Tuesday, March 6, 2018

NCHINI TANZANIA ....WANAWAKE MIJINI WALEMEWA VITAMBI

 
UWEZEKANO wa wanawake wa mijini kupata vitambi ni mkubwa mara mbili ya asilimia 32 kwa miaka kumi ijayo tofauti na wa vijijini kwa asilimia 12 katika miaka hiyo, imeelezwa. 

Hata hivyo hali ya mama na mtoto kwa sasa ni bora, licha ya kujitokeza tatizo la vitambi na karibu matatizo yote yanayohusu ustawi wa mama ni makubwa zaidi kwa wanaoishi vijijini kuliko wa mjini. 

Hayo yalielezwa na Mratibu wa Elimu ya Awali kutoka Idara ya Elimu ya Msingi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Clarence Mwinuka, Jumatano iliyopita wakati akiwasilisha mada juu ya umuhimu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi minane. 

Mratibu huyo alikuwa ni miongoni mwa wawezeshaji wa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, ambayo yalihusu hali halisi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto Tanzania. 

Alisema moja ya sababu kubwa za wanawake wa mjini kuota vitambi ni matumizi ya vyakula vya aina mbalimbali bila kuzingatia mazoezi ya mwili, tofati na wa vijijini ambao wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za uzalishaji mali. 

Alisema utafiti uliofanyika miaka ya karibuni na Idara hiyo kushirikiana na baadhi ya taasisi na makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya watoto, ambapo wanawake wa mijini wanapaswa kufanya mazoezi ya viungo, ili waondokane na vitambi. 

Hata hivyo, alisema utendaji mbovu, malezi, makuzi na maendeleo ya watoto wadogo, ni kutokuwa na bajeti mahususi kwa ajili ya watoto, kukosekana mpango wa utekelezaji na mwongozo wa viwango vya huduma bora. 

Kwa mujibu wa Mratibu huyo, watoto nchini wako katika hatari ya unyanyasaji, ukatili na uonevu, kutokana na kukosekana sheria ya kulinda mtoto inayotekelezeka na kuwa wanawake wamekuwa na sauti ndogo katika uamuzi wa mambo yanayowahusu. 

Mratibu huyo alisema umuhimu wa lishe kama msingi wa makuzi bora bado haujatambuliwa ipasavyo nchini, ambapo matatizo yanayotokana na lishe duni kwa watoto wenye umri wa miaka chini ya mitano, ni udumavu kwa asilimia 37.7 na uzito mdogo asilimia 21.8 na ukondefu asilimia tatu.