Friday, December 15, 2017

Nini Sababu za Kuchepuka ? Je Kuchepuka ni Asili au Tabia ?

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa sana na malalamiko ya kila kukicha ya wanandoa wengi kutokuwa waaminifu. Wapo waliokabiliana na misuguano, mapigano na magomvi mengi kwasababu ya jambo hili na wapo ambao tayari wameshaamua kutengana. 

Watoto wa familia nyingi sana wamebaki kuwa wahanga wa tatizo hili na bado hakuna dalili za tatizo hili kupungua. Kila mmoja akiulizwa anatoa sababu yake binafsi ya kwanini ametoka au alitoka nje ya ndoa yake, sababu hizi zinamfanano na baadhi zinatofautiana pia. Katika makala hii nimejaribu kuangalia baadhi ya sababu ambazo mara kwa mara zimeripotiwa na wanandoa wengi wanaokuja kwenye ushauri kwenye ofisi zetu. 

Hii inafanya sababu hizi kuwa halisi na zitakazokupa msaada ukizielewa maana haziko kinadharia tu bali zimetokea katika maisha halisi ya ndoa za watu kama wewe. Pamoja na yote haya ukweli unabaki kwamba matendo ya kukosa uaminifu kwenye ndoa au mahusiano yana athari mbaya sana na athari hizi zinaweza kuambatana na maumivu makali na wahusika kuwa maadui badala ya wapenzi kama walivyokuwa awali.

Sababu ya 1: Kutoridhishwa katika tendo la ndoa


Kumekuwepo na malalamiko mengi na yatofauti baina ya wanandoa wanaume na wanawake katika suala hili. Wanaume wanalalamika kwamba wake zao mara baada ya kuolewa na hususani wakishapata watoto wanaanza kuwa wazembe na wasiojituma kwenye tendo la ndoa kama walivyokuwa awali. Tafiti zinaonyesha kwamba mara mwanaume anapohisi kutoridhishwa kwenye tendo la ndoa ananafasi kubwa zaidi ya kutoka nje mapema kuliko mke wake. Wanawake wanauvumulivu wa ziada na kwa wale waliotoka nje ya ndoa zao walifanya hivyo baada ya uvumilivu wa miaka mingi na kukosa tumaini. Kutoridhishwa katika tendo la ndoa kunaweza pia kusababishwa na maumbile ya mwili, kwa mfano watu wenye miili mikubwa na uzito mkubwa hupata shida kwenye kuwaridhisha wenzao ukizingatia kwamba tendo la ndoa ni zoezi la kimwili “physical exercise”. Mtu wa jinsi hii anaweza kushindwa kwasababu ya ukubwa wamwili, kushindwa kuutuma mwili wake kadri anavyotaka na pia wengine kuishiwa pumzi au kuchoka mapema na hivyo kufika kileleni mapema sana. Hali hii husababisha kutoridhika kwa wanawake wengi sana kwenye ndoa.

Sababu nyinginezo zilizotajwa za wanandoa kutoridhishana kwenye tendo la ndoa ni kama vile, uchafu, harufu zisizo nzuri, uelewa mdogo wa namna ya ufanywaji wa tendo hilo, makuzi na mapokeo, mambo yanayohusiana na mila, utamaduni au imani pamoja na magonjwa.

