Thursday, November 9, 2017

Tumia Vizuri Baraka Alizokupa Mungu, Angetaka Kukufanyia Kila kitu Asingekupa Baraka Hizo

Mungu angetaka kukufanyia kila kitu asingekupa miguu ya kutembelea, asingekupa mikono wala macho ya kuona na masikio ya kusikia. Asingekupa akili ya kufikiria na wala asingekupa nguvu za kufanyia kazi. Angekufanyia kila kitu na wewe kukaa tu, ana uwezo huo na angeweza kufanya hivyo lakini hakufanya.
Lengo kuu la Mungu kukupa hivyo vitu ulivyonavyo nikwasababu yeye huanzia pale miguu yako inapoishia kutembea, huanzia pale mikono yako inaposhindwa kushika, pale macho yako yasipoweza kuona, pale ambapo masikio yako hayawezi kusikia na kubwa zaidi pale ambapo akili yako inapoishia kufikiria ndipo nguvu zake huhitajika.
Acha kukaa tu na kusubiri Mungu atende, kuishi kwenye maombi ukiomba baraka zake huku ukiwa hufanyi chochote. Kama unamjua Mungu vizuri basi ungejua kua tayari ameshakupa baraka unazoziomba amekupa baraka ya Mikono, itumie, kashakupa baraka ya miguu, kashakupa baraka ya macho, masikio, akili na nguvu ya kufanya kazi.
Nibaraka nyingine ipi tena unaanza kuomba kama hiyo aliyokupa sasa umeshindwa kuitumia. Unadhani ni wangapi ambao wanaomba kuwa kama ulivyo sasa na Mungu bado hajaamua kuwabariki. Hembu jiulize hutumii mikono yako kufanya kazi, miguu yako kufanya kazi unaomba Mungu akuletee chakula vipi yule ambaye hana mikono au miguu.
Una afya njema umekaa tu nyumbani unalalamika vipi wale waliopo mahospitalini. Wao wanahitaji kumuomba Mungu kuwapa afya kwanza kabla ya kumuomba baraka nyingine wewe tayari unayo baraka ya afya lakini bado unalalamika. Mshukuru Mungu kwa baraka alizokupa, zitumie vizuri na muombe akuongoze katika kuzitumia.
Acha kusema kila kitu unamuachia yeye wakati tayari kashakubariki, tumia baraka alizokupa kwa kadri ya uwezo wako na elekeza sala zako katika kumuomba yeye kuanzia hapo ulipoishia, pale ambapo huna uwezo napo. Mshukuru kwa kutumia alivyokujalia kuwa mtu bora zaidi na si kwa kulalamika kila siku kuwa huna bahati wakati kuzaliwa jinsi ulivyo ni bahati kubwa.