Sunday, December 17, 2017

Kama Uchumba Ni Paradiso Kwanini Ndoa Iwe Jehanamu?


 Wapendwa wanasomaji, kwa wale waliowahi kupitia hatua ya uchumba hadi kufikia ndoa au hata wale ambao hawajawahi kupitia hatua hizo, lakini wameona mifano kadhaa kwenye jamii, watakubaliana na mimi kwamba ndoa nyingi "zinaumwa" na zinahitaji kutafutiwa "chanjo" au "tiba!"
  
 Naamini kwamba kabla ya kufikia ndoa wachumba huwa wanavumiliana na kupendana mno, kila mmoja anamwona mwenzake ni bora kuliko yeye! In fact kama hawajaonana siku inakuwa haijaenda sawa!


Lakini baada ya kuingia kwenye ndoa mambo hubadilika taratibu na kuanza kuleta kero, malumbano yasiyoisha, huzuni zisizoisha, ngumi, mateke, n.k. Kuna baadhi ya wachungaji huwa wanatumia usemi huu ufuatao wakati wanafungisha ndoa: "Wengi wa walio ndani (ya ndoa) wanaka watoke na walio nje (ya ndoa) wanataka kuingia!" Kwa maana hiyo ndoa ni taasisi ya ajabu sana!


 Swali langu ni kwamba kwa nini uvumilivu, upendo, huruma, kujaliana, (ambao mimi nimeuita "utamu") nk ambako kunaonekana kwenye uchumba usiendelee hata wakati wa ndoa?


 Lengo la mada hii ni kujaribu kuwasaidia wenzetu ambao wanataka kuingia kwenye ndoa pamoja na wale walioko kwenye ndoa ili waweze ku-"think twice" na kutengeneza mahusiano yao ili maisha yao yawe na ushuhuda mbele ya jamii na watoto (kama wamefanikiwa kuwapata).


 Kwa kuanza kutoa maoni, kwa  upande wangu naona kwamba (a) wengi wanaingia kwenye mahusiano kwa sababu ya "tamaa za mwili" kiasi kwamba wanaangalia uzuri wa nje zaidi kuliko wa ndani! Uzuri wa nje ukishaanza kuchuja upendo nao unaanza kuchuja vile vile! (b) Kingine ni kwamba baadhi ya watu (hapa nafikiri ni wengi zaidi) huwa wanaingia kwenye mahusiano kwa sababu ya kuangalia vipato zaidi kuliko upendo wa dhati, uchumi ukianza kuyumba, ndoa nako inaanza kuyumba na hatimaye kuvunjika!


USHAURI: Upendo wa kweli usiathiriwe na mazingira: uzuri, kipato na kadhalika! Hii ni sumu mbaya katika ndoa! Naomba maoni yenu zaidi.