Monday, September 24, 2018

Natumaini muwazima bukheri wa afya na mnaendelea vyema na mishemishe zenu za kimaisha kama kawaida. Mimi namshukuru Mungu niko poa tayari kuwaletea mada ambayo nimewaandalia kwa wiki hii.Leo nimeona nikuletee njia kumi ambazo unaweza kuzitumia katika kukabiliana na wivu uliopitiliza ili uweze kudumu na huyo uliye naye.

1. Jiulize ni kwa nini una wivu
Sababu ya wewe kuwa na wivu inaweza kutokana na kitu kilichowahi kukupata hapo nyuma. Inawezekana uliwahi kuwa na uhusiano ukavunjika sasa unaogopa na huo usivunjike kwa kuchukulia poa kila unachokiona kwa mpenzi wako. Hiyo inaweza kukusababisha ukawa na wivu.

Mara nyingi kama mtu aliwahi kuwa na mpenzi ambaye alikuwa akimsaliti huharibu ubongo wake na kukaa na wasiwasi wakati wote kwa mpenzi anayeingia naye tena katika uhusiano.

Cha kufanya hapa ni kujitambua kwanza kisha ujifunze jinsi ya kukabiliana na wivu ulionao.

Kuna watu wengi ambao wana wivu lakini utawajua kwa matendo tu hasa wanapokuwa na wapenzi wao.

2. Usimhisi mpenzi wako
Kama utakaa chini na kuhisi kuwa mpenzi wako ana jambo analifanya nyuma ya pazia, utakuwa umepungukiwa na uaminifu.

Je, kuna kitu kibaya aliwahi kukufanyia kikakufanya ukose uaminifu kwake?
Kama ubongo wako uko sawa hauwezi kukufanya wewe ukawa na wasiwasi wakati wote.

3. Muulize maswali unapojisikia
Ni sahihi kumuuliza maswali mpenzi wako ili mradi uhakikishe hayatamtibua na kusababisha ugomvi. 

Hii itasaidia kuwaunganisha lakini jaribu kuuliza katika hali ya upole na ikiwezekana kwa lugha ya kimahaba. 

Kama utakuwa na wasiwasi jaribu kumuuliza maswali machache ambayo una wasiwasi nayo.
Usiwe ni mtu wa kupaniki wakati wote.

4. Usifananishe kila kitu 
Hupaswi kufananisha kila kilichotokea kwako au kwa mtu mwingine, wala usifananishe jambo alilolifanya mpenzi wako wa sasa na kile alichokufanyia yule wa zamani.

Kila mtu ana hulka zake na tofauti yake. Usiruhusu kuwa na woga kwamba patina wako anaweza kupata mtu mwingine wa kukuzidi wewe wala usifananishe kipato na muonekano wa mtu mwingine unayehisi anaweza kumchukua mpenzi wako. 

Ukithubutu kuruhusu hali hiyo, huwezi kukabiliana na wivu.
Kumbuka kuwa dunia imeumbwa na watu tofauti tofauti kama tutaishi kwa hisia kuwa fulani ana kipato anaweza kumchukua mpenzi wangu, basi dunia itakuwa si sehemu ya kuishi.

5. Wasiliana naye mara kwa mara 
Mawasiliano ni njia nzuri ya kuukabili wivu. Tumia muda mwingi kujadiliana na mpenzi wako ni kwa nini una wivu wa kupindukia. Kwa kufanya hivi unaweza kupunguza uzito wa tatizo la wivu.

Watu wengi wamefanikiwa kuficha wivu wao kwa kutumia njia hii na kama hutamweleza mpenzi wako jinsi unavyohisi wivu hatoweza kukusaidia.

Wengi wao hushindwa kuvumilia pale wanapowaona wapenzi wao wamekaa na mtu wa jinsi nyingine mapozi tata lakini kama utamueleza ni rahisi kukusaidia kwa kujirekebisha au kukufanya uzoee.

Ongea na mpenzi wako sana, gombana naye kidogo, hali hii itakwisha taratibu.

6. Kuwa na ujasiri/ jiamini
Wivu unaweza kuongezeka kama utakuwa hujiamini. Unahisi hujiamini? Unahisi mpenzi wako anaweza kukuacha? Kama maswali yote hayo yako kichwani kwako, unatakiwa kuyajibu na kuyafanyia kazi.

Kama mpenzi wako atakuwa ni mtu wa kujichanganya na watu mbalimbali hii haimaanishi kuwa atakuacha au hakupendi, jiamini na ujipe moyo wewe ndiyo chaguo lake.

Kumbuka kuwa kuna sababu ya yeye kukuchagua wewe na kuwaacha hao waliomzunguka.

7.Chukulia wivu ni adui yako
Ni sawa bila wivu kabisa uhusiano wenu utakuwa na matatizo lakini ukiona sasa unavuka mipaka ni vyema ukauchukulia kama adui wa penzi lenu.

Mpenzi wako atakasirika kuona unamuonea wivu hata katika yale usiyostahili kumuonea wivu, ataona unamboa na kuhisi huenda siyo mtu sahihi kwake. Uko tayari mpenzi wako ajisikie hivyo? 

Kama hauko tayari basi wakati mwingine uchukie wivu, uchukulie ni adui anayeweza kukufanya ukamkosa huyo mpenzi wako uliyempenda. Ukifanya hivyo taratibu utapunguza na kuwa na wivu wa wastani unaoweza kuliboresha penzi lenu.

8. Jenga uaminifu kwake
Ni kweli wivu kwa namna moja ama nyingine kunaufanya uhusiano wako uwe imara lakini sasa unaweza kuuimarisha uhusiano wako kwa kujijengea mazingira ya kumuamini mpenzi wako.

Endapo utajenga mazingira hayo ya kumuanimi utashangaa hata kiwango cha kumuonea wivu kiasi cha kumfanya kuona ni kero kinapungua.

Amini kwamba hata akiwa mbali na wewe hawezi kufanya kitu tofauti kinachoweza kukukwaza. Na kama utashindwa kumuamini mpenzi wako basi unatakiwa kujiuliza kwa nini kwani lazima kutakuwa na tatizo. 

9. Mpe nafasi ya kujiachia
Unapoingia kwenye uhusiano, wewe umekua na hata huyo mpenzi wako atakuwa ni mtu mzima. Itakuwa ni jambo la ajabu endapo utamzuia kujichanganya na wenzake kwa kuhisi anaweza kukuzunguka.

Kama umempenda basi huna haja ya kutumia nguvu nyingi kumchunga kwani  kumchunga kwako kunaweza kumkera na kuhisi hayuko na mtu sahihi licha ya kwamba yawezekana unafanya hivyo kwa nia njema. Mpe uhuru wa kujichanganya.

10. Jifunze kutoka kwa wengine
Wakati mwingine yaweza kuwa rahisi kwako kujua kwamba unachokifanya ni sahihi au siyo sahihi kwa kuwaangalia wapenzi wengine. Je, wao wanaonesha wivu wao waziwazi au umeshawahi kumsikia mmoja wao akilalamika kukerwa na namna mwenzake anavyomuonea wivu mpaka inakuwa kero?

Kama hujawahi kwa nini usione kwamba una kila sababu ya ‘kuikontroo’ tabia yako ya kuwa na wivu kupindukia. Wivu sawa, lakini kupitiliza ndiko kusikotakiwa na endapo hutakuwa mwepesi wa kubadilika penzi lako linaweza kunyauka hivi hivi ukiwa unaliona.