Sababu ya 2: Kutokupata tendo la ndoa kwa muda mrefu

Waathirika wa sababu hii ni wanaume kuliko wanawake. Tunaposema muda mrefu, hili ni suala la tofauti kwa mwanaume na mwanamke. Kwa mwanaume wiki moja yaweza kuhesabika ni muda mrefu kulingana na mazoea yaliyokuwepo kwenye ndoa hiyo. Kisayansi na kibaiolojia, mwanamke anauwezo wa kustahimili au kuvumilia kukaa bila kufanya tendo la ndoa kwa muda mrefu kuliko mwanaume. Baadhi ya tafiti pia zimeonyesha kuwa watoto wengi wa nje ya ndoa wanazaliwa katika vipindi ambavyo tendo la ndoa lina shida, hii inamaanisha nyakati za ugonjwa, ujauzito, magonvi makubwa au vipindi vingine vilivyofanya mwanaume asipate tendo la ndoa ndipo ambapo aliamua kuenda pembeni na huko kukatokea mimba na baadaye mtoto. Utaelewa ukubwa au kiasi cha tatizo kwa kuangalia ukweli kwamba kwenye ndoa nyingi, wanaume ndio wanaoongoza kwa kuwa na watoto nje ya ndoa na sio wanawake. Katika jambo hili la kutokupeana tendo la ndoa kwa muda mrefu, tumekuwa tukishauri kwamba kila mwanandoa ahakikishe anaweza kuzuia migogoro isiathiri tendo ndoa ili wasikae muda bila kulifanya, na kama kuna safari au utengano wa lazima baina yao basi kuwepo na mawasiliano ya mara kwa mara na ikibidi wanandoa watembeleane au kuwa pamoja zaidi ya kutokuwa pamoja. Umbali una athari kubwa sana kwenye ndoa nyingi. Kwa mara nyingine niseme hili, kunyimana tendo la ndoa kama adhabu au kwa matakwa yeyote binafsi hakujengi bali kunabomoa, kwasababu wengi wamejikuta wakitoka nje ya ndoa zao kwasababu hii.

Sababu ya 3: Hofu zinazohusiana na tendo la ndoa

Kati ya vitu vinavyowasumbua wanandoa wengi hususani wanaume kwenye kushindwa kushiriki tendo la ndoa au kulikinai kabisa ni suala zima la kuwa na hofu au woga wowote ule. Hofu na woga katika eneo hili huweza kuletwa na vyanzo tofauti kama vile masengenyo na kejeli pale mtu anavyojaribu kuomba kupata tendo la ndoa au hata baada ya kushiriki tendo hilo. Maranyingine maneno haya yanaweza kurushwa kama utani lakini yanapoingia kwenye moyo wa mwanandoa mhusika yanajenga hofu kubwa akidhani kwamba unamaanisha. Hofu nyingine yaweza kutokea kwenye dhihaka zinazofanywa pale mmoja anapoonyesha kutokufurahishwa au kutoshelezwa na mwenzake. Hapa kunatofauti ya kijinsia, mwanamke anahitaji busara ya hali ya juu kwenye kuongea na mume wake kumwambia kama hajaridhika, pale mwanamke anapoamua kutumia dhihaka, matusi au maneno makali, humwondoa kabisa mwanaume kwenye uwezo wake wa tendo wakati mwanaume huyuhuyu akienda kujaribu pembeni anajikuta bado yuko vizuri wakati kwa mkewe alishindwa, hilo linapotokea inakuwa ngumu sana mwanaume huyu kurudi au kupenda tena kufanya tendo la ndoa na mkewe. Fahamu kwamba hofu ya aina yoyote ni kikwazo na sumu kubwa ya tendo la ndoa, na athari zake ni kubwa zaidi kwa mwanaume kuliko mwanamke.

Sababu ya 4: Penzi kupoa au kufa

Penzi linapopoa au hata linapokufa huwa hali huwa inaonyesha wazi kabisa. Kwenye kupoa mhusika anaweza kuanza kujihisi ndani ya moyo wake kutompenda mwenzake kama alivyokuwa akimpenda awali. Inawezekana mwenzake hajagundua kuanzia mwanzoni kwamba penzi la mpenzi wake limepoa ila kama hali ya kupoa huku itaendelea lazima itagundulika. Baadhi ya vitu dhahiri vitakavyoweza kukufanya ufahamu kwamba penzi la mwenzako limepoa au kufa nikwamba kuna mambo ambayo uliyazoea kuyaona yakifanywa kawaida hautayaona tena. Kuna vitu vilikuwa vikifanywa pasipo kukumbushana sasa utalazimika kuviomba ili ufanyiwe, utaona kila kitu kinakuwa kigumu kumhusu mwenzako na hata uongeaji au kujibu kwake kunakuwa na walakini. Kwenye tendo la ndoa nako maranyingi ndiko kwenye kuonyesha taa nyekundu mapema, ule ushiriki, furaha na bashasha zilizokuwapo awali mkiwa kwenye tendo hauzioni tena, tendo la ndoa linafanywa kama jukumu la kawaida na maranyingine hata hamu ya kushiriki haipo. Hapa ndipo mmoja hukinai hiyo hali ya kulazimishana tendo la ndoa, au kupeana kwa masharti au kunyimwa au hata mmoja kupoteza hamasa ya kulifanya tendo hilo na mtu asiyekuwa na hisia naye. Huo unakuwa mwanzo wa mmoja au wote kutoka nje ya mahusiano au ndoa. Penzi ni kama moto, ukiwashwa pasipo kuchochewa hupoa au hata kuzima kabisa. Wengi wanapoingia kwenye ndoa wanadhani mkishaoana basi mambo yanajiseti yenyewe tu, mapenzi yanajichanulia yenyewe tu, la hasha! Lazima kuwepo na jitihada za dhati za wanandoa kuhakikisha wanachochea penzi lao, kulilinda na kulipalilia ili liendelee kumea, kunawiri na kuzaaa matunda.


