Monday, July 9, 2018

UNAJUA LUGHA NZURI YA KIMAPENZI???



Hakuna linalouma moyo kama mtu kuachana na aliyempenda. Moyo husafiri kilometa nyingi kwa kuwaza. Hakukosea aliyesema sikitiko la mahaba linashinda msiba. Lakini yote hayo yanaweza kuepukika na kukaa mstari ulionyooka endapo mawasiliano yatabeba umuhimu unaotosheleza na kusimama kwenye nguzo zake kuu.
MAWASILIANO: Ni nguzo kuu ya uhusiano. Ikiimarishwa huchochea amani ya kudumu lakini kinyume chake ni kichocheo cha wapenzi kuachana. Ni vizuri kujifunza lugha inayoweza kukufanya uelewane na mwenzako. Sauti yako ukiwa mtaani itofautiane na ile ambayo unaitumia chumbani.
Pengine una kawaida ya kutoa majibu ya mkato unapokuwa unazungumza na rafiki zako, lakini tabia hiyo hutakiwi kuizoea pale unapokuwa na mwenzio chumbani. Ikiwa umezoea kuwaita wenzako: “Wewe!” Mwenzi wako hutakiwi kumwita hivyo.
Ni elimu ambayo kila mtu anatakiwa kuwa nayo kwamba kutofautisha maeneo ni jambo la busara. Kwamba sura yako iwe nyingine unapokutana na watu wa mitaani, itofautiane unapokuwa na wazazi, vivyo hivyo pale ambapo upo sehemu ‘spesho’ na mwenzi wako.
Lazima uwe unabadilika kama kinyonga. Ukiwa kazini mbele ya watu unaowaongoza unazungumza kwa sauti ya amri, lakini hiyo hupaswi kuitumia unapokuwa na wazazi wako. Unaongea kwa sauti kali ya kuamrisha mbele ya baba yako, hiyo adabu umefundishwa wapi?
Kuna lugha ya kuzungumza ukiwa na mwenzi wako. Ni mwiko kutoa sauti ya kuamrisha. Ni vizuri kumnyenyekea lakini si katika kiwango ambacho kitakufanya uonekane una kasoro za kisaikolojia. Tawile kwa kila linalosemwa na mpenzi wako hairuhusiwi, unatakiwa kuweka mbele hisia zako.
Upole kupitiliza hauna maana kwamba wewe ni mpenzi sahihi. Eti, utaonekana una nidhamu na unamsikiliza vizuri mwenzio, la hasha! Utatambulika kuwa mtu hai kulingana na jinsi akili yako inavyofanya kazi. Namna hisia zako zinavyoonesha uhai unapoguswa na matukio mbalimbali ndivyo na ubinadamu wako unavyosomeka.
Unahoji mambo kwa sauti yenye ujazo wa kutosha, unachukia pale unapoona mambo hayajaenda sawa, unaumia pale unapotendwa na unafurahi mipango inapokuwa chanya. Hii ndiyo mantiki ya kukutaka uwe na akili hai. Itashangaza umepata habari kwamba mwenzi wako yupo gesti na mpenzi mwingine halafu utabasamu.
Sumu hatari inayosababisha mmomonyoko wa ndoa au uhusiano wa kimapenzi kwa watu wengi ni kushindwa kujipanga kimaeneo. Ratiba za ofisini kuingiza nyumbani. Marafiki kuathiri taratibu za mapenzi yenu, ingawa kila kitu kina umuhimu wake kulingana na wakati husika.
Umeudhiwa na wafanyakazi wenzako kazini, unatakiwa kuweka hekima mbele. Unarudi nyumbani ukiwa na imani kwamba huko utakutana na mwenzi wako na ndiye mfariji wako. Kichwa kizito, basi mueleze mwenzio ajue kinachokusibu kuliko kumpa majibu ya mkato. Itakuharibia badala ya kukusaidia
Ninachosisitiza hapa ni kuwa uhusiano wa aina yoyote unadumishwa na mawasiliano.
Lugha yako mbele ya mwenzi wako ina nafasi kubwa ya kukufanya uendelee kufurahia penzi lake. Kinyume chake unaweza kujikuta ni kero kwake. Atakuvumilia mwisho atachoka kwa sababu hujui kubembeleza, unapenda kuamrisha.
Unataka kuwa mtu bora kwenye uhusiano? Zingatia chachandu zifuatazo:

TAMBUA MAKOSA YAKO
Hii ni lugha nzuri mno kwenye mapenzi. Unatakiwa kutambua makosa yako haraka na kutafuta njia ya kusuluhisha. Ukijielewa kwamba umekosea halafu ukakaa kimya hutoa ishara mbaya mbele ya safari.

KUWA MWEPESI KUSEMA SAMAHANI
Kiingereza kinatawala sehemu kubwa ya mawasiliano ya Watanzania, kwahiyo ukiona samahani utaonekana upo kienyeji, basi sema I am sorry. Hii ni baada ya kutambua makosa na unapoomba msamaha umaanishe kutoka moyoni.

USINUNE AKINUNA
Ni lugha ya mapenzi kwamba mwenzako akinuna, wewe jishushe ili mpate muafaka. Nyote mkigoma mtafika saa ngapi? Ni kosa kubwa unapobaini mwenzi wako ana hasira, nawe ukapandisha jazba kwani ni kiashiria cha kuachana.

CHUKIA ASIYOYAPENDA
Inafundishwa kwamba rafiki wa rafiki yako ni rafiki yako. Adui wa rafiki yako ni adui yako. Rafiki wa adui yako ni adui yako. Adui wa adui yako ni rafiki yako. Falsafa hii ikupe somo kwamba hutakiwi kupenda yale ambayo anayachukia.
Haikubali mtu ambaye hana jema kwa mwenzi wako, wewe umfanye rafiki. Fikiria upande wako kwamba kuna mtu anakula yamini kukumaliza, halafu ugundue kwamba mpenzi wako huwa anaketi naye na kuzungumza kwa kugongeshana mikono? Heshimu hisia za mwenzako.

ONGEZA MAPENZI KWA ANAYOPENDA
Mapenzi ni sanaa, ukiweza kucheza karata zako mtadumu bila kuchokana. Umeweza kuchukia yale ambayo hayapendi, sasa ni vizuri kuongeza mapenzi kwa yale ambayo anayapenda. Hii itasaidia kuwafanya muonekane ni kitu kimoja daima.
Hata hivyo, iga kwa mambo mazuri, isije ikawa mwenzako ni mtu wa baa kwa sana halafu na wewe umuige. Anapenda siasa, mpe ushirikiano nawe uipende taratibu. Mpira nenda mkaangalie pamoja, muvi na mengineyo, hayo ndiyo mapenzi.

MFANYE AKUTAMANI MUDA WOTE
Ni rahisi, unapokuwa naye muoneshe mapenzi ya dhati. Hakikisha hakasiriki mkiwa pamoja, yanayomhusu unabeba kama yako. Humkaripii na unamfanya yeye ni bora. Msifie kwamba ni mzuri na umueleze kwa hisia jinsi unavyomkubali. Hiyo itamfanya ajenge imani kubwa kwako na ukiwa mbali atajiona pungufu.

USITHUBUTU KUPAYUKA
Hata kama mmegombana, linda sauti yako. Tumia hekima na myamalize kimyakimya.

SWEETHEART, DARLING, BABY, HONEY, DEAR
Mpe heshima yake na umuoneshe ni kwa kiasi gani alivyo na nafasi kubwa kwako. Usipende kumuita kwa kumtaja jina lake au wengine wakishapata mtoto ndiyo utasikia “Mama Chausiku!” au “Baba Semeni!”
Haifai, tumia majina hayo au ukiweza tumia mengine yenye mvuto. Ikupe raha kutamka na yeye imfanye afurahi kusikia kutoka kwako. Mapenzi ni rahisi, utundu kidogo utakufanya uone dunia yote unaimiliki wewe.