Saturday, December 23, 2017

Je, Unazijua Sifa Za Mwanaume Anayefaa Kuwa Mwenza Wako ?

Je, unazijua sifa za mwanaume anayekufaa kuwa mwenza wako? Hili limekuwa swali gumu kwa wanawake wengi ambao wamekuwa wakijiuliza watawezaje kuwafahamu au kumfahamu mwanaume f’lani kama ana sifa za kuwa mpenzi wake? Mwanaume anayekufaa katika uhusiano wa kimapenzi lazima awe na sifa zifuatazo;

AWE CHAGUO LAKO
Ni lazima mwanaume unayetaka au unayempenda awe mpenzi wako, awe na sifa kubwa ya wewe mwenyewe kumpenda, kumridhia na siyo kumpenda kwa sababu au shinikizo f’lani.

MWENYE KUJIAMINI

Mwanamke anapokuwa na mwanaume anayejiamini, anaamini yupo salama zaidi. Hata kama kuna lolote linaloweza kutokea wakiwa wote basi mwanamke hatakuwa na woga kwa sababu tu anaamini yupo na mwanaume mwenye kujiamini ambaye atakuwa kinga au mtetezi wake.

MWENYE UAMUZI
Mwanaume mwenye uamuzi ndiye anayekufaa kwa ajili ya kujenga uhusiano makini na ulio bora. Yule mwenye uwezo wa kusema jambo na kulisimamia. Awe mtu mwenye msimamo na asiyetetereka kwa jambo lolote linaloweza kumyumbisha katika uhusiano wake, kwa sababu yeye ndiye aliyeamua kupenda basi hayuko tayari kusikiliza maneno ya pembeni kwa sababu anaamini katika fikra zake.

ASIWE MVIVU
Ili kuhakikisha kuwa familia au uhusiano wako hauyumbi, mwanaume asiyekuwa mvivu ndiye anayekufaa.

Awe mtu ambaye anajituma ili kudumisha penzi na hata familia yake. Uvivu ninaouzungumzia hapa ni ule wa kimajukumu ya kutafuta fedha na anapokuwa faragha.

ANAYETUNZA SIRI
Katika uhusiano wako kuwa na mwanaume mwenye uwezo wa kutunza siri za ndani hata kama mtakuwa mmekoseana au kuhitilafiana. Awe tayari kuvumilia jambo hilo moyoni mwake. Kama ukiona amelitoa nje basi ujue limemzidi uwezo, ndiyo maana kuna wakati mtu akitaka kukwambia jambo anakuuliza ‘je, una kifua?’

Kuna mambo mengi sana nyuma ya uhusiano ambayo mengine hayastahili kumwambia kila mtu hivyo lazima mwanaume wako awe mtunza siri.

ASIYEPAYUKA
Uhusiano wowote una migongano kama ambavyo kazi zote zina changamoto katika utendaji wake. Kwenye uhusiano, unapaswa uchague mwanaume asiye na tabia ya kupayuka mnapokuwa mmekosana. Tabia ya kupayuka kiasi cha kuwafanya hata majirani wajue jambo mnalogombania haifai.