Kwa nini mapenzi ni tata? Unaweza kujiuliza swali hilo. Ni kwa faida ya kila mmoja kwa sababu yanamhusu kila mmoja wetu. Ni matamu lakini ndani yake hutokea kuwa na ukakasi kama siyo maumivu.Jiulize tena, kwa nini mapenzi yanasumbua? Mapenzi ni maumivu ya kichwa na moyo. Watu wengi waliomo ndani yake wanaweza kukupa ushuhuda wa mateso wanayoyapata kwenye uhusiano wao. Je, baada ya kuteseka huwa wanajiapiza kutorudi tena?
La hasha! Wanajaribu mara nyingi, hawakomi. Unaweza kujiuliza ni kwa nini lakini ukweli ni kwamba pamoja na maumivu ambayo mtu anaweza kuyapata kwenye mapenzi, bado yanabeba hisia kubwa kabisa katika maisha ya kila binadamu.
Maisha bila mapenzi hayajakamilika. Kutokana na hilo, uwanja upo wazi kwako kujiuliza ni kwa nini kitu kitamu namna hiyo kikafanywa kuwa tata, jumlisha na maumivu ya hapa na pale. Uvumilivu ukizingatiwa, huyeyusha utata unaojitokeza hapa na pale.
Muhimu zaidi ni kwamba mapenzi hayatoshelezi kwa uwajibikaji wa nusunusu. Yanahitaji nidhamu na utekelezaji wa moja kwa moja kutoka moyoni. Yanayomhusu mwenzi wako ni vema uyabebe kama yako, hivyo ndivyo uhusiano unavyotaka.
Mapenzi yanahitaji akili, utashi na fikra zako bila kusahau nguvu zote katika kuzalisha matunda ya kila siku kwenye uhusiano ulionao. Utata unaoonekana ni ule unaotokana na wenzi kutotimiza matarajio ya kila mmoja.
Imetokea kuamini kuwa maneno ni mhimili wa kudumu kwa uhusiano na ngono husuluhisha migogoro ya muda mfupi. Wapenzi wanaponuniana, endapo watakutana faragha, hasira zote hupotea. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, ni zaidi ya kutosheka kimwili na utamu wa maneno mazuri.Kwa mfano, ndoa nyingi zinakumbwa na matatizo ya watu kushindwa kuwa wakweli. Mwanaume au mwanamke anaweza kusema ni kiasi gani mwenzi wake anamuumiza. Lakini mwisho wa mazungumzo hawezi kukiri kasoro zake ambazo pengine ndiyo chanzo cha kila kitu.
Utata zaidi katika mapenzi ni kuwa inapotokea watu wanajuana kwa undani mno, hasa baada ya kuishi muda mrefu, ni hapo ndipo maneno hayawezi kufaa kitu, wala mchezo wa faragha hautaleta maelewano kwa maana hakuna kitu kigeni.
Lingine la utata katika mapenzi ni kwamba huwezi kuficha tabia yako muda wote.