Sababu ya 5: Ushawishi wa marafiki

Wako watu wengi sana kwenye ushauri wa wanandoa na hata wale wasiowanandoa ambao wamekiri kuchepuka kwasababu ya kushawishiwa na marafiki. Ni lazima ukafahamu nguvu waliyonayo marafiki. Usipokuwa na hekima ya juu ya kuweza kuchagua nani wa kuwanaye rafiki na nani sio basi utajikuta unapelekeshwa kila upande hata kule usipopenda utapelekwa kwasababu tu nguvu ya maamuzi haiko kwako tena bali iko kwa marafiki zako. Yamkini unasema mimi ni rafiki tu sifanyi vile wanavyovifanya wao, mimi nasikiliza na kuchangia tu hoja zao, lakini ngoja nikwambie, taratibu utasikiliza, taratibu utaanza kuchangia na taratibu utavutika kuyafanya yale wanayoyafanya. Yamkini wao kuchepuka ni hadithi ya kwaida na kwako sio kawaida, ukiendelea kukaa nao kidogokidogo utaanza kuona kuchepuka sio kitu cha kushangaza sana maana wengine nao wanafanya, na utaanza kidogokidogo na mwisho utakuwa mtaalamu. Wako waliofundishwa kiutaniutani leo hii ni wataalamu kuliko walimu wao. Jifunze kuwa na msimamo. Jifunze kuchagua marafiki wanaokujenga na sio kukubomoa. Jifunze kufanya maamuzi binafsi yenye busara na yasiyokufungulia milango ya majuto. Kumbuka ukijakujuta hautokula majuto hayo na hao marafiki zako. Utayala mwenyewe na wanaokuhusu. Ni hasara na anguko kwao na familia yako na ndugu zako.


Sababu ya 6: Ushawishi wa kilevi (pombe au madawa)


Wako watu wanaojiamini sana na wanajihisi wenye uwezo wa kujizuia, lakini mara wanapokuwa katika ulevi wowote ule hushindwa kujizuia. Hili liko kwa wanawake na hata wanaume. Tabia ya ulevi wowote hupunguza uwezo wa mtu wa kufikiria ilivyo sahihi “rational thinking”. Unaweza kukuta watu wameketi pamoja na wanaheshimiana lakini kwa kadri wanavyoendelea kulewa wanaanza kushikana maungo na kila mmoja anaona nisawa tu, heshima na nidhamu waliyokuwa nayo awali imeshapeperukia dirishani kwasababu ya ushawishi wa ulevi “the influence of alcohol”. Hali hii ina majuto sana maana mtu anajikuta kasha shiriki ngono na mtu mwingine, ama mtu anayemjua au hata asiyemjua pasipo utashi wake. Majuto yanakuwa makubwa zaidi maana mara nyingine hata usiri unakuwa haupo, heshima na nidhamu yako yote inaathirika. Ziko baadhi ya pombe ambazo badala tu ya kukuondolea aibu, zinaweza kukulegeza mwili na viungo na kuongeza hamu ya ngono. Ndio maana watu wanaotumia vilevi wanashauriwa kuwa na wenza wao katika nyakati hizi ili walao kujizuia kuingia mitegoni. Watu wengi tuliowahoji nyakati za ushauri wanakiri kwamba safari ya kuingia kwenye mahusiano ya kingono na watu wanje ilisindikizwa zaidi na matumizi ya kilevi au vilevi, na wengine wanaendelea kukiri kwamba ni ngumu kuchepuka bila kuwa na kilevi akilini.

