Tuesday, November 14, 2017

Kama Unataka Kumsahau Basi Msamehe Na Muache Aende, Chakula Kikishatoka Tumboni Hakifai Tena Waachie Inzi

Mapenzi yanaumiza, tena sana si kidogo hasa pale unapoachana na mtu ambaye bado unampenda. Inaweza kuwa ni yeye kakuacha tena wakati mwingine bila sababu yoyote ile au ikawa ni wewe umemuacha kwa sababu umeshindwa kuvumilia baadhi ya tabia zake lakini bado ukiwa unampenda.
Kwa vyovyote vile njia rahisi ya kuweza kuendelea na maisha yako kwa furaha kwanza ni kukubali kuwa yameisha, kukubali kua hakuna namna ambavyo mnaweza kurudiana hata kama mnapendana vipi. Ukishakubaliana na hili inamaana kuwa hutajaribu kumtafuta au kutaka kumrudisha tena.
Hili ni muhimu sana kwani kuishi kwa matumaini kuwa labda atanirudia au tutarudiana unashindwa kumtoa kichwani na unashindwa kuendelea na maisha yako. Unashindwa kufungua moyo wako na kupenda tena. Pili unapaswa kujua kuwa kuna kupenda tena na kuna furaha nyingine.
Kwa maana kuwa hata kama hutakuwa tayari kwa wakati huo kuwa na mtu mwingine basi jua kuwa kama ulivyompata uliyeachana naye utapata mwingine lakini pia kama unavyompenda uliyeachana naye utapenda tena. Kwa kufanya hivi itakupa faraja na itakupa kitu cha kuangalia mbele, itakupa sababu ya kuishi tena kwa furaha.
Jambo la tatu unalopaswa kufanya ni kusamehe. Hapa inawezekana wewe ndiyo ulisababisha kuachika au kuachana, basi jisamehe wewe mwenyewe kwa uliyoyafanya, jifunze kutokana na makosa yako na jiambie utakuwa bora zaidi. Lakini pia inawezekana wewe ndiyo ulikosewa, basi huna haja ya kuendeleza kinyongo msamehe na jifunze kutokana na aliyokufanyia.

Najua wakati mwingine ni ngumu lakini kwa afya ya mahusiano yako yajayo msamehe kwa roho safi kabisa. Najua hutasahau, najua maumivu hayataondoka kirahisi namna hiyo lakini ukisamehe unaondoa donge katika roho yako hivyo kuondoa sumu ya chuki ambayo unakuwa nayo kwa kutokusamehe.
Ukishasamehe basi muache aende, hapa nikiimaanisha kuwa acha kumfuatilia anafanya nini? Yuko na nani? Acha kuangalia huyo aliye naye kakuzidi nini? Acha kumfuatilia huyo aliyeko naye/ acha kujaribu kuwagombanisha au kutaka kulipa kisasi? Acha kutafuta kasoro za huyo mpya na kujaribu kuzitumia kumharibi!
Kwa kifupi achana kabisa na maisha yake na muache aendelee na furaha yake. Hili ni jambo muhimu sana kwako kulifanya. Itakusaidia kujikita katika mambo yako, kutafuta furaha yako na kubwa kabisa haitakupotezea muda wa kumfuatilia. Anza maisha yako na kama  ukipata mtu mpya basi acha kumlinganisha na yule wa zamani.

Hutakuwa umesonga mbele kama kila unayekutana naye unampima kutokana na yule wazamani. Kila mwanadamu kaumbwa kipekee hivyo kila mtu ana sifa zake nzuri na mbaya, mambo mazuri na mabaya. Kwa maana hiyo basi si haki kuwalinganisha watu wawili tofauti kwa kuangalia vigezo vilevile wakati kila mmoja kaumbwa kivyake.
Angalia mambo mzuri, mambo unayoyapenda kwa huyu mpya, angalia upekee wake na ufurahia upekee huo. Kwa kufanya haya utakua umefanikiwa kusonga mbele kimahusiano na kimaisha na kama ni kisasi hakuna kisasi kizuri kama kufurahia na kufanikiwa zaidi. Achana na ya zamani, chakula kikishhatoka tumboni si chakul atena waachie inzi wale.