Monday, March 26, 2018

Umeshamboa na kumuuzi Mpenzi wako, Tumia Njia Nzuri ya Kumuomba Msamaha.

"Hakuna kitu hawa watu wa jinsia tofauti wanachokijua kama kununa, na kama upo kwenye uhusiano wa kimapenzi lazima siku ifike mwenzio anapokataa kuongea nawe, inawezekana kosa likawa dogo au kubwa, hata kama hujui ni nini kimesababisha hawa viumbe ndivyo walivyoumbwa, kwao lazima kuna kitu utakosea tu, uwe umemtukana bibi yake au hujamsalimia mama yake lazima tatizo litakukumba tu ."
Jopo la Kiumeni.com baada ya kukaa na kufanya utafiti wa kina kwa marefu na mapana limekuandalia njia sita ambazo zitakufanya haya matatizo yasikuumize na kukusumbua sana moyo, njia hizi mbadala zitahitaji juhudi zaidi kutoka kwako na pia itakubidi uwe mbunifu kidogo na saa nyingine itakubidi umeze mate, uvute pumzi na kujifunga kiuwanaume na kitanashati na kukubali ya kuwa umekosea.

          #1; Tengeneza hali ya kimaongezi.

Utajua amekununia ikiwa kila ukimsemesha hataki kuongea nawe na kamwe huwezi kuyamaliza matatizo mpaka pale atakapoanza kuongea nawe na kukitoa kile kinachomuumiza moyo, kwa hiyo tengeneza hali ya kimaongezi ili aweze kukiongelea kile kinachomsibu mpaka kuwa hivyo na kukununia, using'ang'anize neno kwa kumuuliza mfululizo ni tatizo gani linalomsibu, kurudia rudia swali ni kusababisha makubwa zaidi.

Kama hujui kweli chochote kinachomfanya awe hivyo, jaribu kupatishia hata kama ukipatishia ambacho sio itasaidia maana utakua umetengeneza hali ya kimaongezi itakayofanya nyie wawili muweze kuongea tena.


          #2; Mfanye acheke na kutabasamu.

Ukiwa na uwezo wa kumchekesha ni kipaji kizuri kitakachoweza kukufikisha mbali na wanawake, japo sio kila muda kumfanya arudishe tabasamu kunawezekana, saa nyingine kunaweza kukufanya uonekane wa ajabu na kulipua hasira yake zaidi, kwahiyo kama ameuzika kwa hali ya juu, kumtania kutaongeza matatizo mara mbili zaidi na kuona kama unamchukulia ki mzaha sana.

Unatakiwa kupima hali halisi, kama kosa lako ni kusahau kuendea maziwa dukani kama ulivyokua umemuahidi, ucheshi kidogo unaweza kumaliza tatizo, na iwapo kosa ni kuwa amekukuta na alama ya lipstiki kwenye shati lako la kazini lile jeupe, hapo kijana usiingize utani hata kidogo.

          #3; Mnunulie maua ukiambatanisha chokuleti na kadi.

Kumnunulia zawadi ni njia rahisi nzuri kuondoa mnuno wake.
Ushauri; Kumtumia maua au zawadi baada tu ya kumuuzi kunapoteza uzito, anaweza kukudhania unajaribu kumnunua kwa zawadi wakati unajua ulichokifanya kimemuuiza hisia zake.

Ili uweze kudhibiti hii hali, mtumie zawadi baada ya kuwa umeshazungumza naye na kuweka mambo kidogo katika hali nzuri, na itaongeza chachu nzuri zaidi maana hata kuwa anategemea kitu kama hicho kutoka kwako na kufanya aongeze hamasa zaidi juu yako.
Ukimtuia kazini kwake ni vizuri zaidi maana atapewa sifa na wafanyakazi wenzake na kukufanya uwekwe juu zaidi.

          #4; Msikilize kile anachokiongea.

Mara nyingi wanawake wanapenda kutoa hasira zao kwa kuongea, anataka kujua kuhusu tabia yako mbaya iliyomchukiza na kwanini imetokea hivyo, na unaweza kuta ni kitu kidogo tu, labda wewe hukumsikiliza vizuri na ndo kimesababisha mambo yote haya kutokea.

Kusikiliza ni karama, mwache aongee na hakikisha upo makini wakati unamsikiliza na ni vizuri ukamwacha aongee bila wewe kuingilia kati kwenye maongezi, kumuingilia wakati anaongea ili kujitetea kutasababisha zogo na kufanya tatizo lipanuke zaidi.

          #5; Ondoka.

Saa nyingine kitu cha msingi unachoweza fanya ni kuondoka, toka nje ya chumba au nyumba, mpe nafasi apumue hasira zishuke, ni mwiko na usijaribu kuondoka wakati bado anaongea, ukishatambua yupo kwenye hasira kubwa sana haja ya kuendelea kuongea naye haito saidia, kwa muda huo ni vizuri kumwambia kuwa unampa nafasi apunguze hasira na kuweka mawazo yake vizuri ili baadae muweze kuongea mpate mwafaka na kuelewana vizuri zaidi, baada ya hapo unaweza kuondoka.


          #6; Omba msamaha.

Mwishoni hakuna kitu kinachoweza kufunika neno "Samahani" lililotoka moyoni, na huwezi kumaliza ugomvi naye iwapo usipolitumia.

Hakikisha wakati unaliongea unalimaanisha, mwangalie machoni kwa upole na sema "SAMAHANI", usiseme naomba msamaha wala samahani matendo yangu yamekuudhi, maelezo kama hayo hufanya maongezi kuhusu hilo jambo yaendelee zaidi, sema samahani na maanisha kweli baada ya hapo bainisha samahani yako ni ya sababu gani ili aelewe umeelewa kwanini ulikua umemuudhi, kama ulikua ni uhusiano wa muda mrefu, mkumbushe mlikotoka.