Sababu ya 7: Kutostahimili ukaribu usio na mipaka

Wapo watu wengi ambao wamejikuta wakikamatika katika mahusiano ya kingono na wale waliowaita marafiki wakaribu. Mwanzoni alionekana kama rafiki, mnashauriana, mnasaidiana, mnasindikizana, mnatembeleana, na wala haukuwahi kudhani mngefikia hapo mlipofikia. 
Lakini kwasababu mlishindwa kuwamakini kwenye kuilinda mipaka ya urafiki wenu, sasa uhusiano wa kawaida na waurafiki umekuwa uhusiano wakingono. Hali hii huathiri uthamani wa urafiki baina ya watu na maranyingine waliokuwa marafiki wanaweza kujakuwa maadui kabisa. Ukaribu zaidi na mtu wa jinsia ya tofauti na wewe huwa sio mzuri sana kwa afya ya mahusiano au ndoa yenu. Yamkini unajitetea kwamba hakuna kinachoweza kutokea lakini fahamu kwamba hata kikija kutokea hautakuwa na ujasiri wa kusema kwamba kuna kilichotokea. 
Heri kuziba ufa kuliko kujenga ukuta. Ninakushauri kwamba watu wote ambao uko nao karibu nivema wafahamike kwa mwenza wako, epuka urafiki wa sirini, na mikutano ya sirini. Mkutano na rafiki ambaye ukonaye karibu na wajinsia tofauti kamwe usifanyike maeneo yakificho au sehemu ambayo mkopekeyenu. Yamkini nia na dhumuni lenu sio ovu lakini mazingira shawishi yanaweza kuwafikisha ambako hamkupanga kufika. Kuwa na ujasiri wakuiweka mipaka ya urafiki wenu bayana, na rafiki yako au rafiki zako waiheshimu mipaka yako. Iheshimu mipaka hiyo maana usipoiheshimu mipaka yako na wengine kamwe hawawezi kuiheshimu mipaka hiyo. Pia ukitaka watu waheshimu mipaka yako na wewe pia iheshimu mipaka ya wengine. Na mwisho ni kwamba kamwe usimwamini yeyote kwa asilimia 100, Jilinde uwapo mazingira yeyote.


Sababu ya 8: Kulipiza kisasi (revenge)

Aina hii ya kuchepuka huwa kwa wanaume na wanawake ingawa inaripotiwa zaidi kuonekana kwa wanaume kwasababu ya ukweli kwamba maranyingi wanaume wanaweza wakakwazika na bado wasifunguke kuelezea walivyokwazwa lakini wakati huohuo wanakiu ya kulipiza kisasi kwa maumivu waliyoyapata tofauti na wanawake ambao wao kufunguka ni rahisi na ni kawaida kwao. Wanaume kwa kawaida wanaweza kuamua kutoka nje ya ndoa kwasababu tu amekasirishwa na kuona haheshimiwi katika mambo flani kwenye mahusiano au familia. Kwamfano akihisi hasikilizwi, hapewi kipaumbele, hahudumiwi, anachosema hakifwatwi anavyotamani havifanywi basi kuna uwezekano mkubwa akaanzisha mahusiano pembeni kwa siri.

Tafiti za kisaikolojia zinasema kwamba mwanaume anapochepuka kwa msukumo wa hali kama hizi ile hali ya kujihisi anafanya kosa “guilty conscious” inapungua au kupotea kabisa na kwahivyo anaweza kujihesabia haki kabisa kwa kile anachokifanya. Hii inaweza kumfanya aendelee kuchepuka kwa muda mrefu zaidi tofauti na mwanamke ambaye hata hali hii ikijitokeza wengi huwa wanajihisi kuhukumiwa na kujisikia vibaya moyoni. Kuchepuka kwa kulipiza kisasi hutokea pia nyakati ambazo mwanandoa mmoja anahisi kuwa mwenzake ana mahusiano nje, iwe kuna ushahidi au nitetesi, wengine jambo hili humsukuma na yeye kufanya hivyohivyo ili kutafuta uwiano au kujisuuza nafsi. Kwa bahati mbaya matokeo ya tabia hizi yamekuwa hasi zaidi na kwa wengi imepelekea kuharibu mahusiano na ndoa. Ninashauri kwamba yanapotokea maumivu au makwazo ya aina yeyote yasihifadhiwe moyoni au kuonewa aibu kuzungumzwa maana visasi havilipi balihuongeza maumivu na uharibifu zaidi.

