa mwaka jana tukaamua kuanza ujenzi.
Mimi nilichukua mkopo kazini kwani niko serikalini na yeye binafsi kazi ya mkataba hivyo hawezi kuchukua mkopo, tukaanza kujenga harakaharaka, ili tukioana tusiishi nyumba za kupanga. Nyumba imemalizika na imebaki vitu vidogo vidogo tu, mwezi uliopita nilienda Dar kikazi, kilikuwa kitu cha ghafla tu safari ambayo sikupanga.
Nilitaka kumpigia simu kuwa nakuja lakini alikuwa hapatikani hivyo nikaamu kwenda tu kwakua hata funguo za kwake ninazo. Huwezi amini nilifika na kumkuta na mwanamke mwingine. Alikasirika eti kwanini naenda kwake bila taarifa na alinipiga, nilitegemea kama atamfukuza yule mwanamke lakini alikataa na kunifukuza mimi akisema niende gesti, kweli nilienda.
Niliumia sana na nilitegema hata angeomba msamaha lakini wapi, kumbe yule mwanamke na yeye walianzana muda mrefu na yeye hata katika ujenzi alishiriki. Kwamba kumbe ile nyumba tulijenga watatu ingawa mimi ndiyo nilichangia sana. bado nampenda lakini ameshamchagua yule kwani anasemaa napatana sana na ndugu zake tofauti na mimi.
Alishanitambulisha kwa baadhi ya ndugu zake lakini hatuko karibu kihivyo si kwamba tumegombana ila yule inaonekana kampeleka mpaka kwa Mama yake. Sitaki mnishauri kuhusu kumrudia bali naomba ushauri ni namna gani nitapata haki yangu, kwani kiwanja kanunua kwa jina lake, mkopo bado nakatwa nilichukua wa miaka mitano na kuachwa nimeachwa nisaidieni mawazo yenu.
Hakuna ushahidi wowote kuwa nilitoa chochote kwani nilikuwa namtumia tu pesa, mbaya zaidi nasikia anafuatilia hati ya kile kiwanja kwa jina lake tu kwani kilikuwa hakina hati. Nikimpigia hapokei simu zangu na alishaniambia hataki tujuane, suala la nyumba ndiyo hataki kuliongelea kabisa, nipo njia panda naomba mnisaidie mawazo nini cha kufanya?