Saturday, July 14, 2018
Je.Umekata tamaa ya kupata mwenzi wa maisha
KATI ya vitu muhimu katika maisha ya binadamu ni pamoja na ndoa. Ni tendo la muunganiko ambalo linaongeza thamani, heshima na utu mbele ya jamii inayokuzunguka. Wengi wanatamani sana kupata wenzi.
Pamoja na ukweli huo, zipo changamoto ambazo husababisha kuchelewa kupata au kumpata mbabaishaji ambaye hana lengo la dhati.
Wapo wasichana warembo, wanaume watanashati sana, lakini kila wanapokuwa kwenye uhusiano, wanagundua kwamba wapo na watu ambao ‘bado wanazuga’. Hawana mpango wa kuingia kwenye muunganiko wa ndoa.
Hapo ndipo panapotokea kuachana. Rafiki yangu, kuacha, kuacha au kuachana mara kwa mara, kunasababisha sononeko la moyo. Kunakaribisha simanzi na mwisho wake, mhusika hukata tamaa ya kupata mwenzi wa maisha.
Inawezekana kabisa, hata wewe uko kwenye kundi hili. Aaaah! Usihuzunike, anza sasa kutabasamu, maana unakwenda kukutana na dawa baada ya kumaliza kusoma mada hii.
ANZA KUJIJALI
Maumivu ya kuachwa kila wakati, yanaweza kusababisha kutokujiweka ‘sopsop’, kitu ambacho ni tatizo kubwa sana. Sahau maumivu yote, angalia maisha yako yajayo. Rafiki yangu, hivi unadhani kama hujipendi, hujithamini nani atakupenda?
Ninaposema ujipende namaanisha ujipe upendo ule wa kawaida wewe mwenyewe kabla ya kuhitaji upendo wa mtu mwingine. Mwingine inawezekana hajitunzi, anavaa nguo chafu, hapigi pasi, nywele zipo timtim n.k
Nani atakupenda kwa misingi hiyo? Hakuna anayependa kuwa na mtu ambaye hana desturi ya usafi, kwanza hata kama ni mzuri kiasi gani unapokuwa upo rafu, hakuna mtu ambaye atausumbua moyo wake kuanza kukufikiria wewe usiyejipenda.
Siyo lazima wakati wote uwe ‘smati’, kwa kuwa inawezekana wengine wanafanya kazi ambazo zinawalazimu kuvaa nguo chafu, lakini baada ya hapo, unatakiwa kuwa katika hali ya usafi.
Upande wa wasichana siyo lazima uweke nywele zako dawa au usuke rasta wakati vitu hivyo huna uwezo navyo, unaweza ukasuka nywele zako vizuri au wakati mwingine ukanyoa mtindo mzuri unaokubalika ambao hautakuweka katika mtazamo mbaya kwa jamii.
Anza kujipenda kabla ya kuhitaji upendo kutoka kwa mtu mwingine, hiyo itakusaidia kuwa na mvuto na mwonekano mzuri kiasi cha kuweza kumpagawisha mtu mwingine kuanza kuhisi cheche za moto wa mapenzi katika moyo wake.
Safiri na neno hili, huhitaji tena mateso katika maisha yako. Sawa jamani? Haya, tuendelee.
KUJIAMINI NI MUHIMU
Hili ni tatizo la kisaikolojia zaidi kwa sababu kuna baadhi ya watu wanakosa kujiamini. Kuna mwingine anaweza akakaa kwenye kioo kwa saa kadhaa na kuanza kujitoa kasoro katika mwili wake.
Hujiona mbaya asiyevutia na ambaye hana thamani kabisa katika ulimwengu wa mapenzi, hujiona hawezi kupata mpenzi katika maisha yake yote baada ya kujitoa kasoro hizo. Mwingine hujiona ana matiti mabaya, mfupi sana, mrefu sana ana matege, ana makengeza na kasoro nyingine zozote ambazo huhisi ni kosa kuwa nazo.
Nani amekuambia kuwa una kasoro? Mshukuru Mungu kwa kukuumba jinsi ulivyo, amini kuwa Mungu ana makusudi yake kukuumba kama ulivyo.
Kuna watu wengine wanaweza kukupenda kutokana na hizo kasoro unazoziona katika mwili wako!
Kujitoa kasoro na kutojiamini ni kosa kwa kuwa unakuwa unajiathiri kisaikolojia na kujiona hufai kupendwa mwisho wa yote unakuja kumparamia mtu yeyote kwa nia ya kujiondolea mkosi na akishakutumia anakuacha solemba unabaki na machungu moyoni na kujiongezea matatizo zaidi.
Naamini baada ya kujipenda wewe na kujiamini kuwa unavutia, utakuwa katika hali ya kawaida kisaikolojia na wakati mwingine anaweza akajitokeza akupendaye na kukuomba hifadhi ya moyo wake kwako.
Sababu ya kukaa muda mrefu bila mpenzi au kutamkiwa kuwa unapendwa isiwe chanzo cha kupata maumivu mapya ya moyo. Kuachwa kwako, kusiwe chanzo cha kuingia kwa mwingine ambaye anaweza kuwa mwiba zaidi.
Acha papara, tulia, pata wasaa wa kumchunguza huyo anayedai anakupenda kwa muda wa kutosha kwa kuwa inawezekana naye akawa ni mmoja kati ya wale wanaotaka kukufanya chombo cha starehe!
Akikuhitaji kuwa na wewe (huyo mwanaume)lazima umchunguze kwanza na usiruhusu aujue mwili wako kabla ya kuelewa nia yake hasa kwako ni ipi; starehe ya muda mfupi au anakuhitaji kimaisha.
Usifanye mambo kwa papara, unahitaji utulivu wa kutosha ili uweze kumpata yule ambaye ni muhimu kwa ajili yako.
Ukijiamini na kuwa makini ni wazi kuwa utampata yule anayekupenda kwa dhati