Wednesday, November 15, 2017

FIKIRI na Ujiulize Unaanzaje Kumponda Anayekupigania?


NIMEKEREKA hadi nimepoteza siku yangu, yaani kanikera hasa mtoto wa Kidigo, kama ningekuwa na uwezo ningemzabua vibao nijue moja, lakini nikifikiria jela, naona bora tu ninyamaze, ila nyie wenzie niwapashe mpashike!
Yaani mtoto wa kike kweli unathubutu kumwambia mumeo maneno ya kumkatisha tamaa, yanayomuonyesha yeye kuwa siyo mchakarikaji na kwamba anachokifanya kazi bure? Kweli? Hivi, jamani, unaanzaje sasa kusema maneno hayo?
Khaaa! Ona sasa, mihasira imenifanya hadi nimeshindwa kuwasabahi, mtanisamehe ndugu zangu, maana huyu mtu kaniudhi haswaaa.
Kaja barazani, nimempokea kama kawaida, najua hawa ndo wateja wangu, wapashkuna wenzangu, lakini mwisho wa siku tunapataga kitu cha maana cha kufanya au cha kuwaambia wenzetu huko mliko, sasa nimekaa mkao wa kula si ndiyo kaja na kimbwanga?
Kaanza, eti oooh nimefukuzwa kwa mume, kisa, nimemsimanga! Hee, umemsimangaje? Eti nimemwambia mume wangu hana akiba hata shilingi benki, hela yetu inaishia tumboni tu, hatuna cha kujidai!
Mh, nikamuuliza unaujua mshahara wa mumeo, kasema ndiyo, nikamuuliza unajua matumizi yenu yalivyo? Kasema najua, nikauliza tena, kwa hiyo unaona matumizi yetu hayamalizi mshahara wake, eti ooh, yanazidi!
Nikajua hapa naongea na juha, nikamu-uliza tena, hivi pale kwako na mumeo, wewe una ndugu wangapi
 na mumeo ana ndugu wangapi wanawategemea, kasema eti yeye anao watatu, mumewe hana ndugu!
Jamani, sasa mtu kama huyo wewe humchapi kibao kweli? Yaani mshahara wa mumewe anaujua, anafahamu kwamba kama siyo hela ya ziada anayotafuta, pasingetosha hapo nyumbani. Haya, achana na hiyo, humo ndani ya nyumba, ndiyo kwanza mke kajaza ndugu, halafu unamwambia mumeo eti huna hata akiba, fyuuutu!
Alinikera, nikamwambia nenda kwanza, hali yangu imebadilika ghafla, uje baadaye tuzungumze. Pale mwanzo nilikuwa sitaki kabisaa kuzun-gumza naye, maana nilimuona kama mchawi, lakini baada ya kufikiria sana, nikaona hapana, huyu anahitaji kufunzwa, ajielewe ili asije akaendelea na ujinga wake akajikuta anapoteza mume kizembe.
Lakini pia nikaona hili jambo lazima na nyie mlipate, maana inavyoonekana au huenda tabia hii mnayo pia.
Sikia, katika maisha ya ndoa, kitu cha msingi sana kwa mwanamke ni kuhakikisha mumewe ana amani naye kwa asilimia zote mia moja. Asiwe mtu mwenye kujisikia aibu, kinyaa, hasira au kinyongo kwa mke wake. Lazima tuwe na kauli ambayo siku zote inamuongezea hamasa na nguvu katika kutafuta uhai wa familia yenu.
Unapompa maneno ya kukatisha tamaa au kuudhi, unampa muda wa kukufikiria kwa mabaya. Atajiuliza amewasaidia ndugu zako wangapi, halafu wewe umewasaidia nini ndugu zake, ataangalia jinsi unavyoishi na nduguze hao, akiona kuna tofauti, basi lazima kichwa kitamuuma na kufikiria vitu vingine vibaya.
Hata kama hupendezwi na baadhi ya vitu kwa mumeo, kuna namna yake ya kumweleza ili uso wake uendelee kupambwa na furaha, amani na matumaini. Kauli za kuvunjana nguvu zinachangia sana migogoro katika ndoa.