Monday, December 25, 2017

Linogeshe penzi lako kwa kuzingatia mambo haya !

post-feature-image
WAPENZI wasomaji wangu, naomba leo niende moja kwa moja kwenye mada yangu ya wiki hii ambayo kwa kiasi kikubwa inawagusa wanawake. Nazungumzia mambo ambayo mwanamke anatakiwa kuyazingatia ili aweze kumshika ipasavyo mumewe na kuinogesha ndoa yake.

Ni mengi anayostahili kufanya mke kwa mumewe lakini kwa leo nitazungumza machache ambayo naamini yatakuwa na manufaa kwako.

Timiza wajibu wako kama mke
Mwanamke anayemjali mume wake ndiye anayetimiza wajibu, lakini wengi hujikuta wakisalitiwa au kuachwa kabisa na waume zao kutokana na ufahamu mdogo ama dharau ya mambo madogo.

Ni busara kutambua kwamba, ndoa haina mambo madogo. Kila kitu kina umuhimu mkubwa kulingana na nafasi yake sambamba na utekelezaji wako. Mfano, kumpokea bahasha anaporejea kutoka kazini ni kitu kidogo tu ambacho wewe unaweza kukidharau lakini thamani yake kwa mumeo ni kubwa kuliko unavyofikiria.

Tambua kuwa, mwanaume harogwi kwa limbwata la sangoma, mahaba peke yake yanatosha kumshika vilivyo. ‘Ukimhendo’ kwa kiwango kitakachomridhisha, hatawaza kukuacha. Unawezaje? Jibu ni rahisi, muoneshe unampenda na uthibitishe mapenzi yako kwa vitendo na si kwa maneno tu.

Daima hili liwe kwenye akilini yako, mwanamke kupitia mapenzi yake ana uwezo mkubwa mno, lakini lazima awe anajua kutimiza wajibu wake kwenye maisha ya ndoa.

Kama mumeo anakuacha, ujue kuwa kuna mambo unayomkosea na kuyafanya mapenzi yako yageuke kuwa kero kwake. Unyenyekevu kwa wanawake wa kisasa kimekuwa ni kitu adimu sana kiasi ambacho kimekuwa kikihatarisha ndoa zao.

Wanaume wanawapenda wanawake ambao hujionesha waziwazi kuwa wenyewe ni wasaidizi wao wakuu katika masuala mbalimbali. Hawavutiwi na wale ambao hupuuza mambo kwa visingizio visivyokuwa na maana.

Kuwa mjanja kiana
Sababu ya wanaume kuwapenda wanawake wajanja ni kukwepa aibu wanazoweza kuzipata pindi watakapokuwa kwenye uhusiano na wanawake washamba.
Huogopa kujiingiza katika mapenzi na watu wasio na uelewa mpana wa mambo ambao  huwafanya kuwa mafundi wa kuiga mambo yasiyofaa.

Washamba mara nyingi huwa ni malimbukeni, hujifunza mambo yasiyokuwa na faida kwa imani kwamba naye ataonekana mtu kati ya watu. Wanawake wa aina hii ni rahisi kuwaingiza wenzi wao katika hasara kubwa. Hawakawii kusaliti pamoja na kudanganyika kwa mambo madogo.

Wanawake malimbukeni huharibika vibarazani na saluni kutokana na sifa kubwa ya umbeya kwenye sehemu hizo. Wanaume wasiokuwa na subira hujikuta wakiwaacha wake zao mapema, mara tu wanapoanza kuhisi nyendo zisizoeleweka kwa wenzi wao.

Tumekuwa tukishuhudia wanawake malimbukeni wakiiga tabia za ulevi wa pombe, kuwa na makuu katika maisha yao kutokana na kuwaona wenzao wakiwa hivyo. Hili ni tatizo ambalo wewe mke wa mtu unatakiwa kuliepuka ili uishi milele na mumeo.

Siku zote mwanamke mjanja hawezi kuiga hovyo hovyo, siku zote anajua kitu cha kuanzia na kinachofuata. Hadanganyiki kirahisi na hiyo ni sifa kubwa ambayo inaweza kuinogesha ndoa yako kwa kiasi kikubwa