Saturday, October 6, 2018

Tiba ya Wivu...

DAWA YA WIVU


1. ACHA KUJIFANANISHA
Kuna tabia ambayo huwatesa watu. Ni kujifananisha na watu wengine. Mfano; mwenzi wako ana ukaribu na mtu fulani, wewe badala ya kushughulikia tatizo ili amani ichukue mkondo wake, unaanza kumtazama huyo mtu halafu unajifananisha.
Pengine ukampima na kujifananisha kutokana na muonekano wako ukilinganisha na yeye. Unaweza pia kuweka kigezo cha fedha, ukajiuliza kama anakuzidi au unamzidi. Zaidi ya hapo, sura, mavazi na kadhalika vinaweza kukutesa akili. Acha tabia hiyo, wekeza upendo na mambo yatakaa sawa.
Huwezi kujifananisha na mtu mwingine, vilevile kwa mwenzi wako, haipendezi pia haitakiwi kumlinganisha na yeyote yule. Kila mmoja yupo tofauti kwa sababu kadhaa. Pamoja na ukweli kwamba suala la kumtazama mtu na kumuona anakuzidi linaweza kukupa unyonge lakini ni ujinga wa kupindukia.

Watu wengi husumbuliwa na mawazo kuwa wenzi wao wanaweza kuwaacha na kwenda kuanzisha uhusiano na wengine wenye ubora kuliko wao. Kama mpenzi wako aliwahi kuvutiwa na mtu mwingine kabla yako, huwezi kujua, muhimu ni kuzingatia kile ambacho amevutika kwako.

Zingatia kuwa endapo mwenzi wako angekuwa amedata kwa mtu mwingine tofauti na wewe, huwezi kujua lakini ukweli ni kwamba msingekuwa na uhusiano wa kimapenzi mlionao leo. Achana na mawazo yasiyojenga, amini kuwa mwenzako amedata kwako ndiyo maana leo mpo pamoja.

Jenga utaratibu mzuri wa kuheshimu jinsi mwenzako alivyo. Kadhalika jiamini kwamba duniani hakuna mtu bora kama wewe, kwa hiyo usiishi kwa kumuogopa mtu kutokana na fedha zake au sifa nyingine yoyote. Dunia imeumbwa na vitu tofauti, hivyo na watu wametofautiana, ingekuwa wote tunafanana, hakika ingekuwa ni
ulimwengu ‘unaoboa’ kuishi.

2. BADILI WIVU KWA HISIA CHANYA
Jifunze kutafsiri matendo yake kwa upendo. Vuta picha na ujipe hamasa chanya badala ya kuumia kwa kila atendalo. Katika hili, ni vizuri ukaongozwa na subira, kwani asili ya watu wenye wivu wa kupindukia, hukimbilia kupandwa na jazba badala ya kuuliza kwa utaratibu na kupokea jibu linalojitosheleza.

Hata siku moja usije ukadanganywa kwamba ukiwa mkali ndiyo utamfanya mpenzi wako asikusaliti. La hasha! Wekeza upendo kisha muishi kwa maelewano, hapo utaweza kumpa sababu ya kuishi kwa uaminifu. Utafiti unaonesha kuwa kundi la wasaliti wa uhusiano wao, huundwa na idadi kubwa ya watu waliochoshwa na migogoro ya kimapenzi.
Mantiki hapa ni kuwa mtu yupo kwenye uhusiano wake lakini anaamua kutoka nje baada ya kuona hana maelewano na mwenzi wake. Hivyo basi, ni vizuri ukawa unafuata hatua zinazofaa katika kupata ufumbuzi wa kila jambo unaloona halipo sawa kwa mwenzi wako, badala ya kugombezana. Itakugharimu.
Kama wivu wako unakufanya ujione wewe ni dhaifu, huna jambo la kufanya zaidi ya kuhakikisha unaishinda hali hiyo. Ukiwa na tabia ya kujiamini, itakusaidia kuufunika wivu, japo bado utaendelea kuwepo ndani yako lakini jinsi utakavyokuwa unashughulikia mambo yako na mwenzi wako, itakupa heshima zaidi.
Wivu ukizidi ni hatari kwa sababu unaweza kukuweka roho juu muda wote, ukaonekana mapepe na jamii ikakucheka kutokana na jinsi kichwa chako kilivyo rahisi kushika moto. Hii ina maana kuwa kudhibiti wivu ni kujiongezea heshima. Tafakari mwenyewe, unataka uheshimiwe au udharauliwe?