Monday, July 9, 2018
Je,Ni sahihi kujiingiza kwenye penzi la muda ‘temporary love’?
mapenzi ni suala linalotakiwa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa ili yasije yakaleta madhara.
Yawezekana mwaka uliopita ulifanya makosa na ukampa nafasi mtu ambaye mwishoni alikutibulia furaha yako. Usifanye tena makosa!
Chagua mtu sahihi kisha hakikisha unampatia mapenzi ya kweli ili naye aweze kukupatia kile ulichotarajia kutoka kwake.
Baada ya kusema hayo sasa nirudi kwenye mada yangu. Nazungumzia mapenzi ya muda au wazungu wanaita ‘temporary love’. Inaweza ikatokea uko kwenye uhusiano na mtu ambaye ulimuahidi kumpenda daima na kwamba hutamsaliti.
Mpenzi wako huyo mnaishi pamoja lakini sasa inatokea mnatengana kutokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wenu. Wewe unabaki Tanzania mwenzako anakwenda masomoni Uingereza.
Katika mazingira hayo ni wachache sana wanaoweza kuvumiliana, wengi huwasaliti wapenzi wao kwa kuanzisha uhusiano wa muda na wa siri na mtu mwingine.
Inakuwaje?
Ilishawahi kutokea kwa rafiki yangu, mpenzi wake alipata nafasi ya kwenda kusoma Marekani. Baada ya muda mfupi akaniambia hawezi kukaa bila demu hivyo kuna kasichana kanajua kila kitu kuhusu uhusiano wao lakini kapo tayari kuwa naye kwa muda lakini kwa siri.
Nilijaribu kumsihi asimsaliti shemeji yangu lakini hakunielewa hivyo jamaa akaendelea na yule demu mpaka siku chache kabla ya yule mpenzi wake kurudi, ndiyo wakaachana.
Sasa hivi jamaa anaendelea na mpenzi wake kama kawaida na yule demu aliyekuwa naye kwa muda wanaheshimiana kama dada na kaka.
Nini madhara yake?
Kwanza katika mazingira haya inaonekana huyu mwanaume hana mapenzi ya dhati kwa mpenzi wake na endapo itagundulika kuwa alikuwa na mtu kwa muda, uhusiano wao hauwezi kudumu.
Lakini pia kuna uwezekano mkubwa wa mtu kunogewa. Mwanaume anaweza kunogewa na penzi la yule demu na huenda akabaini kuna vitu alikuwa akivipata kutoka kwake lakini mpenzi wake hana.
Hali hii inaweza kusababisha akamsaliti tena na kama waswahili wasemavyo kuwa muonja asali haonji mara moja, mwisho atachonga mzinga.
Pia watu wanapoanzisha uhusiano kwa muda ni vigumu kuachana moja kwa moja. Kwa maana hiyo mwanaume huyu anaweza kuutibua uhusiano wake kwa penzi la nje aliloonja.
Uhusiano wa muda ni sahihi?
Hauwezi kuwa sahihi hata siku moja na wanaofanya hivyo ni wasaliti ambao wanaweza kujikuta wanajiingiza kwenye matatizo makubwa.
Uvumilivu unatakiwa kuchukua nafasi yake. Kama mpenzi wako yuko mbali na wewe, mtunzie penzi lake. Ukiwa kiruka njia hata kama ni kwa siri Mungu anaweza kukuadhibu na ukajikuta unajuta.
Neno langu
Tuache ulimbukeni kwa kuwa na tamaa za kijinga. Kila unalomfanyia mwenzako kama ni baya jiulize na wewe ukifanyiwa na ukajua utajisikiaje?
Leo hii ukisikia mpenzi wako aliye mbali na wewe kaanzisha uhusiano na mtu mwingine eti kwa kuwa kashindwa kuzizuia hisia zake za mapenzi utajisikiaje?
Huwezi kujisikia vizuri na kama utachukulia poa basi utakuwa huna mapenzi ya dhati kwake.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo