Monday, April 23, 2018

Ufanye nini unapovutiwa kimapenzi na mtu mwingine

Wapo watu ambao wameoa au wana wapenzi walioahidiana kwa mambo mengi, lakini wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kuvutwa kimahaba na watu wengine. Hali hii huwatokea wawapo masomoni, kazini, kwenye biashara, mbali au pengine hata karibu na wenza wao wa zamani.

Sayansi ya jamii inakubali kuwa mwingiliano wa kijamii mara nyingine huathiri tabia za watu, ukweli huu unathibitishwa na ongezeko la usaliti katika mapenzi, mantiki ikibaki kwenye mwili kulazimishwa na mapokeo ya tafsiri ya vitu vinayotawala mawazo ya mwanadamu.

Katika mapenzi kuna mashujaa wachache sana ambao wanamudu ushawihi wa kimahaba kutoka kwa wengine, hii ina maana asilimia 96.5 kwa mujibu wa uchunguzi huanguka kwenye mapenzi mapya baada ya miili kuelemewa na hisia chochezi.

Maelfu ya wanaume na wanawake hulazimika kuwasaliti wapenzi wao baada ya kuvutiwa na maumbo au sura za wanaume/wanawake wanaokutana nao katika shughuli zao za kimaisha. Wapenzi hao hujikwaa kupitia macho na hisia zao, huku wengi wakikiri kushindwa kuzuia matamanio.


“Msichana/mvulana huyu ni mzuri sana nahisi kumpenda, nimuonapo nachanganyiwa kabisa.” Inawezekana hata wewe unayesoma makala haya umewahi kutamka maneno haya na ukasahau kuwa umeoa/ umeolewa au una mchumba uliyepanga kufunga naye ndoa. 

Kama hilo halitoshi yawezekana umeshakuza mawazo hayo kiasi cha kuona huna jinsi zaidi ya kufanya usaliti, ukatongoza au ukajitongozesha kwa gharama ili utii hisia zako.

Ninapotazama mwenendo wa wapenzi wengi siku hizi, nabaini kuwa mihemko ya miili inawaangusha wengi kwenye usaliti, jambo linalonifanya nilazimike kufundisha namna ya kukabiliana na tatizo hili ili kuweza kuyanusuru mapenzi .

Naliita jambo hili tatizo kwa sababu limeleta madhara mengi katika jamii, kuna watu wameshauana, ndoa kusambaratika na mapenzi kufa, isitoshe uchunguzi unaonyesha kwamba, wasaliti wengi hawakupata faida au raha waliyoitarajia kutoka kwa wale waliowashawashi, hivyo kufanya hisia zao ziwe kazi bure.

Naamini hakuna mwenye akili timamu anayependa kupoteza utu wake bila faida. Ndiyo maana ipo orodha ndefu ya watu walionifuata na kukiri: “Alinirubuni nikamwacha mpenzi wangu, kumbe alitaka kunichezea tu.” 

Wanakiri kurubuniwa, lakini wanasahau kuwa walikubali baada ya kuvutwa na hisia! Je mpaka sasa ni wanaume wangapi wanavutwa kimahaba na akidada warembo wanaokutana nao kiasi cha kuwapuuza wapenzi wao wa zamani na kuamua kuwasaliti? 

Katika matembezi yao, shughuli zao, ni wasichana wangapi wanachanganywa na muonekano wa wavulana wanaofanya nao kazi. Angalia mwenendo wako utabaini umekuwa kwenye mtego huu mara ngapi.

Je umeshawahi kujiuliza: HUYO UNAYEVUTIWA NAYE ATAKUCHUKULIAJE? Unachofikiri ndicho anachofikiri yeye au unajipendekeza? Jaribu kuwaza kama unajipendekeza hatma yake itakuwaje kama si kupoteza utu wako bure.

Jiulize tena, UTAPATA NINI KWAKE. Watu makini hujiuliza faida watakazopata katika matendo yao na hivyo kuwa na maamuzi sahihi. Kukurupuka kufanya jambo bila kutazama faida na hasara zake ni wendawazimu. Swali jingine, UNAYEMBABAIKIA ATAPATA NINI KWAKO, Je asipopata cha maana ataamuaje? 

Baada ya kujiuliza hivyo, malizia kwa kujiuliza UKO SAHIHI? Kitalaamu ukitoa nafasi ya mawazo yako kuhakiki mienendo yako, utajikuta mwili wako haukulazimishi sana kutimiza matakwa yake, lakini ukiwa mtu mwenye kuona na kulea hisia, utajikuta siku moja unafanya jambo baya litakalokuumiza maisha yako yote.

Waendekezao hisia za mvuto ndiyo hao wanaodiliki kufanya mapenzi hata na baba, mama, kaka na dada zao.