Wednesday, November 15, 2017

MNASIKIANA AU MNASIKILIZANA???



Ipo tofauti kubwa kati ya neno kusikia na kusikiliza, hauhitaji kuwa na digrii ya mawasiliano au kuwa mtaalamu wa mawasiliano ili kujua hili. Kusikia ni kitendo cha masikio kuhisi sauti pasipo ulazima wa kuitafsiri maana ya hiyo sauti, wakati kusikiliza ni pale masikio na akili vinapohusika pamoja kuihisi sauti, kuielewa na kuitafsiri maana yake na kuandaa mrejesho kwa kile kilichosikiwa (akili inaelewa kilichosemwa). Sasa kwa kufahamu utofauti huu utagundua kabisa kwamba maranyingi kwenye mahusiano baina yetu na wapenzi wetu tuna sikiana zaidi ya kusikilizana. Hakuna aliyetayaru kumpa mwenzake sikio kwa nia ya kumsikiliza na kujali kile mwenzake anachosema, kila unachojaribu kusema kinapuuziwa na kutokueleweka. Ukosefu wa kusikilizana unaathiri sana mawasiliano baina ya wewe na mpenzi wako na huo ni ufa mkubwa sana katika kuongeza misuguano, tofauti, migogoro na hata kufikia kuachana. Bahati mbaya wanaume wachache wanajua kwamba mwanamke ameumbwa na kiu ya kusikilizwa zaidi kuliko mwanaume, na bahati mbaya kubwa ni kwamba mwanaume ndio kilema mkubwa wa kusikiliza, sasa basi kama kweli unampenda basi jitahidi kumsikiliza, sio tu kumsikia, na wewe mwanaume, zawadi pekee na ya maana unayoweza kumpa huyo mpenzi wako wa kike ni KUMSIKILIZA ..............