Sunday, March 25, 2018

SIMULIZI FUPI POMBE SI DAWA YA MAPENZI


MTUNZI -ADELA DALLY KAVISHE

Jerome alikuwa na ndoto ya kuwa mfanyabiashara mkubwa sana, Alikuwa ni kijana mchapa kazi na wakati wote alikuwa makini sana. Katika maisha yake alisema kamwe hawezi kuchanganya kazi na mapenzi. Kijana huyu alikuwa ni mkarimu mtanashati na mwenye mvuto wa hali ya juu, baadhi ya wanawake walikuwa wakitamani kuwa karibu naye lakini Jerome alikuwa na msimamo hakutaka kabisa kujiingiza katika suala zima la mapenzi.

Akiwa anaendelea  kazi zake ambapo kazi zote alikuwa akizifanya akiwa anaishi Mkoa wa Dodoma. Baadaye alianza kusafiri  na kwenda katika mikoa mbalimbali hususani Mkoa wa Dar es salaam ambapo alikuwa akikutana na wafanyabiashara mbalimbali.

Siku moja akiwa jijini Dar es salaam katika shughuli zake alikutana na dada mmoja ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa chuo na walifahamiana, na kisha kubadilishana namba za simu. Baadaye waliendelea na mawasiliano wakiwa kama marafiki na hatimaye baadaye Jerome aliamua kufungua ukurasa wa mapenzi katika moyo wake na sasa alimpenda sana binti huyu aliyejulikana kwa jina la Selina  makazi yake yalikuwa ni Dar es salaam, mara nyingi Jerome alikuwa akija Da es salaam na wakati mwingine huyu mchumba wake alikuwa akienda Dodoma mapenzi yalikuwa motomoto. Jerome aliamini kabisa kuwa Selina angekuja kuwa mke wake alijitolea kwa kila kitu yaani aliamua kumlipia ada ya chuo na matumizi mengine.
Baada ya mwaka mmoja, Selina akiwa ndiyo anamaliza masomo yake ya chuo, Jerome aliamua kumwambia kuwa wafunge pingu za maisha pindi atakapomaliza chuo. Jambo ambalo Selina alimuhakikishia kuwa asiwe na shaka kwani wangefunga ndoa.
Jambo la kushangaza baada tu ya Selina kumaliza chuo ikiwa ni miezi michache  imepita, siku hiyo Jerome alikuwa amempigia simu, mwanzoni simu hiyo iliita bila kupokelewa na baadaye ilipokelewa na sauti iliyosikika ilikuwa ni ya mwanaume "Habari yako samahani naomba kuongea na mwenye simu" Alisema Jerome "Wewe nani, unapiga simu usiku, na kusumbua watu wakiwa wamelala, ehee ulikuwa na shida gani? mwenye simu amelala, mimi ni mume wake unaweza kusema ulikuwa na shida gani?"
Jerome hakuamini kile alichokisikia aliona kama ni ndoto  alibaki ameduwaa na yule kaka alikata simu. Kesho yake Jerome hakufanya kazi kabisa alikuwa na mawazo sana, akaamua kufunga safari hadi Dar es salaam, alipofika alienda moja kwa moja hadi kwa ndugu zake na Selina na ndipo alipoambiwa ukweli kuwa Selina ameolewa siku za karibuni. Jerome aliumia sana moyoni huku akiwa haamini kilichotokea katika maisha yake. Jerome alikuwa si mtumiaji wa pombe lakini tokea hapo aliamua rasmi kuanza kuwa mlevi ili aweze kupoteza mawazo na pia alijikuta akijiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na wanawake tofauti tofauti, kila kukicha na sasa biashara zake zilikuwa haziendi vizuri kama mwanzo.
 Baadaye Jerome alikuja kuugua sana na alipoenda kupima aligundulika kuwa ameathirika na virusi vya UKIMWI. Alilia sana na kujuta yote aliyokuwa akiyafanya "Eeeh Mungu naomba unisamehe, sikujua kama mapenzi yangeweza kuyaharibu maisha yangu kiasi hiki, nawashauri watu wote hasira ni hasara, unaweza kufikiri kunywa pombe au kuwa na wanawake tofauti tofauti, vinaweza kutuliza maumivu katika mapenzi, fahamu kuwa unajidanganya mwisho wake ni mbaya sana. ama kweli  POMBE SI DAWA YA MAPENZI maumivu yaliyopo moyoni mwangu yamebaki palepale.