Sababu ya 9: Tabia ya asili, mfano, laana au urithi

Pamoja na kwamba mahusiano nje ya ndoa au kwa jina maarufu sikuhizi “kuchepuka” ni tabia na mazoea ya mhusika lakini tusisahau kwamba ziko kesi ambazo ni zaidi ya tabia. Ziko nyakati ambazo tunashuhulikia kesi ya ushauri ambayounaona wazi tabia ya mtu flani sio ya kujitakia au matamanio ya kawaida lakini kuna udhihirisho wa nguvu inayomsukuma kufanya ngono. Mtu anawezakuwa hatamani kabisa au hapendi anachokifanya lakini atajikuta tayari ametumbukia kwenye ngono na baada ya kufanya tendo hilo anajuta sana lakini bado kesho au keshokutwa atarudi kule kule. Ziko koo au familia ambazo zina laana kwenye maeneo haya, unakuta idadi kubwa ya wanaume au wanawake kwenye familia au ukoo flani wana watoto nje ya ndoa, watoto waliopatikana kabla ya ndoa au watoto wanaopatikana nje ya ndoa lakini mtu akiwa ndani ya ndoa. Hapa namaanisha mtu ana mke lakini tunasikia watoto wanaletwa au wanasemekana wamezaliwa na baba huyu. Kesi nyingi, na vikao vingi vya usuluhishi vinaketi vikijaribu kutafuta ufumbuzi wa tatizo. Labda mke anaweza kukimbia kwa kuchoshwa na akaolewa mwingine lakini bado mume anaendelea kuleta watoto wanje tu.

Iko mifano ya familia ambazo baba aliwahi kufahamika kuwa na tabia hizi za kuchepuka, na kwa bahati mbaya watoto wake wakiume au hata wakike nao wakaandamwa na roho ile ile ya baba yao. Yawezekana isiwe baba ikawa ni mama aliwahi kuwa na tabia hizi, alivyokuwa binti kabla ya kuolewa au hata akiwa na mume wake lakini kile kitu watu walichowahi kukiona kwa mama au baba sasa wanakiona kwa watoto wao. Hili ni suala la kurithi, na pia laweza kuwa suala la roho inayotembea. Masuala ya namna hii ni magumu kidogo kuyaelewa maana yanaonekana kwa jinsi ya mwilini lakini nguvu yake sio ya jinsi ya mwilini, na kwahivyo uelewa wake unaweza kuchanganya kidogo lakini fahamu tu kwamba yako dhahiri zaidi ya uwazavyo. Kuyashuhulikia kimwili, au kuyashuhulikia kama vile chanzo ni tabia za kawaida ni ngumu sana kuleta suluhisho. Mambo ya kiroho hayanabudi kushuhulikiwa kiroho. Na endapo kwenye ushauri tunakutana na kesi za namna hii tunamshauri mhusika au wahusika kulishuhulikia jambo kiroho zaidi. Kwa bahati nzuri wahusika wanapoelewa na kuanza mchakato wa kiroho ufumbuzi huwa rahisi sana.

Mwisho niseme kwamba hali yeyote ya kutokuwa mwaminifu kwenye mahusiano yako inanafasi kubwa sana kwenye kuleta uharibifu. Wako walioharibu ndoa zao na zikapasuka wakati bado walikuwa wanazipenda ziendelee kuwepo. Japokuwa kuchepuka hufanywa kwa siri kubwa lakini maranyingi siri hizi huwa ni za muda mfupi na kuna nyakati zinavuja au kuibuliwa na hapo ndipo machungu, majuto na machozi hutokea. Inawezekana kabisa majuto na machozi yakakupa nafasi ya kujirekebisha na kuiboresha ndoa yako iliyopata nyufa baada ya kuchepuka lakini pia inawezekana kabisa ukajuta, ukalia sana na bado usiiokoe ndoa yako maana yamkini mwenzako hatokuwa tayari kuendelea na wewe. Kama unaipenda ndoa yako basi utailinda, na mojawapo ya namna ya kuilinda ni kuwa mwaminifu