Thursday, October 5, 2017

UNAPOANZA NA KUFAFNYA HIKI KATIKA MAPENZI NI MAKOSA

KUNA watu wanaanzisha mapenzi, kabla ya yote tayari wanazungumza kwamba katika uhusiano wetu tutakuwa hivi na vile, lakini kuna mwingine unamwambia tu unampenda, dakika tano zijazo tayari mnakwenda kukutana faragha. 

Wapo watu hawajihurumii kufanya mambo kama haya pasipo kujiuliza huyu ninaye ili awe nani.

Kuna wengine ngono wanaona kama kwenda haja ndogo na kurudi, si suala linalohitaji staha au mazungumzo ya kina kuhusu hatma yenu.

Je wewe ukoje? Ni vizuri kujiheshimu. Usijirahisi, onyesha msimamo. Usiwe mwepesi kuugawa utu wako ili umfurahishe huyo uliyenaye.

Wengine wanatoka kwao wakijua kwamba wana wapenzi, lakini wakifika sehemu za kazi, wanajirahisi, huyu akimtaka anakubali, hana msimamo, haya si maisha. Kama huyu mfanyakazi mwenzako, bosi wako anakutaka, je,   kawataka wangapi? Hili ni jambo la kujiuliza.

Wengi kati ya watu wa aina hii huachwa kwa visa. Ni kwa sababu wanaonekana ni watu wasio na misimamo kwa hiyo humthamini.

Mnaweza kuachana kwenye nyumba ya wageni, au unaweza siku unampigia simu mwenzi wako mliyekubaliana mkutane sehemu fulani, haji kwa wakati. Ni kwa sababu anakuona hufai.

Haiwezikani mwanamke kweli mwenye kujiheshimu, unamtongoza saa moja na nusu, saa mbili kamili mko kwenye nyumba ya wageni.

Tena wengine unaweza kuanza kwanza kutafuta sehemu ya kumpeleka kabla  ya kumhitaji, ni kwa namna tu anavyoonekana hajijali utu wake.

Kuna simulizi moja ni ya kweli, dada mmoja mrembo alikwenda baa kunywa, akakukatana na mwanamume, wakazungumza na kukubaliana waende nyumba ya wageni siku hiyo, lakini wakiwa chumbani mwanamke alidanganya anakwenda chooni, hakurudi, alikimbia.

Simulizi nyingine inahusu msichana aliyetongozwa na kujibu kuwa anachohitaji yeye ni mtu ambaye atakuwa mume na yeye awe mke? Aliendelea na msimamo huo hata baada ya kubembelezwa sana.

Je, kama wewe ni mwanamume ungeoa yupi kati ya hawa? Katika hali ya kawaida, mwenye busara angeoa huyu ambaye ameshikilia msimamo. Kwa sababu ni wazi hata baada ya kuoana atakuwa na msimamo.

Ninachotaka kusema hapa ni kuwa wengi wanaachana kwa visa kwa sababu anaona hana njia nyingine hasa kwa sababu labda anang�ang�aniwa na mtu ambaye hakuwa na sifa.

Japo watu wengine wanaachana labda kwa sababu amepata mwingine, lakini walio wengi wanaachana baada ya kubaini kuwa fulani hamfai.

Wengine pia huachana kwa sababu tu amepata mwingine, ambaye anaamini ni bora zaidi, ingawa wakati mwingine baada ya kujuana kwa kina, anaweza  kuwa ni mbaya zaidi ya yule aliyetaka kumuacha.

Ndugu, kama ambavyo huyo uliyenaye zamani ulikuwa ukimuona mzuri na sasa unamuona mbaya, huwezi kujua kuhusu huyu ambaye unataka kuwa naye baada ya kumuacha huyo wa sasa.

Ndipo huwa nashauri kuwa wakati mwingine kama uliyenaye si mbaya sana, ni vizuri mkaendelea kuwa naye. Mambo yanaweza kurekebishika na kuwa safi.

Fanya hivi hasa kama rekodi yake haionyeshi kuwa ni mtu mbaya, mfano kama mtu aliwahi kuwa na mke au ana mtoto lakini hamjali, huyo kama umeoana naye na ikatokea mmeachana, ni makosa makubwa kurudiana naye.

Dalili zinaonyesha ni mtu asiyefaa, ni vigumu kuishi vizuri hata kama mtarudiana.

Kimsingi ni vigumu kuishi vizuri na mtu ambaye tayari mliachana kisha mkarudiana.

Tafiti nyingi kuhusu jambo hili zinaonyesha kwamba ni vizuri kama tayari mmeachana na mtu, kila mmoja akaendelea na hamsini zake.

Wengi wa wale wanaorudiana hali ya mahusiano yao huwa ni mbaya zaidi ya zamani, hasa baada ya miaka miwili tangu kurudiana kwao. Kama ni visa  huwa ni zaidi.

Ninachotaka kusisitiza katika mada hii ni kwamba haijalishi una mwingine anayekushawishi kuachana na huyo wa sasa, au humtaki tu fulani, ni vizuri kuachana pasipo visa.

Hakuna sababu ya kuanza kumtangaza huyo mwenzi wako vibaya kwa watu ili tu aonekane ni mbaya, wakati pengine si mbaya, ila unataka kuachana naye kwa sababu zako.

Ndugu zangu hapa duniani tunapita, hakuna sababu ya kutendeana mambo mabaya. Jitahidi kuwa wazi, mwambie ukweli kwamba kweli nilikupenda, lakini hatuwezi tena kuwa pamoja kwa sababu hizi na zile.

Ni kweli ataumia, lakini ipi ni bora kuendelea na visa, au kumueleza wazi ajue moja, kama ni maumivu ya mara moja, iko siku yataisha. Ni vizuri kuelezana ukweli.

Lakini jambo moja la kujua ni kwamba ikiwa unamuacha mtu kwa sababu tu  ya kumnyanyasa, hana kosa lolote, unaweza kupata mtu ambaye atakuja kuwa mbaya kuliko yule ambaye umemuacha kwa kumuonea wakati anakupenda.

Kuacha mpenzi kwa sababu zisizo na maana, ni kujitafutia laana.

Ili kuepukana kuachana ni vizuri kabla ya kuanzisha uhusiano kujuana kwa kina, ridhika na nafsi yako kabla ya kuamua.

Zungumzeni kuhusu dini, maana wengine wanakaa weee baada ya muda ndipo wanaanza kusema, eeeh bwana dini yetu si moja, ndugu wamekataa tusioane. Siku zote mlikuwa wapi kuzungumzia hili?