Saturday, January 27, 2018

Namna 10 ambazo watu huwasaliti wenzi wao bila kujua


1. KUTANIANA KIMAPENZI
Kutaniana kidogo na wafanyakazi wenzako ofisini sio jambo baya, unaweza kulidhibiti. Lakini epuka kutaniana nao kimahaba na kimapenzi, hilo ni hatari sana. Mtu akikutania kimapenzi usimtilie maanani. Ni mambo yapi yanayoingia kwenye utani wa kimapenzi? Kuzungumza na kuwa na mwenendo unaoashiria ukaribu usiokuwa wa kawaida na unaoashiria utashi wa tendo la ndoa kwa mtu asiyekuwa mumeo au mkeo. Hilo linaweza kufanyika kwa mawasiliano yenye utani wa kimapenzi, lugha ya mwili, kukonyeza, kutomasa na kadhalika.

Watu walio kwenye ndoa hawapaswi kuwa na tabia hii mbele ya watu ambao sio wenza wao. Hiyo ni aina ya usaliti ambayo huwapeleka pabaya. Yule unayemtania anaweza kulichukulia kama utongozaji na kukuingiza kwenye uhusiano ambao hukuukusudia.

2. KUMFANYA MTU WA JINSIA NYINGINE KUWA MSIRI WAKO.
Unapoyamwaga matatizo yako kwa mwanaume au mwanamke mwingine unakuwa unajiweka katika hali mbaya. Unaweza kudhani kuwa hilo halina madhara yoyote. Lakini, kama unahitaji mfariji, na kama una tatizo, basi lizungumze kwa mwenza wako. Mwenza wako ndio mfariji bora kabisa. Hilo lisipofaa jaribu kuongea na ndugu yako unayemuamini, au kiongozi wa kidini, au mtaalamu. Usimwambie mtu ambaye anaweza kuichukulia hatua yako kama unamtaka. Hata kama athari yake haitaonekana mara moja, mara nyingi huwa inaelekea huko. Hiyo ni aina ya usaliti.

3. KUKAA NA MTU WA JINSIA NYINGINE BILA UWEPO WA MWENZA WAKO.
Kitu kinachoonekana kuwa ni cha kawaida kwa kukaa pamoja na mtu wa jinsia nyingine au kupiga nae soga nyumbani kwake bila mwenza wako kuwepo ni sehemu ya tabia ya usaliti. Wewe au mtu huyo anaweza kusema: "Sisi ni watu wazima, hakuna kitakachotokea." Lakini mambo hutokea. Usifanye hivyo, sio jambo sahihi. Nenda nyumbani na utumie muda wako kukaa na mwenza wako.

4. KUMZUNGUMZIA VIBAYA MWENZA WAKO
Unapokuwa rafiki wa kweli wa mtu huwezi kuzungumza mambo mabaya kumhusu. Mwenza wako ndio rafiki yako bora kabisa na ndiye mtu wa mwisho unayeweza kumzungumzia vibaya. Iwapo una mgogoro na mwenza wako, zungumza naye. Mazungumzo yako yajikite kwenye mambo yake mazuri. Kumzungumza na kumtangaza vibaya mwenza wako ni usaliti.

5. KUPIGA SOGA (Chat) KWENYE INTANETI NA MWANAUME AU MWANAMKE
Kama unadhani jambo hilo halina tatizo, fikiria tena. Inaweza kuanza kawaida, lakini haitaishia hapo. Baadhi ya wanandoa hujiingiza kwenye mazungumzo na wanaume au wanawake ambayo wanaona kama ni ya kawaida, mwisho wa siku wanazihatarisha ndoa zao. Usifanye hivyo. Itasababisha uingie mashakani na kuiharibu familia yako.

6. KUJIPAMBA ILI KUWAVUTIA WATU WENGINE
Iwapo unavaa na kujiremba kwa ajili ya mtu mwingine tofauti na mumeo/mkeo, basi angalia tena sababu yako hiyo. Kujaribu kumvuta mtu mwingine kwa kuvaa mavazi yenye kurusha roho za wanaume/wanawake ni hatua ya kubwa ya kuelekea kwenye kina kirefu cha maji ya usaliti.

7. KUMUANDIKIA UJUMBE WA KIMAHABBA MTU MWINGINE
Kama unaandika ujumbe wa rambirambi au tahania, au kuwatakia heri watu, basi ni bora ujumbe huo utumwe kutoka kwenu nyote wawili, yaani uwe ujumbe unaotumwa kwa niaba yako wewe na mumeo. Hapo hapatokuwa na uelewa mbaya kuhusu nia yako.

8. KUTOKUWA NA UTAYARI WA KUMPA TENDO LA NDOA
Kuwa mwaminifu kwa mwenza wako ina maana ya kujitoa mzimamzima kwa ajili yake na kufurahia ukaribu wa kimahabba wa ndoa yenu. Kumnyima penzi mwenza wako sio jambo zuri katika kuimarisha ndoa yenu. Hatua hiyo huzalisha huzuni na hata kutiliana shaka. Kuwa mwaminifu kwa mwenza wako ina maana ya kutekeleza jukumu lako ili kuufanya uhusiano wa ndoa yenu kuwa maridhawa katika vipengele vyote.

9. KUWAWEKA WAZAZI WAKO KABLA YA MWENZA WAKO
Daima mwenza wako anatakiwa kuwa namba moja katika maisha yako. Unapokuwa na habari njema, mfanye mwenza wako awe wa kwanza kujua, kisha ndo uisambaze kwa watu wengine.

10. KUWAWEKA WATOTO MBELE YA MWENZA WAKO
Watoto ni watu muhimu sana katika maisha yako, lakini sio muhimu zaidi ya mwenza wako. Ukimuondosha mwenza wako kwenye kilele cha orodha ya vipaumbele vyako utakuwa huoneshi uaminifu kamili kwake. Mwenza wako anapaswa kuwa namba moja. Sio tu kwamba hatua hiyo itaimarisha ndoa yako, bali pia itawapa watoto wakeo usalama ambao wanastahiki kuupata.

Jipime kupitia nukta hizo nilizokutajia na uhakikisha kama wewe ni mwaminifu kwa mwenza wako kwa asilimia 100. Kwa kufanya hivyo utatengeneza ndoa yenye furaha halisi na imara.